Kobbie Mainoo: Kiungo mchanga wa Man United anayeibuka kwa kasi

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kobbie Mainoo amefunga katika mechi za mfululizo baada ya kuifungia Manchester United katika raundi ya nne ya Kombe la FA
    • Author, Emma Smith na Simon Stone
    • Nafasi, BBC

Kiungo wa kati Kobbie Mainoo ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Enland baada ya kufanya vizuri msimu huu akiwa na Manchester United.

Mainoo, 18, awali aliachwa katika kikosi cha Gareth Southgate katika mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na Ubelgiji.

Majeraha na ukosefu wa wachezaji vilifungua milango kwa Mainoo kupata nafasi katika mipango ya mkufunzi wa United, Erik ten Hag mwishoni mwa 2023 - alipojitokeza kwa mara ya kwanza katika mechi hii dhidi ya Everton mwezi Novemba.

Mara moja alifanikiwa kucheza mechi 20, pamoja na kuanza mechi 14 kati ya 15 zilizopita.

Alifunga bao la ushindi dakika ya 97 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza wa 4-3 dhidi ya Wolves huko Molineux mwezi Februari.

Mchambuzi wa soka wa BBC, Ian Wright aliandika: "Kobbie Mainoo lazima awe katika kikosi kijacho cha Uingereza. Ukomavu wa namna hii katika mazingira magumu ambayo hatujaona kwa mchezaji wa Uingereza kwa muda mrefu. Ninavutiwa kila ninapomtazama."

Wepesi na kasi ya Mainoo viliwavutia wachambuzi siku ya Jumapili alipokuwa akiwapita wachezaji watatu wa Liverpool ili kutengeneza nafasi dakika ya 34 kwa Scott McTominay katika mechi waliyoshinda 4-3.

Mainoo ndiye nyota kijana wa hivi punde aliyeingia kwenye safu ya United na kucheza Ligi Kuu.

Kocha wake wa utotoni azungumza

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kasi yake inaweza kuwashangaza mashabiki wa United ambao wamemwona kama kiungo wa kati, lakini sio kwa wale ambao wamefuatilia maisha yake tangu umri mdogo.

Mainoo alianza maisha yake ya soka akiwa na timu za Cheadle na Gatley JFC huko Greater Manchester, akiwa na umri wa miaka mitano tu.

Steve Vare alimfundisha Mainoo wakati mchezaji huyo akiwa na umri wa miaka sita - na aliona hata wakati huo alikuwa na mtu wa kipekee mikononi mwake.

"Nimekuwa na watoto wengine ambao walikuwa wa kipekee katika umri huo ambao hawajafikia viwango vyake," Vare aliiambia BBC Sport.

"Ilikuwa dhahiri kabisa wakati Kobbie alipoanza kucheza alikuwa na nguvu, mwepesi, hodari awapo na mpira miguuni mwake. Ilinibidi nimpe changamoto kwa kuweka timu ya watoto wazuri zaidi kwenye timu nyingine ila kumpa changamoto. Nilianza kumchezesha dhidi ya wavulana wakubwa, ili kumpa changamoto.

"Katika umri huo, tayari alikuwa mwepesi sana. Alikuwa na nguvu, alikuwa imara, alikuwa mgumu kupoteza mpira.

Katika umri huo, mara nyingi ni kupiga mpira mbele na kukimbia, lakini yeye alikuwa akiuweka karibu sana na miguu yake. Mpira unakwama kwenye miguu yake.

"Unakuwa na watoto ambapo wanataka tu kucheza mpira na hawana hamu ya kufundishwa. Lakini Kobbie alikuwa na hamu ya kusikiliza na kujifunza.

"Nilijua ni lazima niweke wachezaji bora kwenye timu pinzani ili kujaribu kumpa changamoto. Angewapita wachezaji, akifunga mabao sita au saba.

"Tulikuwa tukimpa tuzo ya mchezaji bora kila mwisho wa msimu. Yeye ungeweza kumpa hata kila wiki."

Wachambuzi wa soka wamzungumzia

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kobbie Mainoo alisherehekea mbele ya mashabiki wa ugenini huko Molineux baada ya kuwapokonya pointi tatu

Vare alizungumza na baba yake Mainoo, Felix na kumwambia ampeleke mwanae katika kituo rasmi cha soka. Kinda huyo alijiunga na Manchester United na mengine ni historia.

Kuhusu vijana wanaocheza kwa sasa Cheadle na Gatley, ambapo Vare sasa ni mjumbe wa kamati, alisema: "Inampa kila mtu msukumo kwamba wanaweza kuwa kama Kobbie Mainoo."

Hadhi ya Mainoo ndani ya United ni ile ya kijana wa akademi aliyefanikiwa. Ni vazi ambalo amerithi kutoka kwa Rashford.

Na huko United wanaonekana kuwa wamegundua talanta ya Mainoo ambayo wataitumia.

"Utulivu anaouonyesha mtoto huyu katika kiwango hiki unaonekana sana katika mchezo wake. Katika timu ya vijana amekuwa akionekana kama mchezaji bora, na kuwepo katika kikosi cha kwanza bila tatizo ni ishara ya mtu ambaye ana kipaji kikubwa,” anasema mlinzi wa zamani wa United Rio Ferdinand kwenye TNT Sports.

"Sisemi ni mchezaji yule yule au ana uwezo sawa lakini ananipa msisimko kama wa Clarence Seedorf. Jinsi anavyoweza kufanya ujanja katika mazingira magumu na anavyocheza mpira na kutumia mwili wake wakati mwingine."