Mali na Burkina Faso: Je mapinduzi ya kijeshi yalisitisha mashambulio ya kijihadi?

Ghadhabu zilizoibuka kutokana na ukosefu wa usalama wa kudumu katika nchi za Afrika Magharibi za Mali na Burkina Faso zilifungua njia kwa wanajeshi kuziondoa serikali zilizoshindwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

"Hakuna nafasi tena ya kukosea," kiongozi wa mapinduzi ya Mali alisema wakati alipochukua mamlaka mnamo Agosti 2020.

"Tuna zaidi ya kile kinachohitajika kushinda vita hivi," aliunga mkono kiongozi mpya wa Burkina Faso mapema mwaka huu.

Lakini je, wananchi sasa wako salama zaidi?

Jibu fupi ni, hapana.

Katika nchi zote mbili, mashambulizi ya wanamgambo wa kijihadi dhidi ya raia yameongezeka.

Hali ndivyo ilivyo kwa vifo vya raia - watu wanauawa na na wanamgambo na wanajeshi.

"Hesabu za kila mwaka zinaongezeka mwaka baada ya mwaka," anasema Héni Nsaibia, mtafiti mkuu anayeshughulikia eneo la Afrika Magharibi la Sahel katika mradi wa Data ya Eneo la Migogoro na Matukio (Acled).

Data iliyotolewa kwa BBC na Acled mwezi Juni inalinganisha siku 661 kabla na baada ya mapinduzi ya Mali mwezi Agosti 2020, na siku 138 kabla na baada ya mapinduzi ya Burkina Faso Januari 2022.

Ili kukusanya data hii Acled inategemea mtandao wa "watoa habari na wataalamu" pamoja na ripoti za vyombo vya habari, lakini Bw Nsaibia anasema kufuatilia vurugu ni jambo gumu sana katika eneo la Sahel kwa sababu ya "taarifa za upotoshaji zinazoendeshwa na Urusi.

Majimbo yenyewe pia mara nyingine huwasilisha taarifa za uwongo kwa vyombo vya habari ili kuwafanya waonekane wamefanikiwa zaidi kuliko hali halisi ilivyo."

Urusi, ambayo inaunga mkono utawala wa Mali, imekuwa ikikanusha madai hayo.

Serikali ya Mali na Burkina Faso haijajibu maombi ya BBC ya kuelezea upande wao.

Mojawapo ya miezi iliyoshuhudia mauaji mabaya zaidi kuwahi rekodi ilikuwa Machi 2022. Acled anasema raia 790 waliuawa nchini Mali.

Baadhi ya raia hawa waliuawa na wanamgambo kutoka tawi la eneo la kundi la Islamic State huko Ménaka, kulingana na Acled, na kulikuwa na mashambulizi mengine madogo.

Lakini wengi wao walikuwa raia waliouawa katika mji wa Moura na jeshi la Mali, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakubali.

"Kulingana na ripoti nyingi, jeshi la Mali na mamluki wa Urusi waliingia Moura kutafuta kile walichodai kuvamia mkutano wa viongozi wa kijihadi.

Waliwashambulia raia na Umoja wa Mataifa ilisema kuwa waliwaua raia 500 katika kipindi cha siku tatu," linasema shirika la kimataifa la kushughulikia majanga. Mkurugenzi wa mradi wa Group (ICG) Sahel, Richard Moncrieff.

Mamlaka ya Mali imekanusha kuwa hakuna raia aliyeuawa huko Moura, ikisema ni wapiganaji wa Kiislamu pekee waliofariki.

Tangu wakati huo imezuia Umoja wa Mataifa kufika eneo hilo kufanya uchunguzi, na badala yake ikaanzisha uchunguzi wake.

Katika baadhi ya matukio wanaopigana na wanamgambo kwa niaba ya serikali hawajulikani - Burkina Faso kwa mfano ina wanamgambo wa kijamii wenye silaha, Bw Moncrieff anasema, ambao serikali serikali iliwapa jukumu rasmi mnamo 2020.

Wanamgambo kama hao katika eneo laSahel wanazidi kupewa jukumu la kukabiliana na tishio la wapiganaji wa kijihadi, lakini mara nyingi wanazidiwa nguvu na kuzidiwa idadi. Baadhi pia wameshutumiwa kwa kufanya dhuluma dhidi ya raia.

'Majeshi ya siri'

Mamlaka ya Mali inadhibiti kikamilifu hadi asilimia 15 ya eneo la nchi hiyo, kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo nchini Burkina Faso ni takriban asilimia 60 tu ya nchi ambayo iko chini ya udhibiti wa serikali, linasema jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi Ecowas.

Wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali na Burkina Faso wana idadi kubwa ya sila, wachambuzi wanasema.