Wakristo wa Gaza: Jinsi waumini hawa wanavyotafuta usalama kati ya makanisa mawili

Chanzo cha picha, AFP
"Mlipuko huo ulikuwa mkali, kama tetemeko la ardhi," Suhail Saba, manusura wa shambulio la Kanisa la St. Porphyrios huko Gaza, alizungumza na BBC usiku wa Alhamisi iliyopita.
Suhail anasema: “Kuta zilibomolewa na kurushwa huku na kule, nilisikia kelele za watoto na wanawake.''
Suhail ni katibu wa Baraza la Wasimamizi wa Kanisa la Othodoksi la Waarabu, alipata majeraha kichwani, mgongoni, na miguuni baada ya kombora hilo kuanguka na kuua watu tisa papo hapo wa familia moja.
Kwa sasa Suhail anaishi katika Kanisa Katoliki huko Gaza na mamia ya Wakristo wanaotafuta hifadhi katika makanisa mawili pekee ya jiji hilo.
Waliondoka makwao kuitikia onyo la jeshi la Israel, lakini baadhi yao wanajikuta hawana makazi tena.
Ubatizo wa watoto wengi
Oktoba 19, moja ya majengo ya Kanisa la Mtakatifu Porphyrus, pia linajulikana kama Kanisa la Kiothodoksi la Ugiriki, lilikumbwa na shambulio la kombora lililohusishwa na jeshi la Israel, lakini Israel ilikanusha kutekeleza shambulio hilo, ambalo lilisababisha vifo vya watu 17 na makumi ya majeruhi wakiwemo watoto.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Lior Hayat aliiambia BBC, ‘kilichotokea ni uharibifu usio wa makusudi baada ya Israel kufanya shambulio kwenye miundombinu ya Hamas ambayo ipo karibu sana na kanisa."
Kanisa la Saint Porphyrus, lenye uhusiano na jumuiya ya Kiothodoksi ya Ugiriki, na Kanisa la Holy Family, lenye uhusiano na madhehebu ya Kikatoliki, ndiyo makanisa mawili pekee yanayofanya kazi kwa sasa huko Gaza.
Takribani Wakristo 900 ambao wamehama nyumba zao wanajihifadhi humo tangu mwanzo wa mashambulio ya Israel katika Ukanda huo zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha ubatizo wa watoto wengi ambao walikuwa bado hawajabatizwa katika Ukanda wa Gaza, kwa hofu ya kuuawa katika vita vya sasa bila kubatizwa.
Munther Ishaq, Mkristo wa Kipalestina anayeishi Ukingo wa Magharibi, anasema, "Wakristo wa Ukanda wa Gaza wanajiandaa kwa hali mbaya zaidi."
Maisha ya Wakristo Gaza

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakristo ni wachache Gaza, idadi yao haizidi 1,100 - kutoka madhehebu ya Othodoksi ya Kigiriki na Kikatoliki. Wako chini ya asilimia 0.05 ya jumla ya watu wote.
Kwa mujibu wa muumini wa Kanisa la Kiothodoksi la Ugiriki la Mtakatifu Porphyrus, ambaye hakutaka jina lake litajwe, baadhi yao walifika Gaza kufuatia kuanzishwa kwa taifa la Israeli 1948 na wengine asili yao ni Gaza.
"Wamekuwa wakiishi katika ardhi hii tangu mwaka 402 baada ya kifo cha Yesu na walibadili imani kutoka upagani hadi Ukristo," anasema.
Elias Al-Jalda, mjumbe wa Baraza la Kanisa la Othodoksi la Kiarabu, anathibitisha kwamba Wakristo wa Gaza wapo huko kwa karne nyingi.
Hali za Wakristo katika Ukanda wa Gaza zinatofautiana na ndugu zao katika maeneo mengine ya Wapalestina kutokana na hali ngumu ya maisha kwa sababu ya mzingiro wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Ikiwa ni pamoja na ugumu wa kupata vibali vya kusafiri kwenda kutembelea familia zao nje ya eneo hilo au kusherehekea likizo nje ya Gaza.
Wakristo wa Gaza wanasemaje?
Reem Al-Jalda, mama wa watoto watatu, anayeishi katika Jiji la Gaza na familia yake. Reem hajamwona dada yake, anayeishi Ukingo wa Magharibi, kwa miaka mitano.
Dada yake Reem alihamia Ukingo wa Magharibi zaidi ya miaka ishirini na mitano iliyopita na kuolewa." Reem anasema: “Mume wangu hakupewa kibali cha kusafiri.”
Israel na Misri zimeweka mzingiro Ukanda wa Gaza tangu vuguvugu la Hamas kudhibiti eneo hilo, na wakaazi wa Ukanda huo hawaruhusiwi kuondoka bila vibali rasmi ambavyo vinapaswa kuombwa mapema.
“Wapwa zangu walioa, na kaka yao alihitimu chuo kikuu, ila hatukuweza kushiriki sherehe zao.” Reem anasema: “Tunajaribu kuwasiliana kupitia Intaneti, lakini haipatikani sikuzote. Tunatumiana picha zetu siku za likizo na kupiga simu za video.’’
Muumini wa madhehebu ya Katoliki, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia BBC: "Matatizo ya ukosefu wa utulivu, matatizo ya kisiasa na kiuchumi tunayoyashuhudia Gaza yanaathiri kila mtu."
Anaongeza kwa kusema, "tunafuata taratibu zetu zote za kidini, lakini katika namna tofauti na Wakristo wa Ukingo wa Magharibi na Bethlehem.’’
Miongoni mwa Wakristo mashuhuri katika Ukanda huo ni watawa wawili kutoka Peru waliokataa kuondoka Gaza - ni Maria del Pilar na Maria Vargas, pamoja na watawa wengine, wanasaidia zaidi ya wagonjwa 600, wazee, na watu wenye ulemavu.
Ubalozi wa Peru ulijaribu kupanga kuwaondoa, lakini walikataa kuondoka.
'Ugumu wa kuwasiliana na waumini wa madhehebu yao katika maeneo mengine ya Palestina, huathiri uhusiano wa kifamilia na kijamii,'' kwa mujibu wa na Elias Al-Jalda, mjumbe wa Baraza la Kanisa la Othodoksi la Kiarabu.
"Sisi ni wachache kwa idadi huku Gaza. Tunataka watoto wetu wafungue jumuiya ya Kikristo, wajue familia zao, na waishi maisha ya kawaida," anasema Elias.
Akibainisha kuwa shambulio la hivi karibuni liliuwa karibu asilimia mbili ya jumuiya ya Kikristo wa Gaza. Aliongeza kuwa miongoni mwao ni familia nzima ambayo ilifutwa katika sajili ya raia.
Changamoto katika makanisa

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Makanisa haya sasa yanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwapokea wakimbizi wanaofika makanisani na kuwahudumia.
Kwa mujibu wa Padri Youssef Asaad, naibu kasisi mkuu wa Kanisa la Holy Family, anasema kuna takriban watu 550 waliokimbia makazi na kwenda katika kanisa hilo kutoka maeneo tofauti ya Gaza, wakiwemo watu sitini wenye mahitaji maalumu na watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi kumi.
Padri Youssef anaelezea hali ngumu ya maisha: “Tuko katika jengo la shule, na hakuna vyumba vya kulala, bafu, blanketi, au kitu chochote.”
Kilichofanya mambo kuwa magumu zaidi ni kuhamishwa kwa makumi ya watu kutoka Kanisa la Kiothodoksi la Ugiriki baada ya kulipuliwa kwa kombora. Takribani watu mia moja walipoteza hifadhi, kulingana na muumini wa Kanisa la Othodoksi la Ugiriki.
Elias Al-Jalda anasema kwa sauti ya huzuni na hasira: “Tunajisikia kunyanyaswa na kukosa haki na hakuna ulinzi, kana kwamba tuko msituni.”
Reem anasema hajui ni nini kitatokea Gaza? Je, tutahamishwa? Nawafikiria watoto wangu. Natamani wangeondoka Ukanda wa Gaza na kufanya kazi nje ya nchi. Sisi tumezoea maisha haya, lakini kosa lao ni nini kuteseka nasi?"














