'Mtoto wangu alikufa baada ya boti yetu kusukumwa'

Yasmin Fatoum

Chanzo cha picha, Haryo Wirawan / BBC

Maelezo ya picha, Yasmin Fatoum, 25, alimpoteza bintiye kwenye boti

Na Astudestra Ajengrastri

Wakati Yasmin Fatoum aliposafiri kwa meli kuelekea Indonesia na watoto wake wawili wachanga, alikuwa na matumaini ya kutoroka mazingira duni na vurugu katika eneo la Cox's Bazaar la Bangladesh - kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, na nyumbani kwa Waislamu wa Rohingya wapatao milioni moja.

Lakini kabla ya mashua hiyo dhaifu aliyokuwa ndani pamoja na Warohingya wengine wapatao 250 kutua kwenye ufuo wa jimbo la Aceh, Bi Fatoum, 25, aliona ndoto yake ya maisha bora ikigeuka kuwa ndoto nyingine mbaya.

Wanakijiji wenye hasira, ambao wanaona wakimbizi kama shida kwa rasilimali za ndani, walizuia mashua na kuisukuma tena baharini mara mbili.

Picha za video ambazo BBC iliona zinaonyesha mwanamume wa eneo hilo akipaza sauti, "Huwezi kutia nanga hapa! Usitufanye tukupige!" huku wanawake na watoto wakilia wakiwa nyuma.

"Nilipowasili Indonesia kwa mara ya kwanza, nilikuwa na watoto wawili. Lakini walipoisukuma mbali mashua yetu, mtoto wangu mmoja alikufa kwa sababu alikuwa mgonjwa na hatukuwa na chakula chochote. Ilitubidi kuutupa mwili wake baharini," Bi Fatoum aliambia BBC, huku akizuia machozi.

Wakati mashua hiyo iliporuhusiwa kutia nanga baada ya siku kadhaa za kutokuwa na uhakika, wakaaji wake walilia. Wakiwa na utulivu kwa sababu safari yao ilikuwa imeisha, lakini pia kwa huzuni kwa kuwa walikuwa wamepoteza watoto wengine watatu kwenye boti kwa ugonjwa na ukosefu wa chakula.

Bi Fatoum ni miongoni mwa Warohingya 1,087 waliofika Aceh mwezi Novemba. Mkoa wa mashariki mwa Indonesia kwa sasa unahifadhi takriban wakimbizi 1,200 wa Rohingya, karibu nusu yao wakiwa watoto, kulingana na data kutoka UNHCR.

Warohingya ni kabila la wachache wasiotakikana katika Myanmar yenye Wabuddha wengi. Wengi wao walikimbilia Bangladesh mwaka wa 2017 kutoroka kampeni ya kile Umoja wa Mataifa umekitaja kama mauaji ya kimbari dhidi yao yaliyoanzishwa na jeshi la Burma.

Rohingya refugees return to a boat after locals turn them away.

Chanzo cha picha, Amanda Jufrian / AFP

Maelezo ya picha, Wakimbizi wa Rohingya warejea kwenye boti baada ya wenyeji kuwafukuza.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bi Fatoum na mwanawe sasa wanakaa katika ofisi ya uhamiaji ambayo haijatumika ambayo imebadilishwa kuwa makazi ya muda ya wakimbizi.

Wenyeji wanasalia na ukatili wa kutomkaribisha yeyote. Wanasema Warohingya wanachukiza imani yao ya kihafidhina ya Kiislamu kwa vile wanaume na wanawake ambao hawajaoana wanaishi pamoja katika kambi moja za wakimbizi.

Pia wanawashutumu Warohingya kwa kutodumisha usafi katika kambi za wakimbizi na kutumia Indonesia kama kituo cha kupita tu kuelekea Malaysia.

"Hawana shukrani," Suryani, mwenye umri wa miaka 48 wa eneo hilo. "Sisi ni wakarimu kuwachukua, lakini walitutemea mate na wakakimbia (kutoka kwenye makazi)."

Makumi ya wakimbizi wa Rohingya walipatikana wakiwalipa watu wanaosafirisha magendo pesa nyingi ili kuwachukua kutoka Bangladesh hadi Indonesia, na baadaye hadi Malaysia - ambapo wengi wao wanakuwa wafanyikazi haramu.

Mnamo tarehe 19 Novemba, polisi wa Aceh walimkamata dereva wa lori kwa kujaribu kuwasafirisha kinyume cha sheria Warohingya 36 nje ya jimbo hilo. Wakimbizi hao walikuwa wamechukua boti mbili kutoka Bangladesh kufika Aceh na safari ya lori ilikuwa sehemu ya usafiri wao kuelekea nchi nyingine, mamlaka inasema.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia ilisema kwamba "nia njema ya nchi katika kutoa makazi imetumiwa vibaya na mitandao ya magendo ya watu"

Kuongezeka kwa safari za mashua hadi Aceh

Aceh imeshuhudia mashua kadhaa za Warohingya wakiwasili tangu mwaka 2015. Waliowasili hivi karibuni wote wametoka Bangladesh, ingawa maafisa wanasema wameona ongezeko la mara kwa mara tangu mapinduzi ya kijeshi ya 2021 nchini Myanmar.

Warohingya wengi hujaribu kusafiri hadi Indonesia kati ya miezi ya Oktoba na Mei wakati upepo unapovuma, na kuruhusu boti zilizojaa kusonga mbele kwa kasi. Lakini ni nadra kuona waliofika wengi kama mwanzoni mwa Novemba. Wataalam wanatabiri boti zaidi zinaweza kufika katika miezi ijayo.

Mwakilishi wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa nchini Indonesia, Ann Maymann, alisema kuzorota kwa usalama katika eneo la Cox's Bazaar kunawalazimu Warohingya zaidi kutoroka.

"Wanaogopa. Ndiyo maana tunaona ongezeko," aliambia BBC.

Rohingya men and children looking out from a window in temporary shelter in Lhokseumawe, Aceh

Chanzo cha picha, ZIKRI MAULANA / AFP

Maelezo ya picha, Takriban Rohingyas 500 wamejaa katika jengo la wahamiaji ambalo halijatumika kama makazi ya muda.

Indonesia inawakubali Warohingya "kwa sababu za kibinadamu pekee" hata kama hailazimiki kufanya hivyo, kulingana na Lalu Muhammad Iqbal, msemaji wa wizara ya mambo ya nje. Nchi haijatia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi wa 1951.

"Makazi haya ni ya muda mfupi na si suluhu za kudumu," alisema, akisisitiza haja ya kutatua kiini cha tatizo nchini Myanmar.

Kando na kuongezeka kwa ghasia za magenge, Warohingya katika eneoCox's Bazaar wamelazimika kukabiliana na kupunguzwa kwa vocha zao za chakula za kila mwezi hadi $8 kutoka $12 Juni mwaka jana. Wiki kadhaa kabla ya hapo, Kimbunga Mocha chenye nguvu kiliharibu nyumba zao nyingi.

Rohima Khatoum, ambaye alifika kwa boti moja na Bi Fatoum mnamo Novemba, alikumbuka kuishi katikati ya magenge katika Cox's Bazaar kabla tu hajaondoka.

"Walitishia kuwaua watoto wetu, kuwabaka mama na binti zetu. Walimchukua mtoto wangu na kuomba pesa. Walimuua mtoto wangu mmoja na kutupa mwili wake," Bi Khatoum aliambia BBC.

Bi Khatoum alisema hali katika makazi ya Aceh ni bora zaidi kuliko huko Bangladesh.

"Nilikuwa na uhakika nitafia baharini," alisema, akikumbuka jinsi wenyeji wa Aceh walivyosukuma mashua yake kurudi baharini.

"Lakini niko hapa sasa na ninahisi afueni."

map of Aceh and Cox's Bazar

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi