Je, Kwanini hatukumbuki maisha yetu tukiwa watoto wachanga?

Mtoto wa asili ya kiafrika akitazama juu akiwa amevalia fulana ya waridi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya Mtoto mchanga
    • Author, Maria Zaccaro
    • Nafasi, BBC World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Siku tulipozaliwa, hatua zetu za kwanza, na maneno yetu ya mwanzo ni matukio ya muhimu sana katika maisha yetu.

Hata hivyo, hatukumbuki hata mojawapo ya matukio hayo.

Kwa nini hali hii hutokea?

Kwa miongo kadhaa, wanasayansi wa neva na wanasaikolojia wamekuwa wakitafakari na kuchunguza swali hili.

Kutoweza kwetu kukumbuka matukio mahususi ya miaka ya mwanzo ya maisha hujulikana kitaalamu kama usahau wa utotoni (infantile amnesia).

Nadharia mbalimbali zimeibuliwa katika juhudi za kuielezea hali hii.

Profesa Nick Turk-Browne, mtaalamu wa saikolojia na upasuaji wa neva kutoka Chuo Kikuu cha Yale, Marekani, anasema kuwa mjadala huu kwa kiasi kikubwa unazunguka maswali makuu mawili.

  • Je, tunatengeneza kumbukumbu katika miaka ya awali lakini hatuwezi kuzipata baadaye?
  • Au hatutengenezi kumbukumbu kabisa hadi tunapokua?

Kwa mujibu wa Profesa Turk-Browne, hadi mwongo mmoja uliopita, watafiti wengi waliamini kuwa watoto wachanga hawatengenezi kumbukumbu.

Picha ya ubongo katika rangi ya samawati, yenye muundo mrefu ndani yake ukiwa umeangaziwa kwa rangi ya chungwa

Chanzo cha picha, Science Photo Library via Getty Images

Maelezo ya picha, Hipokampasi ni eneo lenye umbo la sfarasi wa baharini ndani ya ubongo ambalo lina jukumu kubwa katika kumbukumbu
Pia unaweza kusoma:

Baadhi walihusisha hali hiyo na ukosefu wa utambulisho wa nafsi au uwezo wa kuzungumza.

Nadharia nyingine inayoelezwa na Profesa Turk-Browne ni kwamba hatuwezi kutengeneza kumbukumbu hadi kufikia takribani umri wa miaka minne, kwa sababu hipokampasi—sehemu ya ubongo inayohusika na kuunda kumbukumbu mpya—haijakomaa kikamilifu.

Kuchambua ubongo wa mtoto

Hata hivyo, utafiti uliotolewa mapema mwaka huu na Profesa Turk-Browne mwenyewe unaonyesha matokeo yanayopingana na dhana hiyo.

Timu yake iliwachunguza watoto 26 wenye umri kati ya miezi minne na miaka miwili. Walioneshwa mfululizo wa picha huku shughuli za hipokampasi zao zikichunguzwa kwa kutumia teknolojia ya uchunguzi wa ubongo.

Baadaye, watoto walioneshwa picha moja ya awali pamoja na picha mpya, na watafiti walifuatilia mwelekeo wa macho yao ili kubaini ni picha ipi waliitazama kwa muda mrefu zaidi.

Ikiwa mtoto alitazama picha ya zamani kwa muda mrefu zaidi, watafiti walichukulia hilo kama ishara ya kuwa alikuwa ameikumbuka na kuweza kuitambua kama ilivyopendekezwa na tafiti zilizopita.

A baby wearing ear protectors sitting by a functional MRI machine, being held by her mother, with researcher Prof Turk-Browne opposite

Chanzo cha picha, 160/90

Maelezo ya picha, Prof Turk-Browne and his team have pioneered a way of scanning babies' brains while they are awake and active

Matokeo yalionesha kuwa, kadiri hipokampasi ya mtoto ilivyoonyesha shughuli zaidi alipoona picha kwa mara ya kwanza, ndivyo alivyokuwa na uwezekano mkubwa wa kuikumbuka baadaye hasa kwa watoto walio na umri wa zaidi ya miezi 12.

Hii inaashiria kuwa hipokampasi huanza kuwa na uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu ifikapo mwaka mmoja wa maisha.

Ziko wapi kumbukumbu zetu za awali?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Profesa Turk-Browne anasema kuwa utafiti wake ni "hatua ya kwanza" kuelekea kuthibitisha ikiwa watoto kweli huunda kumbukumbu kupitia hipokampasi, ingawa utafiti zaidi bado unahitajika.

"Kama tunazihifadhi kumbukumbu hizo, hilo linazua maswali ya kuvutia sana: Je, kumbukumbu hizo bado zipo? Je, zinaweza kufikiwa tena?" anauliza.

Utafiti wa mwaka 2023 ulionyesha kuwa panya waliokuwa wamejifunza njia ya kutoka kwenye mtaro wakiwa wachanga walikuwa wamesahau njia hiyo walipofikia utu uzima.

Hata hivyo, kwa kuchochea kimakusudi maeneo ya hipokampasi yaliyohusika na ujifunzaji wa awali, kumbukumbu hizo ziliweza kufufuliwa tena.

Ikiwa hali kama hiyo inaweza kutokea kwa wanadamu bado haijathibitishwa kisayansi.

Profesa Catherine Loveday, mtaalamu wa saikolojia ya neva kutoka Chuo Kikuu cha Westminster, Uingereza, naye anaamini kuwa watoto wachanga wana uwezo wa kutengeneza kumbukumbu angalau ifikapo wakati wanapoweza kuzungumza.

"Tunajua kuwa watoto wadogo hurudi kutoka chekechea na kusimulia yaliyojiri, lakini baada ya miaka michache hawakumbuki tena. Hii inaonyesha kuwa kumbukumbu huwa zipo tatizo ni kwamba hazidumu," anasema.

"Swali kuu ni kwa kiwango gani kumbukumbu hizo huhifadhiwa kwa muda mrefu. Je, zinatoweka haraka? Na je, ni kumbukumbu za fahamu ambazo tunaweza kuzifikiria na kuzitafakari kwa kina?" anaongeza.

Mtoto mchanga anayeendesha baiskeli ya mbao

Chanzo cha picha, ullstein bild via Getty Images

Maelezo ya picha, Haijulikani wazi ikiwa watoto wachanga hufanya kumbukumbu ambazo baadaye hazipatikani

Je, Kumbukumbu Zetu za Awali ni za kweli?

Kile kinachochanganya zaidi kuhusu usahau wa utotoni ni ugumu wa kubaini kama kile mtu anachokikumbuka kama kumbukumbu ya kwanza kweli kilitokea.

Watu wengi hudai kukumbuka tukio walipokuwa watoto wachanga au wakiwa katika kitanda cha mtoto.

Lakini Profesa Loveday anasema kuwa kumbukumbu kama hizo huenda si za kweli, bali ni matokeo ya ubongo kutengeneza picha ya tukio kutokana na hadithi walizosimuliwa au taarifa nyingine.

"Kumbukumbu huwa ni ujenzi upya kila mara. Ukipewa taarifa ya kutosha kuhusu tukio, ubongo wako unaweza kuunda kumbukumbu inayoonekana kuwa halisi kabisa," anafafanua.

"Kinachozungumziwa hapa hasa ni fahamu, na fahamu ni jambo gumu sana kulielezea au kulipima kisayansi," anaongeza.

Profesa Turk-Browne anaamini kuwa fumbo la usahau wa utotoni linagusa kiini cha utambulisho wetu kama binadamu.

"Ni suala la utambulisho wetu binafsi," anasema.

"Wazo la kwamba tuna pengo la kumbukumbu katika miaka yetu ya mwanzo, ambapo hatukumbuki chochote, linawafanya watu wengi kutafakari kwa kina kuhusu wao ni nani."