Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Changamoto kubwa zinazoikumba familia ya kifalme ya Uingereza
- Author, Sean Coughlan
- Nafasi, BBC
Familia ya kifalme imekuwa na mwanzo mgumu 2024, kutokana na matatizo ya kiafya na kuzungukwa na uvumi huu na ule.
Uvumi juu ya Princess wa Wales unaendelea. Hajaonekana hadharani mwaka huu, wakati huu akipata nafuu kutokana na upasuaji.
Kasri la Kensington liliweka wazi mwezi Januari tarehe za kupona kwa binti mfalme. Na kusema litatoa tu taarifa muhimu.
Siri kama sehemu ya utamaduni
Kila mtu ana haki ya faragha, lakini kwa watu mashuhuri, haswa wale wanaofadhiliwa na umma, kuna tofauti kati ya faragha na usiri.
Sehemu ya tatizo la sasa la familia ya kifalme ni mrundikano wa mambo yasiyojulikana; ugonjwa wa Catherine, saratani ya Mfalme Charles na suala la binafsi la Prince William.
Ni ukungu mzito wa kutokuwa na uhakika. Na hufanya uvumi mtandaoni kuongezeka. Ni tatizo pale watu wanapokuwa na taarifa zisizotosheleza, hupelekea kuuliza maswali zaidi.
Saratani ya Mfalme
Kutokuwepo kwa mkuu ni tatizo kwa taasisi yoyote. Mfalme anapata matibabu ya saratani na kwa hivyo inaeleweka hatohudhuria hafla za umma. Kupona ndio kipaumbele kwake na familia yake.
Lakini bado kuna shinikizo la kuonekana. Kuna mazoea ya muda mrefu kwamba ufalme unapaswa kuonekana ili uaminiwe uwepo wake.
Nyakati za kutopendwa kwa ufalme mara nyingi zimehusishwa na pale usipoonekana, kama vile wakati Malkia Victoria, akiomboleza kifo cha Albert, alijiondoa kutoka katika maisha ya umma.
Tarajia kuonekana zaidi Mfalme kwenye video - hotuba au klipu za mitandao ya kijamii, kama hivi karibuni alipoonekana akifurahia kadi za kumtakia afya njema.
Inafaa pia kuzingatia kwamba katika kesi yake, kura za maoni zilionyesha watu wengi wanaamini kiwango sahihi cha habari kilitolewa kuhusu saratani yake. Ni 13% tu waliotarajia maelezo zaidi, kulingana na kura ya maoni ya YouGov.
Andrew na Harry
Prince Andrew alikuwa kwenye kurasa za mbele tena za magazeti wiki hii, kikawaida habari zake huleta shida kwa familia ya kifalme.
Alikuwa akielekea kwenye ibada ya kumbukumbu ya Mfalme Constantine wa Ugiriki, akiongoza na timu ya akiba ya kifalme.
Na huenda atarejea kwenye vichwa vya habari kwa filamu ya mwezi ujao ya Netflix kuhusu mahojiano yake 2019.
Maswali kuhusu Jeffrey Epstein na Virginia Giuffre yatarudi tena kuisumbua familia ya kifalme. Amekuwa chanzo cha habari mbaya.
Naye Prince Harry amekuwa kiini cha mvutano mwingine wa muda mrefu ambao haujatatuliwa ndani ya familia ya kifalme.
Hakujawa na azimio la kudumu juu ya hadhi yake - tangu ahamie Marekani. Amegeuka kuwa kama mpinzani mahakama, mwanamfalme anayesubiri mustakbali wake na mtu asiyetulia.
Familia ya Kifalme hutakiwa kuwa pamoja, hata katika nyakati za mgawanyiko kama huo, lakini ni tatizo inapoonekana kuwa familia inatofautiana yenyewe.
Ufalme hauvutii kwa vijana
Familia ya kifalme ina ukosefu wa mvuto kwa vijana. Hilo lilionekana zaidi wiki hii - bila William au Catherine wakati familia ya kifalme ilipokusanyika kwa ibada ya ukumbusho huko Windsor.
Kinachofanya hili kuwa jambo baya zaidi ni ukosefu wao wa mvuto kwa vijana, tafiti nyingi zinaonyesha hivyo. Ni wazi kuwa kuna changamoto kubwa.
Hata kuwafikia vijana ni gumu kwa familia ya kifalme ambayo bado inatazama habari za kitamaduni za televisheni na kurasa za mbele za magazeti, ambazo hazipatikani kwa watazamaji vijana.
Ikiwa enzi ya heshima imekwisha, ufalme wa kisasa unapaswa kuzungumzaje na watu? Baada ya msimu wa baridi, familia ya kifalme lazima iwe na matumaini ya katika msimu wa jua.
Imetafsiriwa na Rashid Aballah