Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kenji Nagai: Kamera iliyopotea miaka 16 yapatikana na matukio ya kuhuzunisha ya mwisho ya mwandishi wa habari nchini Myanmar
Ni taswira iliyoakisi kumbukumbu ya pamoja ya Myanmar ya ukandamizaji na athari zake.
Mwanamume mmoja wa umri wa kati alionekana ameshikilia kamera, huku akifyatuliwa risasi miguuni na mwanajeshi katika eneo la wazi huku waandamanaji wakikimbia kwa hofu.
Anaonekana akijiviringisha kwa kutumia mgongo wake, akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini bado ameshikilia kamera yake kwa mkono mmoja akiendelea kuchukua matukio.
Mpiga picha wa Reuters baadaye alishinda tuzo ya Pulitzer kwa kunasa tukio hilo.
Mwanamume huyo alikuwa Kenji Nagai, mwanahabari mkongwe wa Kijapani. Aliuawa tarehe 27 Septemba 2007, wakati wa kilele cha Mapinduzi ya Saffron, maandamano makubwa yaliyoongozwa na watawa wa Kibudha katika miji kadhaa nchini Myanmar dhidi ya utawala wa kijeshi ambao ulikuwa umetawala kwa miaka 45 na kuporomosha uchumi.
Kamera yake, iliyopotea kwa miaka 16, sasa imepatikana, ambapo familia yake ililazimika kusafiri kwa ndege hadi Bangkok wiki hii kwa ajili ya kuipokea.
"Nadhani kaka yangu alijiingiza katika msukosuko wa Mapinduzi ya Saffron, akiwa na hakika kwamba angeweza kuisaidia Myanmar kwa kuujulisha ulimwengu kinachoendelea," dadake Noriko anasema.
"Simfikirii kama shujaa ingawa alipoteza maisha. Ningependelea watu wamkumbuke kama mwandishi wa habari ambaye alikuwa tayari kuendelea kupigana."
Onyo - hadithi hii ina picha iliyoshinda Pulitzer ya Kenji Nagai muda mfupi baada ya kupigwa risasi.
Wakati Nagai, ambaye alikuwa anafanya kazi na AFP, aliwasili Myanmar wakati maandamano yalikuwa yakiendelea kwa wiki sita, changamoto ya kwanza kubwa kwa utawala wa kijeshi kwa karibu miaka 20.
"Polisi walitengeneza mistari mitatu kando kando ya barabara ya Sule Pagoda," anakumbuka Myint Yee, mwandishi wa habari kijana wa Burma ambaye pia alikuwa akipiga picha katika tukio hilo akiwa juu ya daraja.
"Wakati huo nilimwona Kenji Nagai akiwapiga picha askari wa vikosi vya usalama kwa karibu. Alikuwa na ujasiri sana. Nilisikia mlio wa kwanza wa risasi iliyopigwa hewani. Kisha askari wakaingia kwenye umati wa watu na kuanza kuwapiga. Nilisikia mlio wa pili wa risasi na kumuona Nagai akianguka chini. Baada ya hapo sikuona akijitingisha."
Wakaonekana wanajeshi wakibeba mwili wa mwanahabari huyo. Hakukuwa na dalili yoyote ya kamera yake ilikuwa wapi ama ilienda wapi, ambayo bado alikuwa ameishika wakati akidondoka.
Mwili wake uliporejeshwa Japan siku 10 baadaye na baadhi ya mali zake, kamera haikuwa miongoni mwao.
Familia ya Nagai na serikali ya Japan ilidai uchunguzi ufanyike. Lakini serikali ya wakati huo ya kijeshi ilidai kuwa aliuawa kwa risasi iliyopoteza muelekeo. Familia pia ilitaka kuombwa msamaha.
Miaka kumi na sita baadaye, na baada ya kifo cha mama yake, dada yake Noriko bado anasubiri. Pia aliendelea kuuliza kamera aliyokuwa ameshikilia wakati anauawa ilipo, ambayo familia ilitengeneza mfano wa camera na kuiweka kwenye kaburi lake katika mji aliozaliwa wa Imbari.
Familia ya Kenji Nagai inasema inatumai kuwa kupatikana tena kwa kamera yake, na video zenye kuhuzunisha zinazopatikana ndani yake, kunaweza kusaidia kufufua kampeni yao ya kifo chake kuelezewa, na hatimaye kuwajibika kwa vifo vingine vyote vya wale waliouawa wakati huo.