Kimbunga Irma 'kitasababisha uharibifu mkubwa' Marekani

Kimbunga Irma kitaathiri sana jimbo la Florida au majimbo jirani, mkuu wa huduma za dharura wa serikali ya Marekani amesema.

Brock Long amesema maeneo ya Florida huenda yakakosa umeme kwa siku kadha na kwamba watu zaidi ya 100,000 huenda wakahitaji makazi.

Hayo yakijiri, taarifa zinasema kumetokea visa vingi sana vya uporaji katika kisiwa cha Caribbean cha St martin.

Kimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwa sana visiwa vya Caribbean, ambapo inakadiriwa kwamba watu 1.2m wameathiriwa.

Kwa sasa, kimbunga hicho kimepungua na kinaorodheshwa kuwa cha ngazi ya nne lakini maafisa wanasema kwamba bado ni hatari sana.

Idara ya taifa ya hali ya hewa Marekani imesema kimbunga Irma kinatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kwa kasi ya takriban 165mph (270km/h) mwishoni mwa wiki.

Watu 500,000 wametakiwa kuhama maeneo ya kusini mwa Florida, kimbunga hicho kikitarajiwa kufika huko Jumapili.

Idadi ya watu ambao wamefariki Caribbean inatarajiwa kuongezeka Ijumaa.

Kufikia sasa watu 19 wamethibitishwa kufariki.

Afisa mkuu wa ubalozi wa Marekani kisiwa cha Curacao amesema Wamarekani karibu 6,000 wamekwama kisiwa cha St Martin.

Watu tisa wamefariki na saba hawajulikani walipo maeneo ya Ufaransa ya kisiwa cha St Martin, ambacho sehemu moja yake humilikiwa na Uholanzi.

Mmoja amefariki katika kisiwa cha Sint Maarten kinachomilikiwa na Uholanzi.

Maafisa wa Ufaransa amesema asilimia 60 ya nyumba St Martin zimeharibiwa kiasi kwamba haziwezi kukalika tena.

Majeshi ya Ufaransa, Uingereza na Uholanzi yanasaidia kutoa misaada.

Mwandishi wa BBC Laura Bicker anasema uharibifu katika kisiwa cha Barbuda ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa.

Kimbunga Irma kinaelekea wapi?

Kimbunga hicho kilikumba visiwa vya Turks na Caicos na kusababisha pia mvua kubwa Jamhuri ya Dominika na Haiti.

Sasa kinaelekea Cuba na Bahamas.

Watalii 50,000 wanaikimbia Cuba, Reuters wamesema.