Nini maana ya "milango takatifu" na kwa nini makanisa manane pekee duniani yana milango hiyo?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Juan Francisco Alonso
- Nafasi, BBC News World
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Mimi ndimi mlango; yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka ,ataingia na kutoka naye atapata malisho."
Kwa mamilioni ya Wakristo wa Kikatoliki, kifungu kutoka kwa Injili ya Mtakatifu Yohane (10:9-11) kitapata maana mpya kuanzia usiku wa sikukuu ya Krismasi, wakati Kanisa litaanza mwaka Mtakatifu au Jubilei ya 2025.
Kuanza kwa sherehe hii, ambayo itadumu hadi Januari 6, 2026, kutatanguliwa na ibada inayofanyika kila mwaka kwa zaidi ya karne sita: ufunguzi wa Mlango Takatifu na Papa Fransisko.
"Imefika wakati wa Jubilei mpya, kufungua mlango mtakatifu upya na kutoa uzoefu hai wa upendo wa Mungu, unaoamsha katika moyo tumaini thabiti la wokovu katika Kristo," aliandika Papa Fransisko katika waraka wake wa Spes non confundit (Tumaini halichanganyi), ambapo alitangaza tukio hili lenye asili yake katika Wayahudi.

Chanzo cha picha, Getty Images
San Pedro haikuwa ya kwanza
Pamoja na hija ya kuenda Roma na ziara kwenye makanisa ya Papa, kuvuka Mlango Takatifu ni mojawapo ya ibada maarufu inayofanywa na waumini wanaoshiriki mwaka wa Jubilei ili kupata msamaha (msamaha wa dhambi).
Lakini, nini maana ya mlango mtakatifu?
"Ni mlango wa kanisa ambao hufunguliwa tu wakati wa Mwaka Mtakatifu," alieleza Padre Fermin Labarga kwa BBC Mundo.
" Mlango ni kipengele cha jengo kinachotuwezesha kuingia mahali fulani.
Hivyo, Yesu mwenyewe ni mlango, na yeye ndiye anayetuongoza kwenye uzima wa milele, kitu ambacho ni mfano wa kipekee," aliongeza mtaalamu huyo ambaye ni profesa wa Historia ya Kanisa katika Chuo Kikuu cha Navarra (Hispania).
Ingawa kanisa la mtindo wa Kirumi ya Mtakatifu Petro huko Vatican ni hekalu kuu la Ukristo wa Kikatoliki, haikuwa ya kwanza kuwa na mlango mtakatifu.
" Mlango wa kwanza na wa zamani zaidi wa takatifu ni ule wa Basilika ya Mtakatifu Yohane Laterano, uliofunguliwa na Papa Martin V mwaka 1423," alisema Labarga.
Hekalu hilo, ambalo asili yake inarejea karne ya 4, ni la zamani zaidi magharibi na pia ni kanisa kuu la Roma.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, miongo michache baadaye, mwaka 1499, ibada ya Mlango Takatifu ilithibitishwa kama sehemu ya desturi za miaka ya Jubilei kwa kuwekewa mlango mmoja wa aina hii katika Basilika ya Mtakatifu Petro kwa amri ya Papa Aleksanda VI.
Papa wa pili wa familia ya Borgia pia aliamuru kufunguliwa kwa miingilio miwili zaidi katika basilika za Roma za Santa Maria Maggiore na Mtakatifu Paulo aliyetengwa nje ya kuta, ambazo zilikuwa tayari kwa mwaka wa Jubilei ulioadhimishwa mwaka 1500.
Miingilio ya makanisa manne ya Kipapa itafunguliwa na Papa Fransisko kwa mpangilio ufuatao: Kwanza itakuwa ile ya upande wa kulia kabisa wa uso mkuu wa Bazilika ya Mtakatifu Petro, inayojulikana pia kama "mlango wa msamaha mkubwa," na hii itafanyika tarehe 24 Desemba.
Halafu, tarehe 29, Papa atafungua ule uliopo katika Bazilika ya Mtakatifu Yohane Laterano. Kisha, tarehe 1 Januari 2025, atafungua ule wa Santa Maria Maggiore.
Na mwishowe, tarehe 5, mlango wa San Pablo Extramuros utafunguliwa, kulingana na ratiba iliyotolewa katika waraka wa kipapa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sio Roma pekee
Ingawa milango tu ya kwenye upande wa mbele wa makanisa ya Kipapa ya Roma na mlango mwingine wa muda katika gereza ndio utafunguliwa wakati wa Jubilei hii, angalau makanisa manne mengine duniani yana milango hii maalum.
Mbili kati ya milango hii pia zipo nchini Italia: moja katika Bazilika ya Santa Maria di Collemaggio, mjini L'Aquila; na nyingine katika kanisa kuu ya Utelekezaji wa Maria huko Atri.
Makanisa haya mawili, yaliyopo katikati mashariki mwa nchi ya Ulaya na yakiwa mbali chini ya kilomita 85, yanadai kuwa na milango ya kwanza inayojulikana ya takatifu.
Asili ya milango hii inaanzia mwaka 1294, wakati Papa Celestine V alitoa waraka wa kipapa ukitoa msamaha kwa yeyote atakayetembelea sehemu hizo takatifu kusikiliza misa na kuchukua Ekaristi, na kuingia kupitia milango fulani.
Ibada hii inajulikana leo kama Celestine Pardon (Msamaha wa Celestine), kulingana na tovuti za sehemu hizo za kidini.
Tofauti na Milango Takatifu ya Roma, milango iliyopo kwenye sehemu za ibada za miji hii miwili ya Italia haifunguliwi tu katika Miaka ya Takatifu, bali hufunguliwa kila mwaka, ingawa kwa siku chache tu.
Vivyo hivyo, ufunguzi wake unaweza kufanywa na Papa au kiongozi mwingine wa Kanisa atakayemteua kwa ajili ya lengo hilo.
Katika L'Aquila, hili hufanyika kati ya tarehe 28 na 29 Agosti, wakati katika Atri ni tarehe 14 ya mwezi huo huo.
Ingawa milango hii inaonekana kuwa ya zamani zaidi kuliko ile ya San Juan de Letran, Labarga ana shaka kuhusu hili.
"Waraka wa kipapa unaoanzisha Msamaha wa Papa Celestine V unadhihirika kuwa wa tarehe 29 Septemba 1294, lakini milango hii ni ya baadaye, pengine kutoka mwishoni mwa karne ya 15, kama nakala ya ile ya Roma," aliongeza mtaalamu huyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika eneo la Galicia na Marekani kaskazini
Nchini Hispania pia kuna mlango mwingine mtakatifu: ule ulio nyuma ya kanisa kuu ya Santiago de Compostela, mji mkuu wa mkoa wa kaskazini wa Galicia.
"Moja ya sehemu muhimu zaidi za kanisa kuu ya Santiago ni, bila shaka, mlango mtakatifu.
Kama milango ya makanisa makuu ya Roma huu pia hufunguliwa tu katika miaka ya takatifu.
Katika Santiago, Mwaka Mtakatifu hutokea wakati tarehe 25 Julai, siku ya sikukuu ya Santiago, inapojikuta kuwa Jumapili," ilieleza kanisa kuu ya Hispania.
Pia kuna siutafahamu kuhusu asili ya mlango huu.
"Wataalamu wengine wanadhani kwamba huenda kulikuwa na desturi ya kihistoria ya katikati ya karne, kabla ya ile ya miaka ya takatifu ya Roma, ingawa inawezekana zaidi kwamba Santiago ilichukua ibada hii kutoka Ukristo," ilisomeka sehemu ya habari kutoka kwa gazeti iliyotumwa kwa BBC Mundo na Idara ya Mawasiliano ya dayosisi ya Quebec.
"Inakadiriwa kwamba Mlango Takatifu ulijengwa mwanzoni mwa karne ya 16, chini ya Askofu Mkuu Alonso III de Fonseca, ambaye alikuwa na ufahamu wa ibada ya Kirumi iliyoanzishwa na Papa Aleksanda VI," iliongeza taarifa hizo.
Na mwishowe, kuna Bazilika-Katedrali ya Notre Dame ya Quebec (Kanada), ambayo ilifunguliwa mwaka 2014 kwa ruhusa ya Papa Benedikto XVI na ni ya pekee nje ya Ulaya.
Mlango Takatifu umefunguliwa kipindi chote cha mwaka 2024 kuadhimisha miaka 350 tangu kuanzishwa kwa dayosisi hiyo, ambayo ilikuwa dayosisi ya kwanza ya Kikatoliki nchini Canada, kama ilivyoelezwa na Idara ya Mawasiliano ya Dayosisi ya Quebec kwa BBC Mundo.
Kwa nini ni makanisa haya pekee yanayo na milango hii maalum?
"Kwa sababu papa waliotangulia wameamua hivyo," alieleza Labarga, ambaye alisema kwamba papa ndio wanao uwezo wa kuamua wapi mlango wa aina hii utawekwa.
"Katika miaka mingine ya Jubilei, papa walikuwa wakiamua kwamba kila dayosisi iwe na mlango wa jubilee katika makanisa yake au sehemu zake za ibada muhimu. Hii ilikuwa hivyo kwenye Jubilei ya awali ya mwaka 2015, iliyojitolea kwa Huruma," alikumbuka mtaalamu huyo.
Papa Fransisko alitumia tena uwezo huu na, katika tukio hili, aliamua kwamba katika gereza la Roma la Rebibbia kutakuwa na mlango mtakatifu ili wafungwa waweze kupata wokovu wa kiroho.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kilichomtishia Paul VI
Wakati mwaka mtakatifu hauadhimishwi, milango hubaki imefungwa na hadi si zamani sana, baadhi yake zilikuwa zimejengewa kuta za mawe.
Hata hivyo, desturi hii ya karne nyingi ilibadilishwa baada ya tukio ambalo lilimtia Papa hofu kubwa.
Yote yalitokea usiku wa Krismasi mwaka 1974, miaka 50 iliyopita.
Papa Paulo VI alikuwa akijiandaa kufungua mlango wa Bazilika ya Mtakatifu Petro na hivyo kuanza Jubilei ya 1975.
Papa huyu ambaye sasa ni mtakatifu aligonga ukuta unaofunika mlango mara tatu kwa nyundo ya fedha, huku akitamka sala kadhaa, kama inavyosema desturi, wakati ghafla kifusi kilidondoka karibu na yeye kwa sentimita chache.
Papa aliguswa kidogo tu, kulingana na video iliyotolewa na Vatican News, shirika la habari la Vatikani.
Ripoti za wakati huo zinasema kuwa mawe yalimpiga Papa Paulo VI, na kumjeruhi kidogo.
Kwa nini tukio hili lilitokea?
"Baadhi ya wafanyakazi walikuwa wakivunja ukuta wakati Papa alipoendelea na ibada, lakini baada ya tukio hili iliamuliwa kuufanya mchakato huu kuwa rahisi ili uwe wa haraka na usio na hatari," alieleza Labarga.
Hivyo, katika Bazilika ya Mtakatifu Petro, ukuta unaoziba mlango mtakatifu sasa huondolewa siku chache kabla ya kufunguliwa.
Katika Santiago, desturi ya ukuta iliondolewa ili kuepuka kifusi kuchafua au kuharibu sehemu za ndani za kanisa, ambalo limepitia mchakato mkubwa wa ukarabati katika miaka ya hivi karibuni.
Usiku huu wa Krismasi, macho ya Wakristo bilioni 1.4 yatakuwa tena kwa mlango ulioumbwa na mchongaji Vico Consorti mwaka 1949, ambao una paneli kumi na sita zenye vifungu vya biblia vinavyoanzia kufukuzwa kutoka Bustani ya Edeni hadi ufufuo wa Yesu.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla












