Kwa nini Wakenya wanaandamana tena?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Maelfu ya wakenya wameingia mtaani leo kuandamana. Ni muendelezo wa maandamano yaliyoanza juma lililopita kwa uchache, lakini ya leo yanaonekana kuwa na sura na picha kubwa kuzunguka kifo cha mwanablogu wa Kenya Albert Ojwang aliyepoteza maisha akiwa kizuizini.
Kifo chake akiwa anashikiliwa na maafisa wa polisi kimeendelea kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya, wengi wakishinikiza waliohusika na mauaji hayo wawajibishwe kisheria.
Japo, kuna kesi inaendelea Mahakamani, kuna waliokamatwa na kujiweka kando, kupisha uchunguzi, lakini hiyo haijawatosha wakenya, ambao leo wameingia tena mtaani.
Kifo cha Ojwang ni kisa cha punde zaidi kuchunguzwa na iIdara za usalama za Kenya baada ya miaka kadhaa ya mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu kwa njia ya kutatanisha.
Rais wa Kenya, William Ruto amekuwa akiahidi kukomesha vitendo hivyo mara kwa mara licha ya hasira ya umma inayoongezeka. Wiki iliyopita kifo cha Ojwang kilipotokea Rais Ruto aliwaomba Wakenya wawe na subira wakati uchunguzi ukiendelea.
Licha ya wito huo waandamanaji wamejitokeza katika mitaa ya jiji la Nairobi wakiongozwa na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kupinga mauaji ya mwanablogu huyo.
Je, hii inaashiria nini kuhusu juhudi zinazofanywa serikali kushugulikia malalamiko yao?
Kifo cha Albert Ojwang

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata kabla ya mauaji ya Albert Ojwang, vijana nchini humo wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kujiandaa kwa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu maandamano ya Juni 25, 2024 kupinga muswada wa fedha wa 2024, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya vijana hao wamekuwa wakiiomba serikali kutangaza Juni tarehe 25 kila mwaka kuwa siku kuu ya kitaifa lakini Msemaji wa Serikali Issac Mwaura ameweka bayana kwamba siku hiyo ni siku tu kama nyingine yoyote ya kawaida.
Mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang ambaye alikuwa akiandika kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii alikamatwa nyumbani kwake huko Homabay, Magharibi mwa Kenya na kusafirishwa hadi jijini Nairobi ambapo alifariki baada ya kukamatwa na Polisi, katika hali ya kutatanisha.
Awali Polisi walisema Ojwang, 31, alikamatwa kwa madai ya kumkashifu Eliud Lagat, Naibu Mkuu wa polisi nchini humo mtandaoni, na kwamba alifariki kwa kujiua "baada ya kujibamiza kichwa kwenye ukuta wa mahabusu".
Hatahivyo akiwa mbele ya kikao cha baraza la Seneti kuhusu mauaji ya Ojwang, Inspekta Mkuu wa Polisi nchini humo, Douglas Kanja ameomba radhi mbele ya Bunge la Seneti kwa niaba ya polisi ya taifa kwa kutoa taarifa isiyo sahihi kuhusu uchunguzi wa mauaji ya mwanablogu huyo.
Majeraha yake, ikiwa ni pamoja na jeraha la kichwa, shingo na sehemu zingine za mwili, yalionesha kuwa alishambuliwa na sio kujiua, kulingana na timu ya wataalamu illiyochunguza maiti yake.
Kifo cha Ojwang, kimezua shutuma nyingi kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu na kusababisha maandamano nje ya chumba cha kuhifadhia maiti juma lililopita ambapo mwili wake ulifanyiwa uchunguzi.
Uchunguzi wa kifo

Chanzo cha picha, EPA-EFE/Shutterstock
Inspekta mkuu wa polisi Kanja alipofika mbele ya Bunge la Seneti Jumatano wiki iliyopita aliwaambia Maseneta kwamba uchunguzi ulianza wakati machapisho ya mtandaoni yalipodai Naibu Imspekta mkuu wa polisi Lagat alihusika katika ufisadi ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
"Chapisho hilo lilidai kuwa alihusika katika ufisadi ndani ya NPS. Hasa, habari iliyochapishwa ilidai kuwa Lagat amewaweka kimkakati maafisa wake wa kuaminiwa kusimamia dawati la vitabu vya mamlaka ya upelelezi ya (DCI) na mabadiliko ya polisi wa usalama barabarani ili kudhibiti njia zote mbili za mapato na ujasusi," Kanja alisema.
Hapo jana Naibu Inspekta Jenerali (DIG), Huduma ya Polisi ya Kenya alijiondoa kupisha uchunguzi unaoendelea kwa sababu ya kifo cha Albert Ojwang.
Katika taarifa iliyotolewa Juni 16, 2025, Lagat alisema amechukua hatua hiyo kwa nia njema kutokana na jukumu na wajibu alionao kwenye nafasi yake.
Lagat aliongeza kuwa majukumu yake yatatekelezwa na naibu wake hadi uchunguzi utakapokamilika.
Pia "natoa rambirambi zangu kwa familia ya Bwana Albert Ojwang kwa kumpoteza mpendwa wao," taarifa hiyo ilisema.
Lagat aliahidi kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi.
Kifo cha Albert Ojwang, kimesababisha hasira miongoni mwa umma huku maafisa kadhaa waliokuwa kazini wakati huo wakikamatwa.
Shinikizo kutoka kwa makundi ya kutetea haki

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la kutetea haki haki za binadamu limewasilisha ombi mahakamani likitaka kuanzisha kesi ya binafsi dhidi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Kipkoech Lagat kuhusu kifo cha Ojwang.
Kulingana na ombi hilo, mazingira yanayozunguka kifo cha mwanablogu huyo - kinachodaiwa kuwa baada ya kukamatwa, kushikiliwa na kuteswa haitakuwa sawa kushughulikiwa tu kupitia taratibu za ndani za kinidhamu.
Walalamikaji hao Julius Ogogoh, Khalef Khalef, Francis Auma, na Peter Agor wanahoji kuwa mamlaka za uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka zimeshindwa kuchukua hatua ifaayo katika suala hilo.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja alipofika mbele ya Bunge la Seneti la Kenya alisema Naibu wake Eliud Kipkoech Lagat ndiye mlalamikaji aliyehusika na kukamatwa kwa Ojwang', kwani alidai kuwa marehemu alikuwa ametoa matamshi ya kashfa dhidi yake kwenye jukwaa lake la X.
Lagat yuko mashakani wakati uchunguzi wa kina kuhusu kesi hiyo ukianzishwa, huku wanaharakati wa haki za kiraia na Wakenya wakitaka ajiuzulu kwa madai kwamba alihusika na kifo cha Ojwang.














