Suu Kyi alalamikia habari za uongo kuhusu watu wa Rohingya

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi amedai kwamba watu wamekuwa wakieneza habari za kupotosha kuhusu mzozo wa watu wa jamii ya Rohingya, ambao ni Waislamu, katika jimbo la Rakhine.
Watu wengi Myanmar ni wafuasi wa Buddha.
Akizungumza mara ya kwanza tangu kutokea kwa mzozo wa sasa, amesema hali ya wasiwasi imezidishwa na habari za uongo ambazo zinasaidia maslahi ya magaidi.
Bi Suu Kyi amesema hayo akizungumza kwa njia ya simu na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, afisi yake imesema.
Watu zaidi ya 123,000 wa jamii ya Rohingya wameikimbia Myanmar na kutorokea Bangladesh katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Suu Kyi amesema nini?
Taarifa ya karibuni zaidi ya serikali inasema Bi Suu Kyi amemwambia Bw Erdogan kwamba serikali yake "tayari imeanza kuwalinda watu wote katika jimbo la Rakhine katika njia bora zaidi inayowezekana".
Bi Suu Kyi amenukuliwa akisema: "Tunafahamu vyema sana, zaidi kabisa, maana ya watu kunyimwa haki zao za kibinadamu na haki ya kulindwa kidemokrasia.
"Kwa hivyo, tunahakikisha kwamba watu wote katika nchi yetu wanapata haki hizo zote, pamoja na haki, na sio tu za kisiasa, bali pia za kijamii na kulindwa kibinadamu."
Taarifa hiyo pia imesema kuna picha nyingi bandia ambazo zinaendezwa ili "kuzidisha matatizo kati ya jamii mbalimbali kwa lengo la kuendeleza amslahi ya magaidi."

Chanzo cha picha, Mir Sabbir/BBC
Ni habari za uongo?
Ni kweli kwamba kumekuwa na habari nyingi za uongo kuhusu yanayojiri Myanmar, nchi ambayo pia hufahamika kama Burma.
Kufikia 5 Septemba kulikuwa na ujumbe 1.2 milioni kwenye Twitter kuhusu mzozo huo tangu wakimbizi walipoanza kuvuka mpaka kuingia Banglabesh.
Nyingi zilikuwa na picha zilizodai kuonesha watu wakikimbia mapigano.
Tatizo ni kwamba, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC eneo la Asia kusini mashariki Jonathan Head, "nyingi ni za uongo".
Nyingi zilitoka maeneo mengine yaliyokumbwa na vita duniani. Moja iliyopakiwa na naibu waziri mkuu wa Uturuki Mehmet Simsek ni ya mauaji ya Rwanda ya mwaka 1994.

Watu 123,600 wamevuka mpaka na kuingia Bangladesh tangu 25 Agosti, kundi la Inter Sector Co-ordination Group limesema.
Pamoja na idadi ya watu wanaooneshwa kwenye ramani, kuna wakimbizi ziada 36,000 wanaoishi katika maeneo ya jamii nyingine na kwenye kambi ambazo hazijatambuliwa rasmi karibu na mpaka.
Kutokana na hilo, wengi wa watu walio nje wanalazimika kutegemea simulizi za watu wa Rohingya wanaotoroka Myanmar.
Hata hivyo, kinachofahamika kwa sasa ni kwamba mzozo wa sasa ulianza 25 Agosti wanamgambo wa Rohingya waliposhambulia vituo vya polisi. Jeshi, lilijibu mashambulio hayo.
Jeshi limesema linakabiliana na wanamgambo wa Rohingya wanaowashambulia raia.
Lakini jamii za Warohingya ambao wameingia Bangladesh wamekuwa wakidai kwamba wanajeshi , wakati mwingine wakisaidiwa na waumini wa Buddha, wamechoma nyumba za raia na kuwafyatulia risasi wakazi maeneo hayo.
Waziri wa usalama mpakani wa jimbo la Rakhine Kanali Phone Tint amekanusha taarifa hizo.
Hayo yakijiri, wadokezi wawili kutoka serikali ya Bangladesh wameambia Reuters kwamba wanaamini serikali ya Myanmay inatega vilipuzi vipya maeneo ya mpakani, licha ya watu wengi kutaka kuvuka mpaka kukimbilia usalama.
Kuliwekwa mabomu miaka ya 1990 na utawala wa kijeshi kuzuia watu kuvuka. Serikali hadi sasa haijasema iwapo kuna vilipuzi vipya vilivyotegwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu kusikitishwa na Suu Kyi?
Bi Suu Kyi alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa juhudi zake za kutetea kurejeshwa kwa demokrasia Burma, lakini sasa wanataka apokonywe tuzo hiyo.
Ingawa awali amekiri kuna matatizo jimbo la Rakhine, amekanusha kwamba kuna operesheni ya kuwaangamiza watu wa jamii ya Rohingya,
Watu wa jamii ya Rohingya wameungwa mkono na Rais Erdogan, na kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov, miongoni mwa wengine.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alikuwa Myanmar kukutana na Bi Suu Kyi Jumatano.
Alisema serikali yake ina wasiwasi sawa na wa serikali ya Myanmar kuhusu mapigano na chuki zinazoendelea jimbo la Rakhine.
Mwezi jana, Modi aliapa kuwafukuza watu 40,000 wa jamii ya Rohingya wanaoishi India.
Thailand hata hivyo inaonekana kuwa tayari kuwapokea watu wa jamii hiyo.

Chanzo cha picha, AFP

Chanzo cha picha, AFP/ Getty Images

Chanzo cha picha, Reuters












