Walalamika kuhusu gharama za juu za pombe Zanzibar

Alfred Lasteck

BBC Swahili

Wanamuziki wakitumbuiza

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/ BBC

Si watalii, si wenyeji lakini hata waandaji wa Tamasha la 21 Sauti za Busara wameeleza kuwa pombe kuwa gharama ya juu ilipunguza shangwe za tamasha hilo.

“Tamasha lilikuwa zuri lakini mwaka huu bei imepanda, kuna wasanii tuliwatarajia. Leo nakunywa maji, ukweli ni kuwa mimi si wa kunywa maji . Mimi nakunywa bia ya safari tena ya baridi lakini leo unaniambia bia shilingi 8,500 (Zaidi ya dola tatu za kimarekani), siwezi kununua nina watoto wanaosoma,” anaeleza Dominic Miyombilwa ambaye ni moja ya watu walioshiriki tamasha hilo.

Kwa upande wake, Najash Azali anasema kuwa amekuwa akiona tamasha la busara na kwasasa ananufaika nalo lakini bei ya vinywaji imekuwa kubwa na kupunguzia mvuto.

Alisema, “Sauti za Busara zilikuwa na mvuto sana na tulikuwa tukinunua bia kwa shilingi 1500 (chini ya dola moja) lakini sasa bia moja ni shilingi 10,000 (zaidi ya dola nne). Je unaona kama kutakuwa na furaha kwa wanywaji wengi kama mimii?.”

Wengi wa liiambia BBC, tatizo si kutopatikana kwa pombe kwenye tamasha bali ni kupatikana kwa gharama ya juu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions, Lorenz Herrmann aliieleza BBc kuwa upatikani hafifi wa vileo Zanzibar unafahamika na hivyo ilikuwa ni lazima vileo katika tamasha vipatikane kwa bei ya juu.

“Tunajua hali ilivyo, bei lazima ziwe juu lakini pombe zitakuwepo,” alisema Herrmann wakati tamsha hilo liiendelea.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, alisema kuwa tamasha hilo lilipokuwa likianza, msambazaji wa bia aliweza kupeleka maboksi 60 badala ya 100 yaliyokuwa yameagizwa.

Tangu januari mwaka huu, upatikanaji wa pombe visiwani Zanzibar umekuwa wa shida baada ya Serikali kusitisha kutoa vibali vipya kwa kampuni tatu zilizokuwa zikiingiza pombe visiwani Zanzibar.

Siku tatu za burudani visiwani

Wageni

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Maeneo mengi ya Mji Mkongwe kwa siku zote tatu mfululizo zilikumbana na pilika nyingi, kuanzia kwenye soko la chakula kwenye viwanja vya forodhani mpaka kwenye majukwaa ya ndani ya Ngome Kongwe.

Kila ukipita kwenye maeneo ya karibu tamasha hilo lilikuwa gumzo wengi wakiamini pia msimu wa 22 wa tamasha hilo utafana vilevile.

Wasanii 200 majukwaa matatu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kila siku jioni burudani zilianzia kwenye jukwaa la nje zilipo bustani za Forodhani ambapo kila mtu aliweza kupata burudani bila ya kulipa.

Giza linapozama, Sanaa ilikuwa ikiamia kwenye majukwaa ya Ngome ambapo burudani ilidumu mpaka usiku mnene.

Sholo Mwamba alikonga nyoyo za mashabiki wake siku ya kwanza wa tamasha na kuacha alama juu ya mziki wa Singele, mziki ulio na mizizi kwenye pwani ya bahari ya Hindi.

Sambamba, Medi Kuti, ambaye ni mjukuu wa Fela Kuti, msanii mashuhuru nchi Nigeria naye alivutia wengi huku wakimtaja kuwa moja ya wasanii wanaokuja kwa kasi barani Afrika.

Pia alikuwemo nyota wa Zimbabwe ambaye naye ni Mtoto wa gwiji wa mziki, Oliver Mtukudze, huyu ni Selmor Mtukudzi.

Tamasha hili maarufu zaidi la muziki kwa Afrika Mashariki, liliwakutanisha pia wasanii wengine kutoka Nigeria, Msumbiji, Afrika Kusini, DRC, Niger, Uganda, Zimbabwe, DRC, Uganda, Kenya na maeneo mengine ya Afrika.

Mwaka huu azma ya tamasha ni kutumia Muziki katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuweka uelewa mzuri wa mazingira kwaajili ya ustawi wa jamii.

Fursa kwa wenyeji

Wafanyabiashara

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Si hoteli, si kwnye migahawa, unapoambiwa hakuna nafasi basi wengi walikujibu kuwa Sauti za Busara nsiyo sababu kuu.

Awadhi ambaye ni mfanyabiashara wa chakula bahari alisema, “Nimekuwa hapa forodhani nikiuza chakula kwa zaidi ya miaka 20, uwepo wa tamasha la Busara umekuwa ni neema kwani tunauza chakula kingi haswa kwa watalii.”

Kwa upande wa watoa huduma za usafir, nao walidai kuneemeka na tamasha hilo.

“Sisi tunalipenda sana hili ni tamasha, ni fursa kubwa sana kwetu, tumekuwa na kazi nyingi sana na hilo limetupa fedha,” alisema Hassan Shafii dereva wa Taxi.

Siku tatu mfululizo za wageni na wenyeji walijumuika kuangalia na kuburudika kwa ala na sauti maridhawa za wanamuziki katika jukwaa la Ngome Kongwe.

"Nafurahi sana kuja hapa , ni kumbukumbu ya muda mrefu najiwekea. Muziki, chakula na mavazi yamenivutia sana na naweza kurudi wakati mwingine na watu wangu wa karibu," amesema Tim raia wa Marekani.

Sholo Mwamba

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Kwa mujibu wa baadhi ya makisio ya waandaji wa tamasha hilo, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, tamasha hili limeiingizia Zanzibar takribani Dola Milioni 70 za mapato

''Hili si tamasha la Zanzibar, hili ni tamasha la Afrika na Dunia, sisi ni wenyeji tu, hivi sasa kwa ukubwa wake hatuwezi kusema ni la wazanzibari kabisa'' amesema mwanzilishi wa tamasha Yusuph Mahmoud.

Kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, wandaaji wa tamasha hili wanapanga kupanda miti 10000, ambapo kila mwaka watapanda miti 2000.

Lengo lao kuu, ni kuhifadhi mazingira na kuhakikisha tamasha hilo linakuwa sehemu ya kuiweka Zanzibar salama kwa miaka ijayo.