Albert Ojwang: Mkuu wa polisi Kenya aomba radhi kwa madai ya udanganyifu kuwa mwanablogi alijiua

Inspekta Mkuu wa polisi (IG) nchini Kenya Douglas Kanja ameomba radhi kwa kutoa ripoti isiyo sahihi kuhusu uchunguzi wa mauaji ya mwanablogi mwenye ushawishi Albert Ojwang.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya mubashara kwa leo, tukutane tena hapo kesho.

  2. Albert Ojwang: Rais wa Kenya asema mwanablogu alikufa 'mikononi mwa polisi'

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais William Ruto amewataka Wakenya kuwa na Subira wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu kifo cha Albert Ojwang

    Rais wa Kenya William Ruto alisema Jumatano kuwa kifo cha mwanablogu aliyekuwa kizuizini kilitokea "mikononi mwa polisi", na kuwaomba Wakenya wawe na subira wakati uchunguzi ukiendelea.

    Kifo cha Albert Ojwang kimekuwa tukio la hivi punde zaidi kuchunguzwa na idara za usalama za Kenya baada ya miaka mingi ya mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu ambao Ruto ambapo amekuwa akiahidi kukomesha vitendo hivyo mara kwa mara licha ya hasira ya umma inayoongezeka.

    Awali Polisi walisema Ojwang, 31, alikamatwa magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa kwa madai ya kumkashifu naibu mkuu wa polisi nchini humo mtandaoni, na alifariki "baada ya kugonga kichwa chake kwenye ukuta wa mahabusu".

    Hatahivyo akiwa mbele ya kikao cha baraza la Seneti kuhusu mauaji ya Ojwang, Inspekta Mkuu wa Polisi nchini humo Douglas Kanja ameomba radhi mbele ya bunge la Seneti kwa niaba ya polisi ya taifa kwa kutoa ripoti isiyo sahihi kuhusu uchunguzi wa mauaji ya mwanablogi mwenye ushawishi Albert Ojwang.

    Majeraha yake, ikiwa ni pamoja na jeraha la kichwa, shingo na uharibifu wa mwili, yalionesha kuwa shambulio lilikuwa sababu ya kifo chake, kulingana na Mchunguzi maiti wa serikali ,Bernard Midia, ambaye alikuwa sehemu ya timu iliyofanya uchunguzi wa maiti.

    Kifo cha Ojwang, ambaye aliandika kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii, kimezua shutuma nyingi kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu na kusababisha maandamano nje ya chumba cha kuhifadhia maiti ambapo mwili wake ulifanyiwa uchunguzi katika mji mkuu Nairobi.

    Maelezo zaidi:

  3. Albert Ojwang: Mkuu wa polisi Kenya aomba radhi kwa madai ya udanganyifu kuwa mwanablogi alijiua

    g

    Chanzo cha picha, National police/Kenya

    Maelezo ya picha, Inspekta Mkuu wa polisi (IG) nchini Kenya Douglas Kanja

    Inspekta Mkuu wa polisi (IG) nchini Kenya Douglas Kanja ameomba radhi kwa kutoa ripoti isiyo sahihi kuhusu uchunguzi wa mauaji ya mwanablogi mwenye ushawishi Albert Ojwang.

    Mapema wiki hii, IG Kanja alidai kuwa Ojwang alifariki kwa kujitoa uhai baada ya kujigonga kichwa kwenye kuta za mahabusu za polisi, madai ambayo yalizua taharuki kutoka kwa umma, ambao uliishutumu polisi kwa kujaribu kuficha kifo cha mshawishi huyo.

    Katika kikao cha baraza la Seneti Jumatano, IG Kanja alisisitiza kwamba hangeweza kutoa tamko lolote hadi Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) ikamilishe uchunguzi huo.

    Pia aliapa kuwachukulia hatua maafisa waliompatia ripoti hiyo akisema taratibu za kinidhamu zitaambatana na Taratibu za Kawaida za Uendeshaji.

    "Ikiwa katika uchunguzi unaoendelea na IPOA, tutajua ukweli. Maafisa waliotoa ripoti ya awali watalazimika kukabiliwa na taratibu za kinidhamu," Kanja alisema.

    "Kutokana na kile tulichosikia hapa, tutaendelea na kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya afisa aliyetupa taarifa siku hiyo."

    Hata hivyo maseneta hao walipinga matamshi ya Kanja na kudokeza kuwa IPOA imefutilia mbali kujiua kufuatia kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi wa maiti.

    Akikabiliwa na maswali makali , IG Kanja aliomba msamaha kwa huzuni kwa ripoti ya awali.

    "Ninaomba msamaha kwa niaba ya [Huduma ya polisi ya kitaifa] NPS kwa sababu ya habari hiyo," Kanja alisema huku akishangiliwa na maseneta.

    Maelezo zaidi:

  4. Albert Ojwang: Wanaharakati waomba mkuu wa polisi ashtakiwe kuhusiana na kifo cha mwanablogi

    g

    Chanzo cha picha, National police/ Kenya

    Maelezo ya picha, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Kipkoech Lagat analaumiwa kuhusu kifo cha mwanablogu Albert Ojwang.

    Kundi la haki za binadamu limewasilisha ombi mahakamani likitaka kuanzisha kesi ya kibinafsi dhidi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Kipkoech Lagat kuhusu kifo cha mwanablogu Albert Ojwang.

    Kulingana na ombi hilo, mazingira yanayozunguka kifo cha mwanablogu huyo - kinachodaiwa kuwa baada ya kukamatwa, kuzuiliwa na kuteswa - ni mbaya sana kuweza kushughulikiwa tu kupitia taratibu za ndani za kinidhamu.

    Walalamishi hao Julius Ogogoh, Khalef Khalef, Francis Auma, na Peter Agor wanahoji kuwa mamlaka za uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka zimeshindwa kuchukua hatua ifaayo katika suala hilo.

    Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja amekuwa katika bunge la seneti la Kenya Douglas Kanja amesema DIG Lagat ndiye mlalamishi aliyehusika na kukamatwa kwa Ojwang', kwani alidai kuwa marehemu alikuwa ametoa matamshi ya kashfa dhidi yake kwenye jukwaa lake la X.

    h

    Chanzo cha picha, Mitandao ya kijamii

    Maelezo ya picha, Albert Ojwang'. aliuliwa katika erumande ya polisi

    Naibu Inspekta Jenerali (DIG), Huduma ya Polisi ya Kenya Eliud Kipkoech Lagat amekuwa mkuu wa polisi katika mazungumzo kuhusu kifo kisichojulikana cha Albert Ojwang'.

    Inspekta mkuu wa polisi Kanja amewaambia Maseneta Jumatano kwamba uchunguzi ulianza wakati machapisho ya mtandaoni yalipodai Naibu Imspekta mkuu wa polisi Lagat alihusika katika ufisadi ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

    "Chapisho hilo lilidai kuwa alihusika katika ufisadi ndani ya NPS. Hasa, habari iliyochapishwa ilidai kuwa Lagat amewaweka kimkakati maafisa wake wa kuaminiwa kusimamia dawati la vitabu vya mamlaka ya upelelezi ya (DCI)na mabadiliko ya trafiki ili kudhibiti njia zote mbili za mapato na ujasusi," Kanja alisema.

    Lagat yuko mashakani huku uchunguzi wa kina kuhusu kesi hiyo ukianzishwa, huku wanaharakati wa haki za kiraia na Wakenya wakitaka ajiuzulu kwa madai kwamba alihusika na kifo cha Ojwang.

    Soma pia:

  5. Sabuni zilizotengenezwa kutokana na maji ya kuoga ya muigizaji yauzwa kwa $2,000

    g

    Chanzo cha picha, BBC/Getty Images

    Sabuni iliyotengenezwa kutokana na maji ya kuoga ya muigizaji wa Hollywood Sidney Sweeney, ambayo ililianza kuuzwa Ijumaa, Juni 6, na kuuzwa sekunde moja baada ya kutangazwa, Sasa zinauzwa kwenye $2,000, vyombo vya habari vya Magharibi vinaripoti.

    Muigizaji huyo wa filamu ya Euphoria ni mmoja wa nyota wa filamu wanaokabiliwa na udhalilishaji wa kingono zaidi wa Hollywood na mara nyingi hukabiliwa na maoni yasiyotakikana kuhusu mwili wake kutoka kwa mashabiki - ambao baadhi yao hata wameonyesha hamu ya kunywa maji yake ya kuoga.

    "Mashabiki wako wanapoanza kuomba maji yako ya kuoga, unayapuuza au kuyageuza kuwa sabuni ya Dk. Squatch," Sweeney alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari akitangaza sabuni yake mpya, inayojulikana kama "Bathwater Bliss."

    Katika mauzo yasiyo ya kawaida sabuni ya Sweeney na Dk Squatch ambayo ina la gome la msonobari, na matone ya maji kutoka bafu la muigizaji, iliuzwa moja kwa moja na mashabiki, ikiuzwa kwa $8, kwa kila sabuni linaandika gazeti la Independent.

    Kulingana na NBC New York, wanunuzi wengine watarajiwa waliambiwa watalazimika kusubiri dakika 250 kufanya ununuzi, wakati wengine walidai tovuti ya mauzo ilikuwa imekwama kabisa.

    Sabuni sasa inaorodheshwa kwenye mtandao wa eBay kwa bei kuanzia $100 hadi $2,000.

    Katika mahojiano na GQ, Sweeney alizungumza juu ya mchakato wa kuunda bidhaa hii.

    "Tulipokuwa tukirekodi [Dr. Squatch], kulikuwa na beseni langu la kuogea. Na kwa kweli niliingia mle ndani, nikachukua sabuni, tukaoga kidogo vizuri, na wakachukua maji hayo. Kwa hiyo haya ni maji halisi kutoka kwenye beseni langu," alithibitisha.

    Licha ya ujanja wa ucheshi wa uuzaji, hadithi iligusa mada za kina.

    "Nilitaka sabuni ifanane na nyumba yangu, kwa hiyo ina harufu ya asili sana - kitu kama msonobari . Na harufu ya kiume. Lakini pia waliongeza maji kidogo ya kuoga, "mwigizaji alisema.

  6. Miili ya wanajeshi 1,212 waliokufa yarudishwa Ukraine - Ukraine yathibitisha

    g

    Miili ya wanajeshi 1,212 waliokufa imerejeshwa nchini Ukraine, Makao Makuu ya ya taasisi ya matibabu ya wafungwa wa vita yaliripoti katika mtandao wa telegram.

    Miongoni mwao ni wale waliouawa katika eneo la Kursk, na pia katika mikoa ya Kharkiv, Luhansk, Donetsk, Zaporizhia na Kherson.

    "Wachunguzi kutoka vyombo vya kutekeleza sheria, pamoja na taasisi za kitaalam za Wizara ya Mambo ya Ndani, watabaini utambulisho wa marehemu haraka iwezekanavyo," taasisi hiyo imesema katika taarifa yake.

    Jeshi la Urusi liliitaka Ukraine kuchukua kundi la kwanza la miili mwishoni mwa juma la tarehe 7-8, Juni na kudai kwamba Kyiv inadaiwa kukataa kuwapokea wanajeshi waliokufa wa Ukraine.

    Urusi na Ukraine zilikubaliana kuhusu kubadilishana miili ya wafu, na pia kubadilishana wafungwa wa vita (wenye umri hadi wa miaka 25, waliojeruhiwa na waliojeruhiwa vibaya), katika duru ya pili ya mazungumzo ya moja kwa moja huko Istanbul mnamo Juni 2.

    Unaweza pia kusoma:

  7. Marekani yaitaka Rwanda kuondoa majeshi yake Congo kabla ya makubaliano

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani inataka makubaliano kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kujumuisha Rwanda kuyaondoa majeshi yake kutoka Mashariki mwa Congo kabla pande hizo mbili kutia saini makubaliano ya amani.

    Duru zinaarifu kuwa rasimu ya makubaliano ya amani inaanisha kuwa sharti Rwanda iyaondoe majeshi yake,silaha na vifaa vyake mashariki mwa Congo ndipo makubaliano hayo yatiwe saini.

    Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umekuwa ukisimamia mazungumzo ya kuvimaliza vita vya Congo na kuhakikisha uwekezaji hasa katika sekta ya madini

    Mshauri mkuu wa Trump kuhusu Afrika Massad Boulos mnamo mwezi uliopita,alisema anataka makubaliano ya amani kuafikiwa katika kipindi cha miezi miwili,muda ambao wachambuzi wanautilia mashaka ikizingatiwa matatizo yaliyokita mizizi yanayochochea uhasama kati ya DRC na Rwanda.

    Serikali ya Rais Felix Tshisekedi imekuwa ikiishutumu vikali Rwanda kuunga mkono kundi la waasi la M23,madai ambayo Rwanda mara kwa mara imekuwa ikiyakanusha. Rwanda imekuwa ikisema kuwa inalinda mipaka yake na Congo kutokana yapo Congo na tisho dhidi ya waasi wa Kihutu (FDLR)wanaoutuhimiwa katika mauaji ya halaiki ya mwaka 19994 yaliyowaua karibu watu milioni moja, wanaohatarisha usalama wake. Imeilaumu pia serikali ya Kinshasa kwa kuwaingiza wanamgambo hao katika jeshi lake.

    Duru zinasema Rwanda bado haijatoa msimamo wake kuhusu rasimu hiyo ya makubaliano. Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe ameliambia shirika la Reuters kuwa wataalamu kutoka Congo na nchi yake watakutana wiki hii mjini Washington kujadili zaidi makubaliano hayo.

    Hata hivyo Congo inahisi Rwanda inajikokota katika kufikia makubaliano ya amani ikisisitiza kuwa ili mchakato huo wa amani ufanikiwe,Rwanda lazima iondoe majeshi yake na ikome kuwaunga mkono waasi wa M23.

    Serikali ya Congo pia inafanya mazungumzo mengine na waasi hao yakisimamiwa na Qatar lakini walio na ufahamu na yanayojiri katika mazungumzo hayo ya Doha wanasema hakuna juhudi kubwa zilizopigwa na pande zote mbili.

    Soma zaidi:

  8. Elon Musk asema 'anajutia' baadhi ya ujumbe aliyochapisha kuhusu Donald Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Elon Musk ameomba radhi katika mtandao wa X akielezea masikitiko yake juu ya vita vyake vya maneno na Rais Donald Trump wiki iliyopita, na kukiri kwamba "baadhi" ya ujumbe wake wa kumshambulia kiongozi huyo wa taifa "ulivuka mpaka."

    "Najutia baadhi ya ujumbe wangu kuhusu Rais Donald Trump wiki iliyopita. Ulivuka mpaka," tajiri huyo aliandika kwenye mtandao wa kijamii anaoumiliki mapema Jumatano asubuhi.

    Wawili hao walijikuta katika mzozo hadharani, baada ya mmiliki wa Tesla kupinga mswada wa ushuru wa Trump.

    Ujumbe wake unawadia baada ya Trump kutangaza kuwa uhusiano wao umefikia kikomo na kwamba hana nia ya kuurekebisha.

    Bajeti hiyo, ambayo inajumuisha punguzo kubwa la ushuru na matumizi zaidi ya ulinzi, ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita na sasa ipo katika Bunge la Seneti.

    Musk aliwataka Wamarekani kutoa wito kwa wawakilishi wao "kutoupitisha muswada huo" kwa sababu anaamini "utasababisha mdororo wa uchumi katika nusu ya pili ya mwaka".

    Soma zaidi:

  9. Idadi ya walioachwa bila ya makazi Haiti yavunja rekodi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinasema idadi ya watu walioachwa bila ya makazi Haiti imevunja rekodi.

    Tangu mwezi Desemba idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 24 ikifikisha idadi jumla ya walioachwa bila ya makazi Haiti kupindukia milioni 1.3.

    Mji mkuu wa Port-au-Prince ndiyo ulioathirika zaidi lakini pia ghasia zimezagaa hadi kwa miji mingine ya nchi hiyo.

    Magenge ya wahalifu yanadhibiti maeneo mengi ya mji huo ikiripoti kuwa magenge hayo yameungana na sasa yanadhibiti asilimia 85 ya mji mkuu.

    Umoja wa Mataifa unasema watu hao milioni moja nukta tatu walioachwa bila ya makazi ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa Haiti, taifa linalokumbwa na ghasia kali kwa miaka mingi.

    Mauaji, ubakaji, utekaji nyara na uporaji vimechangia pakubwa katika kulitumbukiza taifa hilo katika msukosuko wa kisiasa.

    Mkurugenzi mkuu wa shirika la uhamiaji la IOM Amy Pope ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kudhibiti hali akisema watu wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa na mzozo huo haupaswi kuchukuliwa kuwa hali ya kawaida.

    Pope ameongeza kuwa waathiriwa wanapitia dhiki na mateso yasiolezeka na wengi wao hawana chochote na wanaishi katika mazingira yasiyo salama na kwenye mahema bila ya mahitaji muhimu kama huduma za afya, maji safi ya kunywa, chakula cha kutosha na elimu kwa watoto wao.

    Robo ya walioachwa bila ya makazi wanaishi mjini Port au Prince lakini idadi ya wanaokimbilia katika maeneo mengi ya nchi inazidi kuongezeka.

    IOM inasema idadi ya walioachwa bila ya makazi kaskazini mwa Haiti imeongezeka kwa asilimia themanini.

    Mnamo mwezi Februari, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, liliripoti ongezeko la visa vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

    Umasikini mkubwa pia umewafanya watoto wengi kujiunga na magenge ya wahalifu.

    UNICEF inasema nusu ya idadi ya wapiganaji wa magenge hayo ni watoto.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Kevin De Bruyne akubali mkataba wa miaka miwili kujiunga na Napoli

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Gwiji wa Manchester City, Kevin De Bruyne, anajiandaa kuuungana na kiungo wa zamani wa Manchester united, Scott McTominay katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kukubali mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa ligi hiyo, Napoli.

    Mchezaji huyu wa kimataifa wa Ubelgiji sasa amekubali rasmi kujiunga na klabu hiyo ya Italia na anatarajiwa kusafiri kwa ajili ya vipimo vya afya na Napoli. De Bruyne atasaini mkataba wa miaka miwili, wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, kufuatia kuondoka kwake Manchester City.

    De Bruyne alikuwa akivutiwa na timu kutoka Ligi Kuu ya Marekani (MLS) lakini ameamua kuendeleza maisha yake ya soka barani Ulaya na Napoli.

    Kuwasili kwake kutakuwa jambo kubwa kwa klabu hiyo kufuatia ushindi wao mzuri wa taji la Serie A msimu uliopita. Ataungana na aliyekuwa kiungo wa Manchester United, Scott McTominay, katika klabu hiyo ya Italia.

    McTominay alifurahia msimu mzuri wa 2024-25 na alichangia pakubwa katika mafanikio ya taji hilo la Napoli, akifunga mabao 12 ya ligi.

    Katika kipindi chake akiwa Manchester City, De Bruyne ametoa pasi nyingi zaidi za mabao akiongoza ligi zote tano bora za Ulaya katika mashindano yote: pasi 170 katika mechi 422.

  11. Mzozo wa mazishi ya aliyekuwa rais wa Zambia wachanganya waombolezaji

    .

    Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

    Kupanga mazishi kunaweza kuwa majaribio makubwa hali ikiwa sio tofauti hata kwa rais wa zamani nchini Zambia.

    Watu wakiwa katika hali ya huzuni, wapendwa lazima wafikirie kuhusu gharama, matakwa ya mwendazake na mambo mengine mengi ili kumuaga mpendwa wenu kwa njia ambayo mungependa.

    Kwa kiongozi huyu wa zamani, jumuisha matakwa ya serikali, wapinzani wa kisiasa na familia hali inaweza kuwa ngumu mara mbili.

    Edgar Lungu, ambaye aliongoza Zambia kutoka mwaka 2015 hadi 2021, alifariki Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 68.

    Kifo chake kimewashtua Wazambia - na kuna hali ya huzuni ya kweli huku vituo vyote vya redio vikipiga muziki wa injili kwa kiongozi huyo ambaye alikuwa amebakia kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Zambia licha ya kuzuiwa kugombea uchaguzi wa mwaka jana.

    Zambia ni rasmi nchi ya Kikristo - na watu wengi huchukulia dini na vipindi vyao vya maombolezo kwa umuhimu mkubwa.

    Lakini mvutano kati ya familia yake, serikali na chama cha siasa cha Lungu, Patriotic Front (PF), umewaacha waombolezaji wakiwa wamechanganyikiwa kuhusu jinsi gani hasa rais huyo wa zamani anapaswa kupewa heshima yake ya mwisho.

    Serikali ilitangaza kutakuwa na mazishi ya kitaifa na kutangaza kwamba mahali rasmi pa maombolezo itakuwa sehemu ya kulala wageni inayomiliki katika mji mkuu, Lusaka, lakini chama cha PF kilitupilia mbali mpango huu, na badala yake, kikaelekeza waombolezaji kwenye makao yake makuu.

    Kuhusu familia ya Lungu, wamesema hawapingi mazishi ya serikali, lakini wamesisitiza kuchagua ni nani atakayesimamia mazishi hayo, wakili wa familia Makebi Zulu ameambia BBC.

    Kisha kuna kitabu rasmi cha maombolezo, ambacho waombolezaji wanaweza kumuenzi Lungu. Serikali imetenga kitabu rasmi – katika eneo walilolitenga - lakini PF imewataka watu kusaini kitabu chao - katika makao yao makuu.

    Serikali ilitaka kurudisha mwili wake kutoka Afrika Kusini wiki iliyopita - Lungu alifia huko baada ya kupata matibabu ya ugonjwa ambao haukujulikana.

    Hata hivyo, PF na familia ya Lungu waliingilia kati, wakitaka kupewe fursa ya kufanya maandalizi wanayotaka kwa kiongozi huyo wa zamani.

    "Serikali ilikuwa ikisema, 'Tunampa heshima kamili ya kijeshi, kwa hivyo tutachukua mwili kuanzia hapa' - kana kwamba wanasema 'hamna uamuzi juu ya kile kinachotokea,'" Bw Zulu alisema.

    Mipango ya kurejesha mwili wa Lungu bado haijulikani, ingawa familia sasa inashirikiana na serikali kuhusu suala hili.

    Pia kumekuwa na mkanganyiko juu ya kipindi "rasmi" cha maombolezo wakati aina zote za burudani kama vile mechi kubwa za kandanda na matamasha zimesimamishwa.

    Serikali ilitangaza kipindi cha siku saba cha maombolezo ya kitaifa kuanzia Jumamosi iliyopita, ingawa PF ilitangaza siku moja kabla.

    Mkanganyiko huu, unaonekana kuwa mwendelezo wa uhusiano wa misukosuko kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema.

    Wawili hao ni wapinzani wa muda mrefu - mnamo 2017, Lungu alipokuwa rais, Hichilema aliwekwa kizuizini kwa zaidi ya siku 100 kwa tuhuma za uhaini baada ya msafara wa Hichilema kudaiwa kukataa kumpisha njia.

    Ilibidi Jumuiya ya Madola kuingilia kati kwa Hichilema kuachiliwa. Miaka minne baadaye, na baada ya majaribio matano ya urais, Hichilema alimshinda Lungu.

    Sasa, chama cha PF na wakili wa familia ya Lungu wanaishutumu serikali ya Hichilema kwa kuhusika kwa kiasi fulani na kifo cha rais huyo wa zamani.

    Soma zaidi:

  12. Raia wa Austria waomboleza waathiriwa wa shambulio la ufyatuaji risasi shuleni

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelfu ya watu nchini Austria wamefanya mkesha wa kuwasha mishumaa kwa waathiriwa wa shambulio la ufyatuaji wa risasi shuleni ambapo watu 10 waliuawa.

    Polisi walisema mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye ni mwanafunzi wa zamani, alijitoa uhai katika bafu la shule muda mfupi baada ya kutekeleza shambulizi hilo huko Graz siku ya Jumanne – likiwa ni baya zaidi katika historia ya hivi majuzi ya nchi.

    Kisa hicho kilitokea katika shule ya upili ya Dreierschützengasse kaskazini magharibi mwa jiji.

    Watu wengine 12 walijeruhiwa, wengine vibaya, na nia ya mshambuliaji huyo bado inachunguzwa, maafisa walisema.

    Wanawake sita na wanaume watatu waliuawa katika shambulio hilo, na mwanamke wa nne alifariki baadaye hospitalini.

    Shirika la habari la APA la Austria limeripoti kuwa saba kati ya waliouawa walikuwa wanafunzi.

    Astrid, mwanamke anayeishi na mumewe Franz katika orofa ya chini ya jengo la makazi karibu na shule hiyo, aliambia BBC kwamba alikuwa amemaliza tu kufua aliposikia milio ya risasi.

    Alisema: "Nilisikia milio ya risasi. Nyingi, moja baada ya nyingine. 'Poof... poof... poof…. poof…' tena na tena. Niliingia aliko mume wangu na nikamwambia: 'Kuna mtu anapiga risasi!'

    Kufikia Jumanne alasiri, foleni ndefu zilikuwa zinashuhudiwa nje ya kituo cha uchangiaji damu huko Graz.

    "Leo ni siku ngumu kwetu sote Graz. Niko hapa [kuchangia] damu yangu kusaidia watu wengine wanaohitaji," Stephanie Koenig mwenye umri wa miaka 25 aliambia shirika la habari la Reuters.

    Soma zaidi:

  13. Marekani yashutumu hatua ya kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Israel

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amelaani hatua ya Uingereza, Norway, Australia, Canada na New Zealand kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Israel wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali kutokana na mzozo wa Gaza.

    Marco Rubio alilaani hatua hiyo, akiandika kwenye mtandao wa X: alisema "Vikwazo hivi haviendelezi juhudi zinazoongozwa na Marekani kufikia usitishaji vita, kuwarudisha mateka wote nyumbani, na kumaliza vita".

    Aliyataka mataifa kubatilisha vikwazo hivyo, akiongeza kuwa Marekani "imesimama bega kwa bega na Israel."

    Uingereza imewawekea vikwazo Waziri wa Fedha Smotrich na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Ben-Gvir kwa sababu ya "kuchochea ghasia za itikadi kali na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za Wapalestina".

    Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich wote watapigwa marufuku kuingia Uingereza na mali yoyote nchini Uingereza itazuiwa kama sehemu ya hatua zilizotangazwa na waziri wa mambo ya nje.

    Ni sehemu ya hatua ya pamoja na Australia, Norway, Canada na New Zealand iliyotangazwa Jumanne.

    Ikijibu, Israel ilisema: "Inasikitisha kwamba wawakilishi waliochaguliwa na wanachama wa serikali wanachukuliwa hatua za aina hii."

    Soma zaidi:

  14. India: Bibi harusi akamatwa kwa madai ya kumuua mumewe kwenye fungate

    .

    Chanzo cha picha, Familia ya Raghuvanshi

    Maelezo ya picha, Sonam na Raja Raghuvanshi walifunga ndoa mnamo Mei 11.

    Mwanamke aliyetoweka baada ya mumewe kuuawa kikatili walipokuwa kwenye fungate yao amekamatwa baada ya kujisalimisha, polisi wa India wamesema.

    Familia za wanandoa hao zilidai kuwa bibi harusi pia alikuwa ameuawa au kutekwa nyara, na wakaanzisha msako mkubwa kumtafuta.

    Miongoni mwa waliokamatwa ni mkewe bwana harusi Sonam Raghuvanshi mwenye umri wa miaka 25, kuhusiana na mauaji ya Raja mwenye umri wa miaka 30.

    Babake Sonam, Devi Singh, alimtetea binti yake, akisema, "Yeye hana hatia, hawezi kufanya hivi."

    Wapenzi hao wapya, wanaoishi Indore, Madhya Pradesh, walichagua Meghalaya kwa fungate yao kwa sababu walisikia kuwa ina "mabonde mazuri sana", kakake Raja, Sachin Raghuvanshi aliambia BBC kabla ya Sonam kukamatwa.

    Wenzi hao walifunga ndoa mnamo Mei 11 huko Indore katika sherehe ya harusi yenye baraka za familia zao zote mbili.

    "Ndoa yao ilipangwa miezi minne kabla ya siku yenyewe. Wote wawili walikuwa na furaha sana, hakukuwa na mzozo wowote kati ya wawili hao kabla au baada ya ndoa," alisema kaka mwingine wa Raja, Vipin Raghuvanshi.

    Wenzi hao waliondoka kwenda Meghalaya mnamo Mei 20. Lakini walipotea siku nne katika safari yao.

    Wiki moja baadaye, mwili wa Raja uliokuwa umeoza ulipatikana kwenye korongo la milimani, koo lake likiwa limekatwa, na pochi yake, pete ya dhahabu na mkufu haukuwepo. Hakukuwa na dalili yoyote ya Sonam, ambaye alikuwa bado hayupo.

    Lakini Jumatatu asubuhi, Mkurugenzi Mkuu wa Polisi wa Meghalaya Idashisha Nongrang alisema kwamba Sonam alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Ghazipur wilaya ya Uttar Prades.

  15. Amri ya kutotoka nje yaanza kutekelezwa katika jiji la Los Angeles

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meya wa Los Angeles Karen Bass ametangaza amri ya kutotoka nje katika jiji Los Angeles kukomesha uharibifu.

    Bass amesema amri ya kutotoka nje itatekelezwa kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi.

    Akielezea hitaji la amri ya kutotoka nje, na kuongeza kwamba kumekuwa na "uharibifu mkubwa" katika jiji lote.

    "Nitashauriana na viongozi waliochaguliwa na maafisa wa kutekeleza sheria kesho ... tunatarajia idumu kwa siku kadhaa."

    Mkuu wa polisi wa LA Jim McDonnell, alisema amri ya kutotoka nje ni hatua muhimu ili kuokoa maisha na kulinda mali baada ya mfululizo wa machafuko yanayoongezeka katika jiji hilo.

    Alisisitiza kuwa watu watakaovunja amri ya kutotoka nje bila upendeleo watakamatwa.

    Bass alisisitiza maneno yake ya awali - kwamba anataka Trump asitishe hatua ya kutumiwa kwa wanajeshi katika jiji hilo.

    "Nafkiria juu ya familia ambazo zinaogopa kwenda kazini na kwenda shule," alisema.

    Wakati huo huo, Jaji wa Marekani alizuia ombi la dharura kutoka kwa Gavana wa California la kutaka kuzuia kutumiwa kwa wanajeshi kwenye vurugu zilizoshuhudiwa katika mji wa Los Angeles.

    Gavana Gavin Newsom ameitaja hatua hiyo kuwa kinyume na sheria.

    Rais Donald Trump ametetea uamuzi wake wa kutuma majeshi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga sera kali dhidi ya wahamiaji na kuapa kuwa kamwe hataruhusu mji wowote wa Marekani kuvamiwa na kutawaliwa na wageni.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 11/06/2025