Wahalifu wa Urusi walivyosaidia magenge ya dawa za kulevya Uingereza kutakatisha fedha

Ekaterina Zhdanova alitajwa na NCA kama mhusika mkuu katika mtandao wa kimataifa wa utakatishaji fedha

Chanzo cha picha, NCA

Muda wa kusoma: Dakika 6

Operesheni ya utakatishaji fedha ya mabilioni ya dola ambayo ilianzishwa wakati magenge ya Uingereza yalipokuwa yakihangaika kupakua pesa wakati wa amri ya kutotoka nje imefichuliwa na Shirika la Kitaifa la kupambana na Uhalifu.

Kugundua mtandao unaozungumza Kirusi uliopachikwa katika soko la dawa za mitaani nchini Uingereza ni mafanikio makubwa zaidi dhidi ya utakatishaji fedha katika mwongo mmoja, wadadisi wanasema.

Operesheni hiyo ya kimataifa, yenye makao yake makuu mjini Moscow, imekuwa ikichukua pesa chafu kutoka kwa magenge ya uhalifu kwa ada, na kuwaruhusu kuzibadilisha kwa fedha za mtandaoni zisizoweza kutambulika, kulinda wasiweze kugundulika. Mtandao huo pia umetumiwa na serikali ya Urusi kufadhili ujasusi.

Mtandao huo umeenea katika nchi 30, na watu 84 hadi sasa wamekamatwa, ikiwa ni pamoja na 71 nchini Uingereza, NCA na washirika wake waliwaambia waandishi wa habari katika mkutano mapema wiki hii.

George Rossi na Elena Chirkinyan waliwekewa vikwazo na Marekani siku ya Jumatano kutokana na kuhusika kwao katika mtandao huo

Chanzo cha picha, NCA

Waziri wa Usalama wa Uingereza Dan Jarvis alisema operesheni hiyo "ilimfichua kiongozi wa Urusi aliyejitajirisha kwa kufuja mali ya umma, magenge ya dawa za kulevya na wahalifu wa mtandao, ambao wote walitegemea mtiririko wa pesa chafu".

Siku ya Jumatano, Hazina ya Marekani iliidhinisha takwimu kuu za mtandao.

Ekaterina Zhdanova, mkuu wa mtandao wa fedha za kidigitali wenye makao yake mjini Moscow uitwao Smart, ametambuliwa kuwa kiini cha operesheni hiyo. Hapo awali aliorodheshwa na mamlaka ya Marekani mnamo Novemba 2023 kwa madai ya kuhamisha pesa kwa wasomi wa Urusi.

Bradley Smith, Kaimu Waziri anayeshughulikia masuala ya Ugaidi na Intelijensia ya fedha wa Hazina ya Marekani, alisema nchi hiyo "imesalia na nia ya kuvuruga juhudi zozote za Urusi kutumia mali ya kidijitali au miradi mingine haramu ya kifedha kujilimbikizia, kuhifadhi, na kuhamisha faida walizopata kwa njia isiyo halali" .

Rob Jones, mkurugenzi mkuu wa oparesheni katika NCA, alisema uzi unaounganisha wasomi wa Urusi, wahalifu wa mtandao wenye utajiri mkubwa wa pesa na magenge ya dawa za kulevya Uingereza "umekuwa hauonekani hadi sasa".

Yaliyobainika wakati wa janga la corona

Njia ambayo ilisababisha mtandao mkubwa na ngumu ilionekana wakati wa kufungwa kwa janga la 2021, wakati magenge ya dawa za kulevya kote Uropa yakijitahidi kuhamisha rundo la pesa kutoka kwa mauzo ya kimagendo hadi katika uchumi halali.

Hilo nalo lilifanya iwe vigumu kwao kununua bidhaa nyingi zaidi, kama vile kokeini kutoka Amerika Kusini.

NCA inasema mitandao miwili ya fedha za kidigitali iliyoko Moscow, inayojulikana kama Smart na TGR, ilitoa suluhisho.

Yote miwili ilijificha kwenye rundo kubwa la pesa za kificho kutoka kwa shambulio la ransomware. Hiyo ni aina ya ulafi mtandaoni ambapo genge hulemaza mifumo ya kompyuta ya shirika hadi lilipe ada ili kupata udhibiti tena.

TGR na Smart walipata faida kutokana na mashambulizi hayo na kuafikiana na mitandao ya madawa ya nchini Uingereza, na kuwapa njia ya papo hapo ya kubadilisha pesa chafu za mitaani kuwa rasilimali inayoweza kutumika.

Pesa zilikusanywa kote Uingereza kisha zikabadilishwa kwa fedha za kidigitali kutoka Moscow

Chanzo cha picha, NCA

Matokeo ya kuingia kwenye hatari ya kupokea pesa, mtandao unaoongozwa na Urusi uliitoza tume.

Mtandao wake wa wasafirishaji hufutilia mbali pesa hizo, na kuziweka kupitia biashara zinazoonekana kuwa halali kama vile kampuni za ujenzi nchini Uingereza na kwingineko, au kutumia njia za magendo kuzisafirisha hadi Dubai.

Hatimaye, pesa hizo ziliingia tena kwenye uchumi kwani zililipwa kwenye akaunti za benki kama faida inayoonekana kuwa halali.

Kwa kweli, Smart na TGR walikuwa wakiiga benki halali, kwa kutoza ada ndogo kwa kutoa mtandao wa kuhamisha pesa kutoka nchi hadi nchi.

Dokezo la kwanza lilikuja wakati polisi walipomsimamisha Fawad Saiedi, msafirishaji wa faida ya madawa ya kulevya, mwaka wa 2021. Alikuwa amebeba £250,000 kwenye gari lake.

Baadaye alikiri kuratibu uhamisho wa £15.6m za pesa chafu na akafungwa jela kwa zaidi ya miaka minne.

Fawad Saeidi, mtu wa kwanza kutambuliwa katika mtandao huo, alifungwa jela miaka minne

Chanzo cha picha, NCA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

NCA ilipochimba zaidi, waligundua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa Ekaterina Zhdanova, mkuu wa huduma ya ubadilishanaji wa sarafu ya digitali ya Smart huko Moscow.

NCA kisha ikagundua muundo wa uhusiano kati ya watu wanaohusika katika biashara ya dawa za kulevya na wale wanaohusika na sarafu za kidigitali. Pia waliona uhusiano zaidi na kundi maarufu la dawa za kulevya la Kinahan ambalo asili yake ni Dublin na msingi wake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Wasafirishaji wa faida wa madawa ya kulevya sawa na operesheni ya Saidi walikuwa wakikusanya pesa kutoka kwa magenge baada ya kuweka mfumo rahisi wa kuhakikisha kwamba wanaweza kuaminiana na kufanya uhamisho ufanyike haraka.

Mara tu pesa taslimu zilipothibitishwa kuwa zimepitishwa kwa msafirishaji, pesa sawia katika sarafu ya kidigitali, iliyotolewa na mitandao ya Kirusi ya Smart na TGR, ilitumwa kwenye akaunti za siri za mtandaoni za genge la dawa za kulevya.

Fedha hiyo kwa upande wake inaweza kutumika kununua kokeini kwa wingi kutoka kwa makampuni ya Amerika Kusini.

Wachunguzi waligundua kundi moja la wasafirishaji wakikusanya pesa kutoka maeneo 55 tofauti ya Uingereza kwa muda wa miezi minne kwa niaba ya takribani magenge 22 na dalili za mipango sawa na hiyo kwingineko barani Ulaya.

Semen Kuksov aliwezesha kuhamisha £12.3m

Chanzo cha picha, NCA

Mtandao mwingine wenye makao yake nchini Uingereza uliendeshwa na Semen Kuksov, mtoto wa mtendaji mkuu wa kampuni ya mafuta ya Urusi. Yeye na washirika wake walikusanya zaidi ya £12m ya fedha taslimu ya madawa ya kulevya katika muda wa wiki 10 tu ili kubadilishwa kwa sarafu ya mtandaoni. Februari mwaka jana, alifungwa jela kwa karibu miaka sita.

Kufikia sasa, NCA na washirika wake wamekamata pesa taslimu £20m, zinazohusiana na wastani wa £700m katika mauzo ya madawa ya kulevya na idadi kubwa ya waliokamatwa na mashtaka hadi sasa dhidi ya Saiedi na Kuksov.

Rob Jones kutoka NCA alisema: "Ikiwa wewe ni mtu ambaye sasa unataka kuhamisha pesa kutoka kwa biashara ya dawa za kulevya, ambayo imesababisha madhara makubwa nchini Uingereza, utafikiria mara mbili, kwa sababu hujui biashara hiyo itafikia wapi.

"Hujui kama tunawafuata, na hujui mapato hayo ya uhalifu yataishia wapi.

"Tunatarajia biashara hii itaenda wapi, na tutakuwa mbele na kusubiri."

Vikwazo na ujasusi

Vikwazo vya Jumatano vya Marekani ni hatua ya mwisho katika kufichua mtandao huo, kwa kuwalenga watu walio juu.

Ofisi ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ilisema kuwa imewatambua mkuu wa TGR, raia wa Ukraine mzaliwa wa Urusi George Rossi, anayejulikana pia kama Georgy, na wa pili mkuu wake, Elena Chirkinyan, raia wa Urusi.

Rossi amejionesha kuwa mfanyabiashara halali anayeishi London, lakini hajulikani aliko.

Hazina ya Marekani inasema Ekaterina Zhdanova na wanachama wengine wa mtandao wa TGR walitumia sarafu ya fiche na huduma za kifedha za Uingereza kuhamisha £2m kwenda Uingereza kununua mali kwa raia wa Urusi, ambaye hajatajwa hadharani.

NCA haijafichua ikiwa imechukua hatua kunyakua mali hiyo.

Hata hivyo, jukumu la madai ya Zhdanova katika kusaidia watu waliowekewa vikwazo ni sehemu moja tu ya kile NCA inasema ni uhusiano wake na Moscow.

Wachunguzi wanasema kuwa, mnamo 2022, serikali ya Urusi ilitumia huduma za kubadilishana fedha za Smart na TGR kuhamisha pesa za ujasusi.

Kisha, mwaka wa 2023, NCA inasema mpango huo ulisaidia jukwaa la vyombo vya habari la Russia Today linalodhibitiwa na serikali, lililopigwa marufuku nchini Uingereza, kuhamisha pesa taslimu nchini kwa moja ya shughuli zake.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga