Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachojua kufikia sasa kuhusu raia wa Israel waliotekwa na Hamas
Idadi kubwa ya raia wa Israel na wanajeshi wanaendelea kuzuiliwa mateka na wapiganaji wa Palestina Hamas katika ukanda wa Gaza kwa mujibu wa jeshi la Israel.
Wengine wako hai na wengine wanakisiwa kuwa wamekufa, msemaji wa jeshi Luteni Kanali Jonathan Conricus alisema.
Watoto, wanawake, wazee na walemavu ni miongoni mwa waliotekwa, alisema.
"Hii ni idadi ambapo hadi sasa haiwezi kufikirika," alisema. "Huu ndio mustakabali wa vita hivi."
Hamas inasema idadi ya Waisraeli waliokamatwa ilikuwa "mara kadhaa" zaidi ya makumi na walikuwa wamepelekwa katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema Hamas inawajibika kwa ustawi wao na Israel "itamchukulia hatua yeyote atakayewadhuru".
Picha zinaonyesha Waisraeli wakichukuliwa kutoka majumbani
Kuna video nyingi zinazosambaa mtandaoni zikidaiwa kuwaonyesha Waisraeli wakiwa mikononi mwa wapiganaji wa Hamas.
Video moja iliyochapishwa ambayo imethibitishwa na BBC inaonyesha lori likiendeshwa katikati ya umati wa watu kwenye Ukanda wa Gaza, likidaiwa kuwa limebeba mateka wa Israel.
Nyingine, iliyoko katika eneo la Ukanda wa Gaza, inaonyesha mwanamke asiye na viatu akiburutwa kutoka nyuma ya lori huku mikono iliyo na damu imefungwa nyuma yake.
Wanandoa walichukuliwa kutoka kwenye karamu
Baadhi ya mateka wanasemekana kuchukuliwa kutoka kwenye karamu ya nje katika eneo la Kibbutz Re'im, kitongoji cha mji wa Ofakim kusini mwa Israel - sio mbali na Gaza.
Walioshuhudia waliambia vyombo vya habari vya Israel kwamba washambuliaji waliokuwa kwenye pikipiki walianza kuwamiminia risasi waliohudhuria, ambapo wengi wao bado hawajulikani walipo.
Video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo hazijathibitishwa na BBC, zinaonekana kumuonyesha mwanamke mmoja aliyehudhuria sherehe hiyo akitekwa nyara na kubebwa kwenye pikipiki na wanaume wawili.
Mwanamke huyo alitambuliwa na kaka wa mwenzi wake Moshe Au kama mwanamke wa Kiisraeli jina Noa Argamani.
Alikuwa ameripoti kutoweka kwake kabla ya kumuona yeye na kaka yake kwenye video hizo, wote wakiwa chini ya udhibiti wa wapiganaji kadhaa.
"Nilimwona Noa kwenye video akiwa na hofu na woga, siwezi kufikiria kinachoendelea akilini mwake hata kidogo - akipiga kelele kwa hofu kwenye pikipiki," Bw Or alisema katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Israel Channel 12.
Video ya baadaye - ambayo pia haikuthibitishwa na BBC - inaonekana ikimuonyesha akinywa maji kwenye chumba huko Gaza.
Hali za mateka katika miji ya Israeli
Nje ya Ukanda wa Gaza, vikosi vya jeshi la Israel vimeripotiwa kuwakomboa raia wa Israel waliokuwa wakishikiliwa mateka katika maeneo mawili kusini mwa nchi hiyo.
Huko Kibbutz Be'eri, mateka waliokuwa wamezuiliwa katika chumba cha maankuli waliokolewa baada ya saa 18, vituo vya televisheni vya Israel viliripoti.
Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zilidokeza kuwa hadi watu 50 walikuwa wameshikiliwa huko.
Akiongea na shirika la habari la Reuters, mwanamke aliyetambulika kwa jina la Ella alisema alikuwa amezuiliwa katika makazi yaliosheheni mashambulizi ya mabomu kwa saa nyingi katika mji huo.
"Tunaweza kusikia milio mingi ya risasi, tuliambiwa kuwa wapiganaji wako kwenye ukumbi wa kulia chakula, tunaweza kusikia milio mingi ya risasi," alisema.
"Nimepoteza mawasiliano na familia yangu, najua baba yangu ametekwa nyara ... hakuna mtu anayetuambia nini kinaendelea. Sijui kama mama yangu yuko hai."
Video iliyothibitishwa na BBC inaonyesha watu wakiongozwa kando ya barabara bila viatu na wanamgambo huko Be'eri. Haijulikani ikiwa watu hawa walikuwa mateka sawa na wale waliohifadhiwa kwenye jumba la maankuli.
Wakati huo huo, huko Kibbutz Urim, kitongoji cha mji wa Ofakim, Waisraeli wawili waliokolewa baada ya kutekwa na wanamgambo wa Hamas katika nyumba moja kwa saa za Jumamosi, kulingana na shirika la utangazaji la Israeli la Kan.
Watu wenye silaha walikuwa wameingia katika jiji hilo na kuwafyatulia risasi wakaazi walipokuwa wakitoroka mashambulizi ya mabomu mjini humo, vyombo vya habari vya Israel viliripoti.
Wakazi hao wawili walikuwa wamekaa katika nyumba yao, ambapo wanamgambo wanne kisha waliwateka.
Wapiganaji hao waliuawa baadaye na wanajeshi wa Israel.
Wanajeshi watatu wa Israel walijeruhiwa wakati wa uokoaji, Kan alisema.