REGAN Vest: Ndani ya kizimba cha siri cha nyuklia cha Denmark

Lilijengwa kwa siri katika miaka ya 1960

Chanzo cha picha, Adrienne Murray Nielsen

Likiwa limefichwa katika Msitu wa Rold wa kaskazini wa Jutland, kama kilomita 400 kaskazini-magharibi mwa Copenhagen, ni jumba kubwa la Koldrigsmuseet REGAN Vest (Makumbusho ya Vita Baridi REGAN Magharibi).

Lilijengwa kwa siri katika miaka ya 1960 katika kilele cha mvutano wa Vita Baridi, hapa ndipo serikali ya Denmark na hata malkia wangehamishwa ikiwa vita vya nyuklia vingezuka.

Mpango ulikuwa wa kuendesha nchi kutoka ndani ya makazi haya, mita 60 chini ya ardhi, na kuwepo kwake kulinyamazishwa kwa miongo kadhaa hadi ilipofichuliwa hatimaye mwaka wa 2012. Baada ya miaka ya maandalizi, ilifunguliwa kwa umma kwa mara ya kwanza Februari 2023. kama makumbusho.

Ni wageni 50,000 pekee wanaoruhusiwa kila mwaka, na ufikiaji umepunguzwa kwa vikundi vidogo vya watu 10 kwenye ziara za kuongozwa za dakika 90.

Nilipotoka kwenye kituo cha gari-moshi katika mji mdogo wa Skørping, niliingia moja kwa moja kwenye teksi kwa safari fupi ya kwenda Rold Forest.

Dereva wa eneo hilo alikuwa hajawahi kusikia juu ya kizimba hicho cha ajabu, na bila ishara ya simu, tuliishia kuzunguka katika miduara kujaribu kuipata.

Kwa bahati nzuri, muda si muda tulijibahatisha kwenye barabara inayoelekea kwenye nguzo ya majengo meusi ya chuma na vioo yaliyofichika kwa sehemu kwenye mlima ambao ni makao ya kituo cha wageni mahiri.

Chini ya misitu mirefu na anga ya buluu yenye kung'aa, nilikanyaga njia fupi hadi kwenye lango la bunker, sehemu ambayo wakati fulani ingelindwa na polisi waliokuwa na bastola na mabomu ya kutupa kwa mkono.

Miimo ya milango ya zege iliyochafuka ilikuwa imegeuka kijani kibichi ikiwa na ukungu na unyevunyevu, na ilikuwa ya kawaida sana kiasi kwamba mtandao mpana wa handaki uliouficha ulikuwa wa kushangaza zaidi.

Kuta zilizopinda na zenye mbavu ziliundwa kupunguza kasi ya wimbi la shinikizo la mlipuko wa nyuklia

Chanzo cha picha, Adrienne Murray Nielsen

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Hii ilikuwa ni sehemu ya kutunza siri," alisema Bodil Frandsen, msimamizi wa makumbusho na mwanahistoria, aliponikaribisha ndani na mfanyakazi mwenzake, Lars Christian Nørbach, mkurugenzi wa makumbusho ya Jutland.

Kuingia kwenye handaki, nilihisi kana kwamba nilikuwa nikiingia kwenye ulimwengu wa siri. Sijawahi kuona mahali popote kama hapo.

"Sikiliza," alisema Nørbach, mlango ulikuwa ukifungwa, na kuziba miale ya mwanga wa asili na kutuma mwangwi unaorejea kwenye mtaro wa mita 300 mbele yetu.

Tulipoendelea kwenye njia iliyochongwa kwenye chaki na kilima cha chokaa. Utembeaji wa dakika chache tu nilihisi mrefu zaidi tulipofuatilia kuta zilizopinda, zenye mbavu ambazo ziliundwa kupunguza kasi ya wimbi la shinikizo la mlipuko wa nyuklia.

Hatimaye tulifikia jozi ya milango mizito, isiyopitisha hewa ambayo iliashiria mwanzo wa kizimba halisi. Kituo chetu cha kwanza kilikuwa chumba cha injini, ambapo jenereta za dizeli zingefanya kituo kiendelee kutumika.

Mara baada ya kufungwa kutoka kwa ulimwengu wa nje, kutakuwa na umeme wa kutosha, hewa iliyosafishwa na vifaa vingine kwa siku 10, alielezea Frandsen, akiifananisha na manowari.

Vita Baridi kilikuwa kipindi cha mvutano mkali wa kisiasa na kijeshi kati ya kambi za Magharibi na Mashariki, zilizoshikamana na Marekani na Muungano wa Kisovieti, ambazo zilianzia muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, na kusababisha mbio za umiliki silaha za nyuklia.

Baada ya majaribio ya Usovieti ya bomu la hidrojeni linaloweza kuwa janga - na baadaye mgogoro wa Kombora la Cuba - hofu ya Armageddon ilichochewa zaidi.

vifaa vya kizamani vimeachwa kwenye ofisi ambazo hazijaguswa

Chanzo cha picha, Adrienne Murray Nielsen

"Hujawahi kuona silaha kama hiyo," alisema Frandsen. "Ilikuwa na nguvu zaidi na ya kuumiza zaidi."

Mwanachama wa NATO tangu 1949, eneo la Denmark kwenye mdomo wa Bahari ya Baltic lilikuwa (na bado ni) muhimu kimkakati, lakini ukaribu wake na Pazia la Chuma yaani, kizuizi cha kisiasa, kijeshi, na kiitikadi kilichowekwa na Umoja wa Kisovieti baada ya Vita vya Pili vya Dunia ili kujifungia na washirika wake wanaoitegemea mashariki na kati wa Ulaya kutoka kwa mawasiliano ya wazi na Magharibi na maeneo mengine yasiyo ya kikomunisti, pia uliifanya iwe hatarini, ndiyo sababu nchi ilijiandaa kwa hali mbaya zaidi.

Ujenzi wa REGAN Vest ulianza mnamo 1963 na kukamilika miaka mitano baadaye.

Bonde la kuzuia nyuklia lililotokana na hilo lilikuwa la kushangaza lenye mita za mraba 5,500, yenye umbo la pete mbili kubwa, zilizounganishwa, kila moja ikiwa na sakafu ya juu na ya chini, na zaidi ya vyumba 230 ambavyo vingeweza kukaa karibu na wafanyakazi 350.

Mara nyingi hawa watakuwa mawaziri na watumishi wa umma, sehemu ya utawala duni uliopewa jukumu la kuendesha shughuli za taifa wakati wa giza kuu, pamoja na wafanyakazi wachache wa matibabu, waandishi wa habari kadhaa na kasisi.

Tulipokuwa tukipita kwenye ukumbi wenye giza, nilistaajabishwa na kuona ofisi ambazo hazijaguswa bado zikiwa na simu na vifaa vya kizamani, chumba cha mawasiliano na studio ndogo ya redio.

Mapambo mengi yalitokana na miaka ya 1960 na 1970, ikijumuisha viti vingi vya asili vya mbunifu mashuhuri wa Denmark Arne Jacobsen.

"Ni ulimwengu tofauti hapa," alisema Nørbach.

 Regan Vest ilijengwa mapema miaka ya 1960 katika kilele cha mvutano wa Vita Baridi

Chanzo cha picha, Adrienne Murray Nielsen

Na ndio maana REGAN Vest ni ya kipekee sana. majengo mengine ya serikali yapo, alielezea, lakini yamesasishwa, maudhui yameondolewa, au hayako wazi kwa umma.

Kwa bahati nzuri Vita vya Tatu vya Dunia havikutokea na kituo hicho kilitumika tu kwa mazoezi , ingawa kilibakia palepale hadi 2003, ambapo hatimaye kiliondolewa kwenye huduma.

Miaka tisa baadaye, siri iliyofichwa kwa muda mrefu ilifikia mwisho na kisha kukaja matayarisho ya karibu miaka kumi ya kuhifadhi jumba hilo kama jumba la makumbusho.

Ingawa nina kumbukumbu za Ukuta wa Berlin kuanguka, nikiwa mtoto wa miaka ya 1980, Vita Baridi ilikuwa enzi ambayo sijawahi kujua. Hatahivyo, kuingia kwenye "mahali hapo ilikuwa somo kuu. Ramani za kijeshi za Skandinavia na Muungano wa Sovieti zilifunika kuta, tayari kwa mikutano ambayo haikufanyika kamwe.

"Ukiangalia ramani, na kukumbuka jinsi mgawanyiko wa Ujerumani ulivyokuwa, basi Denmark ni nchi iliyo mstari wa mbele," alielezea Frandsen.

Huu ulikuwa wakati wa hofu, lakini pia utayari. Kuanzia vyumba vya chini vya ardhi katika shule za chekechea hadi ngome za kijeshi, takribani miundo 14,000 ya enzi ya Vita Baridi ilijengwa kote nchini Denmark - na nilishangaa kujua kwamba majengo mengine makubwa kama hilo ipo, inayoitwa Regan Øst (Mashariki).