Waridi wa BBC: Watu walijaa kwa wingi kuwashangaa wanawake wakipigana masumbwi

Chanzo cha picha, Eagan Salla/BBC
- Author, Na Eagan Salla
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Monica Joshua Mwakasanga mzaliwa Mbeya nyanda za juu kusini mwa Tanzania ndiye bondia wa kwanza mwanamke kwa Tanzania ambaye mpaka anashuka ulingoni mwaka 2012 kwa mara ya mwisho alikuwa amecheza jumla ya mapambano 68 na kupoteza matano tu huku mengine akipata ushindi au sare.
Safari yake rasmi kwenye ngumi za kulipwa ilianza mwaka 2000 baada ya bondia mkongwe nchini Tanzania, Omar Yazidu kutembelea kijijini kwao huko wilayani Kyela na kumshawishi kuingia kwenye ngumi na baadaye akamuandalia pambano lake la kwanza na pili ambayo yote alishinda.
“Namshukuru sana Omar Yazidu alinishawishi na kunifundisha kama mwezi mmoja halafu akaniletea bondia kutoka Dar es Salaam, anaitwa Theresia Kapinga na yeye lilikuwa pambano lake la kwanza nakumbuka tulichezea Kideko watu walijaa sana kushangaa wanawake wanapigana nilimpiga raundi ya nne na huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yangu” anakumbuka.
Baada ya pambano la kwanza, Monica alisafri na bondia mwenzake Theresia Kapinga hadi Blantaire Malawi ambako alipigana tena na kupata ushindi huku mwenzake akipoteza tena pambano kwenye raundi ya sita na huo ndiyo ukawa mwisho wake.
‘’Alisema tu kama utani mimi sitaki ngumi tena na kweli aliacha kama angeendelea basi tungekuwa mabondia wawili waanzilishi mpaka leo.’’

Chanzo cha picha, Eagan Salla/BBC
Jamii licha ya kuona uwezo na kipaji alicho nacho lakini bado haikuacha kumnyooshea kidole kana kwamba anafanya jambo la ajabu na lisilo stahili kulifanya kama mwanamke. Wapo waliokwenda mbali zaidi na hata kuwasema moja kwa moja wazazi wake kuwa haiwezakani mtoto wa kike kucheza michezo ya wanaume.
Kwa baba yake halikuwa jambo la kushangaza sababu alielewa fika wapi alipoupata ujasiri huo, kwani yeye mwenye alikuwa mwanamichezo alikuwa golikipa na bondia kwa muda mrefu nchini Zambia kabla ya kurejea nyumbani kwao Kyela mkoani Mbeya.
‘’Walikuwa wanakuja kwa baba, mtoto wa kike atawezaje kupigana, baba aliwajibu hata madereva ndege (marubani) wanawake wapo.”
Mapenzi yake kwa michezo yalianza akiwa msichana mdogo alishiriki michezo mbalimbali hata ambayo kwa wakati huo ilionekana kuwa ni ya wanaume tu lakini yeye bila aibu wala uwoga alikuwa akicheza mfano kuruka sarakasi, mpira wa miguu, kuruka vihunzi na hata baadaye alinza kucheza karate na kujipatia umaarifu mkubwa kwani alianza pia kuwafundisha na wasichana wengine.
Jina lake kwenye mchezo wa ngumi liliendelea kuwa kubwa zaidi kwa kushinda michezo ya kimataifa hasa alipompiga mpinzani wake Naomi Wanjiku wa Kenya, ambaye kwa wakati huo alikuwa tishio kwa Afrika ya Mashariki katika pambano lilipigwa viwanja vya Reli gerezani, Kariakoo Dar es Salaam.
“Kwa mwanamke kumpiga Mkenya na wakenya kama mnavyoona wanavyosifika kwa michezo nikampiga raundi ya nne basi safari yangu ya kuishi Kyela ikaishia hapo nikahamia Dar es Salaam rasmi.”
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa sasa Monica ambaye ana umri wa miaka 44 na ni mama wa watoto watatu, ni mwamuzi rasmi wa ngumi nchini Tanzania akiwa miongoni mwa waamuzi takribani hamsini wa sasa, japo baada ya kustaafu masumbwi aliwahi pia kuhudumu kama askari bandarini.
Monica anafurahi kuona mchezo wa ngumi ulipofika kwa sasa mabondia ni wengi na faida ni kubwa.
Anasema kuna wakati anatamani wakati ungerudi nyuma ili aendelee kupigana huenda walau angeambulia chochote kitu, kwani wakati wake alikuwa akicheza zaidi kwa mapenzi na si fedha na hata alipolipwa basi malipo yalikuwa madogo sana kiasi kwamba hakuweza kufanya lolote la kimaendeleo kwa kipato hicho.
‘’Wenzetu wa sasa hivi wao ndiyo wamebahatika, ukipata sasa hivi mchezo usipojenga ni upumbavu wako, mfano mimi nilivyokuwa ninacheza zamani kwa shilingi elfu ishirini thelathini nitajengaje, unalipwa elfu ishirini, elfu thelathini za kitanzania utajenga?’’
Pamoja na shughuli zake kama mwamuzi, bondia huyu mstaafu ambaye pia ni shabiki mkubwa wa mchezo wa mpira wa miguu anayeishabikia timu ya Young Africans ‘Yanga’ maarufu ‘wananchi’, amekuwa akitumia muda wake wa ziada kuwafundisha vijana wa kike na wa kiume mchezo wa ngumi
‘’Nina vijana takribani 20 wa kike na wakiume lakini tatizo ni vifaa ninapokwama nawatuma kwa walimu wengine wenyo vifaa zaidi mfano Mlundwa (Emmanuel)”

Chanzo cha picha, Eagan Salla/BBC
Monica anasema serikali ya Tanzania imewasahu mabondia wa zamani licha ya ahadi za mara kwa mara za kuwasaidia vifaa ili waibue na kuvinoa vipaji lakini wakati wote imekuwa ni kauli isiyo na utekelezaji, jambo linalowavunja moyo na kujiona hawana thamani licha ya majina yao kuimbwa kama waasisi wa ngumi nchini Tanzania.
‘’Kuna wakati tunazungumza na wenzetu wa mataifa mengine wanakuambia namna wanavyopewa nguvu na nchi zao unaumia na kutafakari tu’’
Monica alifanikiwa kumrithisha mikoba ya ngumi binti yake aliyekuwa akiitwa Salome lakini isivyo bahati alifariki dunia ghafla.
“Nina Watoto watatu, wa kwanza ndiyo alikuwa bondia mzuri sana bahati mbaya ametangualia mbele za haki katika mazingira ya kutatanisha, ghafla tu. Yule ndiye alikuwa bondia mzuri na amecheza sana, alikuwa anaitwa Salome”
Vijana anaowafundisha sasa kila mmoja kwa namna yake anamsifu kwamba licha ya umri wake bado ana nguvu na pumzi na uwezo mkubwa kimbinu lakini changamoto kubwa waliyonayo ni ya vifaa.
Imehaririwa na Florian Kaijage












