Soko la Kariakoo lina umuhimu gani?

    • Author, Na Beatrice Kimaro
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania

Mzozo wa wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo unaendelea. Haukuanza jana wala juzi umekuwa wa muda mrefu. Na mgomo wanaoufanya sasa ni kuonesha wazi hisia zao baada ya kugugumia chini kwa chini kwa miaka.

Yapo mambo yaliyoanza kulalamikiwa miaka mingi, na miaka inavyokwenda ndivyo malalamiko yanavyozidi kuongezeka. Yapo yanayoshughulikiwa na Serikali na yapo yanayoonekana kusimika mizizi.

Pamoja na mambo mengine, wanacholalamikia wafanyabiashara wa soko hili ni usajili wa stoo zao za mizigo wasioutaka, tuhuma za rushwa kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wasio waaminifu, kamatakamata na kunyanyaswa na kikosi kazi ‘Task Force’ cha TRA, viwango vikubwa vya makadirio ya kodi na utitiri wa kodi.

Haya si mageni, yako Kariakoo, na yako nchi nzima yanayofanyika kwa namna tofauti.

Msingi wa malalamiko yote na mambo yote unaegemea kwenye ‘kukamuliwa’ mapato yao na hofu yao ya kufa kimitaji kutokana na kile kinachodaiwa na wakusanya kodi na ushuru ukilinganisha na kile wanachokiingiza.

Isivyo bahati yamefikia kutengeneza ‘uadui’ mkubwa kati ya wafanyabiashara na Mamlaka za kukusanya ushuru, tozo na kodi mbalimbali hasa TRA.

Historia na upekee wa Kariakoo

Soko la Kariakoo lipo tangu enzi za ukoloni. Eneo lilipo sasa katikati ya jiji, halikutengwa hasa kwa ajili ya soko. Inaelezwa Wakoloni wa Kijerumani walijenga hapo jengo maalumu lililokusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.

Lakini Vita vya Kwanza vya Dunia vikafanya matumizi yake kubadilika ikawa kambi maalumu ya wapagazi waliobeba mizigo kwa ajli ya vita hivyo waliojulikana kama Carrier Corps.

Baada ya vita pakaanza kutumika kama soko kwa meza chache za saruji. Jina la Kariakoo likazaliwa hapo, licha ya jengo lake la sasa kuzinduliwa mwaka 1975 na Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania.

Eneo lilipo, aina za biadhaa na biashara, muundo na muonekano wake, idadi ya wafanyabiashara na namna linavyounganisha biashara nchini na nje ya nchi linalifanya kuwa soko la kipekee kabisa katika Ukanda huu.

Ni soko lenye bidhaa za aina zote, za jumla na rejareja. Ni soko la kipekee ambalo kwa miaka na miaka limekuwa likikusanya maelfu ya wafanyabiashara Afrika mashariki na nchi nyingine nje ya ukanda huu. Soko hili si jengo tu, ukisema Kariakoo inagusa soko lenyewe na maduka lukuki kwenye mitaa yote ya Kariakoo.

Soko lenyewe limekuwa likiboreshwa kila wakati lakini maboresho ya sasa yatalifanya kuwa soko la kisasa zaidi kimuonekano. Litakuwa na ghorofa 6 zikiwemo mbili za chini ya ardhi. Serikali ilishatoa Sh bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wake unaohusisha ujenzi wa jengo jipya na ukarabati wa jengo la soko la zamani lililoungua Julai 2021.

“Hadi Februari, 2023, Sh4.16 bilioni zimepokewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu, sawa na asilimia 42 ya fedha zilizoidhinishwa,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 bungeni jijini Dodoma Aprili 14.

Ujenzi wa soko hilo unaojengwa na kampuni ya Estim Construction Ltd unatarajiwa kukamilika Oktoba 2023.

Umuhimu wa soko la Kariakoo na kwa nini Serikali inalipigania?

Kariakoo ni soko la Kimataifa, linalohudumia wafanyabiashara kutoka karibu nchi 11 Afrika. Zambia, Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda ni baadhi ya nchi tu zinazolitumia soko hili.

Ni mojawapo ya masoko makubwa na makongwe Afrika lenye kuzungukwa na maelfu ya maduka yaliyoko kwenye makumi na makumi ya mitaa. Ingawa soko linaloboreshwa sasa baada ya kuungua moto Julai 2021 litakuwa na wafanyabiashara zaidi ya 2,300, kwa makadirio ya macho eneo zima la Kariakoo lina wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wachuuzi wanaonufaika nalo kati ya 20,000 mpaka 50,000. Na huenda ikawa zaidi ya hapo.

Ni kiungo muhimu cha biashara za ndani na nje, ikiwa na mchango mkubwa wa katika uchumi wa Tanzania. Ukiacha kuhudumia wafanyabiashara karibu nchi nzima mapato yake yanakuonesha lilivyo soko muhimu kwa nchi.

Kwa wastani kwa mujibu wa ripoti, ni soko linaweza kuingiza mpaka shilingi bilioni 10 kwa mwezi. Mapato yanayozidi halmashauri nyingi tu Tanzania.

Na kwa umuhimu wake huo, hata Serikali ikaamua kuifanya Kariakoo kuwa mkoa wa kikodi ili kuwahudumia wafanyabiashara wake kwa ukaribu na kutatua matatizo yao ya kikodi kwa urahisi.

‘Hili ni soko muhimu sana kiuchumi, likitetereka hili, umeteteresha biashara nchi nzima, leo duka la nguo Moshi, Tanga, Dodoma, Tabora, Kigoma yani kila mahali zina nguo nyingi zimechukuliwa Kariakoo, ni soko muhimu hasa kwa nchi’, anasema Raphael Kugesha, mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa jamii kutoka Tanzania.

Kwa serikali yoyote haiwezi kuruhusu chanzo kikubwa cha mapato kama hiki kukutana na dhoruba. Kwa mantiki hii haikushangaza kumuona Waziri Mkuu akiacha shughuli zake zingine Dodoma zukiwemo za Bunge na kwenda kuwasikiliza wafanyabiashara hawa walioko kwenye mgomo.

Nini cha kufanya kunusuru soko la Kariakoo na biashara Tanzania?

Kiuchumi hili ni soko ambalo halipaswi kutofanya kazi hata siku moja. Kwa kiwango cha mapato yake, kufungwa maduka kwa siku moja ni kupoteza mamilioni ya fedha.

Kwa msingi wa mgogoro ulipo wa wafanyabiashara na mamlaka hasa ya Mapato japo kuna masuala ya elimu kwa mlipa kodi, ushirikishwaji na maboresho ya kisera za kodi, na kuongeza wigo wa walipa kodi ili kupunguza kuwakamua wachache, kuna muarobaini mmoja tu unaoweza kufanya kazi kirahisi na kuondoa mzozo baina ya TRA na wafanyabiashara sio tu Kariakoo bali nchi nzima.

Ni kurejesha bungeni na kuzifanyia marekebisho sheria za kodi zinazowapa nguvu TRA kufanya kazi zao. Licha ya dhamira yao njema, viongozi wa kisiasa kutoa matamko bado kunaleta ukakasi kama sheria inaendelea kubaki vile vile.

Ukusanyaji wa kodi kwa Tanzania unafanyika chini ya Sheria kuu, Kanuni na Sheria za Fedha.

Sheria za Fedha hutoa mabadiliko ya sheria za kodi ambazo zimefanyiwa maboresho kwa mwaka husika wa fedha. Lakini zipo sheria kuu za kodi zaidi ya 20 zikiwemo sheria Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438 R.E 2019, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 R.E 2019, Sheria ya Tozo za Huduma ya Bandari, Sura ya 264 R.E 2019 na Sheria ya Magari (kodi katika Usajili na kuhamisha umilki), Sura ya 124 R.E 2019.

Nyingine ni Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura ya 399 R.E 2019, Sheria ya Forodha (Usimamizi na Ushuru) [CAP. 403 R.E. 2019], Sheria ya Rufaa ya Mapato ya Kodi, Sura ya 408 R.E 2019 Sheria ya Serikali za Mitaa (Ukadiriaji), Sura ya 289 R.E2019 na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290 R.E 2019.

Usipobadilisha hizi, kauli yoyote itachukuliwa ni ya siasa. Mfano mzuri mwezi Juni, 2022 akiwa kwenye ziara yake mkoani Kagera Rais Samia Suluhu alitoa tamko lililoshangiliwa nchi nzima alisema ‘kuanzia sasa (TRA) msidai kodi madeni ya nyuma, achaneni na hiyo biashara, mnaloweza kufanya ni kurudi mwaka mmoja tu nyuma’.

Lakini kwa TRA tamko hili linaonekana ni la kisiasa, leo unakaribia mwaka sasa bado madeni ya nyuma yanadaiwa kama kawaida, ukirejea kauli ya r Rais Samia, maafisa wa TRA wanakueleza ni kauli za kisiasa na ushahidi hata mwenyekiti wa wafanyiashara wa Soko la Kariakoo, Martin Mbwana amelirejea hili mbele ya Waziri Mkuu, Majaliwa.

‘Hilo lililotamkwa na yeye ni agizo, leo TRA halafu mnamwambia mfanyabiashara huyo hilo ni agizo tu la kisiasa, lililotamkwa na rais wako hiyo ni dharau na ningetamani nimjue ni nani huyo, tushughulike naye mara moja’, alieleza Waziri Mkuu Majaliwa mbele ya wafanyabiashara wa Kariakoo kuonesha kuchukizwa nalo.

Hata baada ya kauli hii ya waziri Mkuu, kusisitiza alilolisema rais, wengi hawatarajii kubwa litabadilka kwa kuwa sheria na miongozo mingine ya kikodi iko pale pale na maafisa wa TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria.

‘Rais na waziri Mkuu wafanye kitu kirahisi sana, wamuagize waziri wa fedha apeleke marekebisho ya sheria bungeni, wanayoagiza yaingie kwenye sheria, mzozo umekwisha, anasema Lui Chuwa, mkazi wa Moshi.

Na kwa kuwa huu ni wakat iwa bajeti kuu kupitishwa kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, ni wakati muafaka wa kufanya hilo sasa, si kwa ajili ya Kariakoo, ukirekebisha sheria unagusa nchi nzima.