Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Israel na Iran; Operesheni ya Israel inaelekea wapi?
- Author, Lyse Doucet
- Nafasi, Chief international correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Siku ya Ijumaa, baada ya Israeli kuanzisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Iran, Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu aliwahutubia Wairani moja kwa moja. Akizungumza kwa Kiingereza, aliwaambia kuwa wakati umefika wa wao kusimama dhidi ya "utawala mbaya na dhalimu".
Operesheni za kijeshi za Israeli zilikuwa ni "kukusafishia njia kufikia uhuru wako".
Sasa, wakati makabiliano ya kijeshi kati ya Iran na Israeli yanazidi kuongezeka, na kuongezeka kwa maeneo yanayolengwa , wengi wanauliza - ni nini mwisho halisi wa Israeli?
Je, ni kumalizika tu, kama Netanyahu pia alivyotangaza Ijumaa usiku wa kwanza wa shambulio, "tisho la serikali ya Kiislamu la nyuklia na makombora ya balistiki"?
Ilikuwa pia kumaliza mazungumzo yoyote zaidi kati ya Marekani na Iran, kufikia makubaliano mapya yaliyojadiliwa ili kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran badala ya kuondolewa kwa vikwazo vya kuumiza?
Au ujumbe huo kwa Wairani juu ya kusafisha njia ya kupata uhuru unaweza kufungua njia kwa lengo kubwa zaidi la kujaribu kukomesha utawala wa kidini wa Iran?
Kuanzia majenerali hadi Trump: Nani ana sikio lake?
Kazi ya kisiasa ya waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi wa Israeli imewekwa alama na dhamira yake ya kibinafsi ya kuuonya ulimwengu kuhusu hatari zinazoletwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran – kuanzia kwa bomu bandia ambalo amelionyesha katika Umoja wa Mataifa, hadi kujizuia kwake mara kwa mara wakati wa miezi 20 iliyopita ya vita vya kikanda vinavyowaka kwamba Iran ilikuwa tishio kubwa kuliko zote.
Marais wa Marekani na majenerali wa Netanyahu wenyewe wanajulikana kuwa walimzuia kwa zaidi ya mara moja kwa miaka mingi, kuamuru mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Rais wa Marekani Donald Trump anasema hakutoa hakumruhusu.
"Sasa yuko ndani, yuko ndani," ndivyo afisa mmoja wa magharibi alivyoelezea mchezo wa Netanyahu. Pia alisisitiza maoni kwamba lengo kuu la Israeli lilikuwa kudhoofisha mpango wa nyuklia wa Iran.
Uamuzi huo umelaaniwa sana na kanda zote katika eneo hilo, na vile vile Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambao Mkurugenzi wake Mkuu Rafael Grossi alisisitiza: "Nimesema mara kwa mara kwamba vifaa vya nyuklia havipaswi kushambuliwa kamwe, bila kujali muktadha au hali." Pia wamelaaniwa na wasomi wa sheria ambao wanasema kuwa shambulizi hilo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.
Lakini wengi sasa wanauliza ikiwa waziri mkuu wa Israeli anafuata malengo sawa na washauri wake wakuu na washirika.
"Wakati Netanyahu anataka mabadiliko ya serikali, taasisi ya kisiasa na kijeshi ya Israeli imejitolea kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran," anasema Dk Sanam Vakil, Mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya Chatham House.
"Mwisho unaweza kuwa mgumu lakini unaweza kufikiwa kwa kiasi fulani," anaongeza. "Inaonekana kuwa ngumu kuufanya uwe wa muda mfupi huku ukizidi kuongezeka."
Kuharibu mpango wa nyuklia wa Iran
Netanyahu aliitaja operesheni ya Israeli kama mashambulizi ya mapema ya kuharibu tisho lililopo. Alitangaza kuwa harakati za Iran, ni za "dakika ya 90" kuelekea utengenezaji wa bomu la nyuklia.
Washirika wa Magharibi wameunga mkono tamko lake kwamba Tehran haipaswi kuruhusiwa kuvuka mstari huu. Lakini saa ya Netanyahu pia imeibua hoja sana.
Iran imekanusha mara kwa mara kuwa imeamua kutengeneza bomu. Mnamo Machi, Tulsi Gabbard, Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani, alishuhudia kwamba jamii ya ujasusi ya Marekani "inaendelea kutathmini kuwa Iran haitengenezi silaha ya nyuklia".
IAEA ilisema katika ripoti yake ya hivi punde ya robo mwaka kwamba Iran imekusanya urani ya kutosha iliyorutubishwa hadi usafi wa 60% - hatua fupi, ya kiufundi mbali na daraja la silaha, au 90% - ili kutengeneza mabomu tisa ya nyuklia.
Katika siku hizi chache za kwanza, vituo vitatu muhimu katika mpango mkubwa wa Iran vimelengwa - Natanz, Isfahan, Fordow. IAEA imesema kuwa kiwanda cha majaribio cha kurutubisha mafuta, juu ya ardhi, huko Natanz kiliharibiwa.
IAEA pia iliripoti kuwa "majengo manne muhimu" yaliharibiwa huko Isfahan. Israeli inaelezea uharibifu wa miundombinu hiyo ya Iran kama "muhimu"; Iran inasema ni midogo.
Na Israeli pia inapiga "vyanzo vya maarifa" kwa kuua, hadi sasa, angalau wanasayansi tisa wa nyuklia na orodha inayoongezeka ya makamanda wakuu wa jeshi. Orodha yake ya malengo, ambayo ni pamoja na vituo vya kijeshi, vifyatuzi vya makombora na viwanda, sasa inapanuka hadi miundombinu ya kiuchumi na mafuta.
Iran pia inajibu kwa mapigo kwenye na orodha yake ya malengo inayopanuka huku majeruhi wa raia wakiongezeka katika nchi zote mbili.
Lakini ili kushughulikia pigo kubwa kwa mpango mkubwa wa nyuklia wa Iran, Israeli italazimika kufanya uharibifu mkubwa kwa Fordow, eneo lake la pili kwa ukubwa na linalolindwa sana. Jumba hilo, chini ya ardhi ndani ya mlima, ndipo wataalam wengine wanaamini Iran imehifadhi urani yake iliyo karibu na silaha.
Ripoti katika vyombo vya habari vya Israeli zinasema lengo la sasa ni kujaribu kukata ufikiaji wa kituo hicho.
Israeli haina mabomu ya kupasua milima ambayo ingehitaji kuvunja miamba mingi. Lakini Jeshi la Anga la MMarekani linayo. Yanajulikana kama MOP - 30,000lb Massive Ordnance Penetrator yanayoingia kwa usahihi. Lakini bado shambulizi lingine litahitajika, kwa siku nyingi, kuwezesha uharibifu mkubwa.
"Nadhani hali inayowezekana zaidi ni kwamba Netanyahu atampigia simu Trump na kusema 'Nimefanya kazi hii nyingine yote, nimehakikisha kuwa hakuna tisho kwa mashambulizi ya B-2 na kwa vikosi vya Marekani lakini siwezi kumaliza mpango wa silaha za nyuklia,'" Richard Nephew, afisa wa zamani wa Marekani na mtaalam wa Iran katika Kituo cha Chuo Kikuu cha Columbia cha Sera ya Nishati Ulimwenguni, alikiambia kipindi cha Newshour cha BBC.
Afisa wa Magharibi aliniambia, "Bado haijulikani ni njia gani Rais Trump ataichukua."
Imepangwa kuharibu mazungumzo ya amani?
Trump anaendelea kutoa kauli zinazokinzana. Mwanzoni mwa wiki iliyopita, aliitaka Israeli kuacha kuitishia Iran kijeshi kwasababu shambulio linaweza "kuipiga". Inapokuja katika suala la mazungumzo ya nyuklia na Iran aTrump amekuwa akisema anayapendelea zaidi.
Mara tu Israeli iliposhambulia, alisifu mashambulizi hayo kama "bora" na kuonya "kuna mengi yajayo, mengi zaidi". Lakini pia alifikiria kuwa yanaweza kusaidia kuisukuma Iran kufanya makubaliano.
Kisha katika chapisho siku ya Jumapili kwenye jukwaa lake la Truth Social, alitangaza "Tutakuwa na AMANI, hivi karibuni, kati ya Israeli na Iran! Simu na mikutano mingi sasa inafanyika."
Wapatanishi wa Iran sasa wanashuku kuwa mazungumzo hayo, ambayo yalipangwa kuanza tena katika mji mkuu wa Oman Muscat siku ya Jumapili, yote yalikuwa mbinu ya kuishawishi Tehran kuwa shambulio la Israeli halikuwa karibu, licha ya kuongezeka kwa mvutano. Mashambulizi ya Israeli Ijumaa asubuhi yalifanyika kwa kuishtukiza Iran.
Wengine pia wanaona wakati huo kuwa muhimu. "Mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya Israeli yalipangwa kuua nafasi za Rais Trump kufikia makubaliano ya kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran," anasema Ellie Geranmayeh, naibu mkuu wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni.
"Wakati baadhi ya maafisa wa Israeli wanasema kuwa mashambulizi haya yalilenga kuimarisha ushawishi wa Marekani katika njia ya kidiplomasia, ni wazi ilikusudiwa kuharibu kabisa mazungumzo."
Maafisa walio na ufahamu wa mazungumzo haya walikuwa wameniambia wiki iliyopita kwamba "makubaliano yalikuwa yanafikiwa". Lakini yote yalitegemea Marekani kuondoka kwenye mahitaji yake ya juu kwa Iran, kukomesha urutubishaji wote wa nyuklia, hata kutoka kwa asilimia ndogo zaidi ya tarakimu moja inayolingana na mpango wa kiraia. Tehran iliona hilo kama "mstari mwekundu".
Baada ya Rais Trump kujiondoa katika makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya 2015 katika muhula wake wa kwanza, kwa sehemu chini ya msukumo wa mara kwa mara kutoka kwa Netanyahu, Iran iliondoka kutoka kwa wajibu wake wa kuzuia urutubishaji hadi 3.67% - kiwango kinachotumiwa kuzalisha mafuta kwa mitambo ya nyuklia ya kibiashara - na kuanza kuhifadhi pia.
Katika jaribio hili la pili, kiongozi wa Marekani alikuwa ameipa Iran "siku 60" kufanya makubaliano - dirisha linalotazamwa na wapatanishi wenye uzoefu na ujuzi wa uwanja eneo hili kuwa dogo sana kwa suala gumu kama hilo.
Israeli ilishambulia siku ya 61.
"Kituo cha Oman kimekufa kwa sasa," anasema Dk Vakil. "Lakini juhudi za kikanda zinaendelea kupunguza na mkwamo."
'Hisia ya Churchilli' ya Netanyahu
Kwa mtizamo kutoka Tehran, ongezeko hili la mzozo sio tu kuhusu hifadhi, na makombora ya hali ya juu.
"Wanaona kama Israeli inataka, mara moja na kwa wote, kushusha uwezo wa Iran kama serikali, taasisi zake za kijeshi, na kubadilisha usawa wa nguvu kati ya Iran na Israeli kwa njia madhubuti, na labda kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu kwa ujumla, ikiwa inaweza," anasema Vali Nasr, Profesa wa masomo ya Mashariki ya Kati na Masuala ya Kimataifa katika Shule ya Johns Hopkins ya Mafunzo ya Juu ya Kimataifa na mwandishi wa kitabu cha 2025 Mkakati Mkuu wa Iran.
Haijulikani jinsi umma wa Irani unaweza kujibu.
Taifa la watu milioni 90 limeteseka, kwa miaka mingi, athari za vikwazo vya kimataifa na ufisadi wa kimfumo. Maandamano yamepamba moto, mwaka baada ya mwaka, juu ya maswala kuanzia mfumuko mkubwa wa bei hadi ajira ndogo, uhaba wa maji na umeme hadi bidii ya polisi wa maadili inayodhibiti maisha ya wanawake. Mnamo 2002, mawimbi ya maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa yalidai uhuru zaidi; walikutana na ukandamizaji mkali.
Bwana Nasr anatoa tathmini yake ya hali ya umma sasa. "Labda mwanzoni, wakati majenerali wanne au watano wasiopendwa sana waliuawa, wanaweza kuwa walihisi utulivu, lakini sasa majengo yao ya ghorofa yanapigwa, raia wameuawa, na miundombinu ya nishati na umeme ya nchi inashambuliwa," anasema.
"Sioni hali ambayo Wairani wengi wataunga mkono mchokozi dhidi ya nchi yao wakati inailipua mabomu, na kwa namna fulani wanaona hiyo kama ukombozi."
Lakini kauli za Netanyahu zinaendelea kudokeza ulengaji mpana.
Siku ya Jumamosi, alionya nchi yake itapiga "kila eneona kila shabaha ya utawala wa ayatollah".
Siku ya Jumapili, alipoulizwa na shirika la habari la Fox News ikiwa mabadiliko ya serikali ni sehemu ya juhudi za kijeshi za Israeli, Waziri Mkuu wa Israeli alijibu "inaweza kuwa matokeo kwasababu utawala wa Iran ni dhaifu sana".
"Wanataka kucheza kwa hofu ya serikali ya kupoteza udhibiti kama sehemu ya vita vyao vya kisaikolojia," anasema Anshel Pfeffer, Mwandishi wa Israeli katika The Economist na mwandishi wa wasifu wa Netanyahu.
"Makubaliano ndani ya ujasusi wa Israeli ni kwamba kutabiri au kuhandisi kuanguka kwa utawala wa Irani hakuna maana. Inaweza kutokea hivi karibuni, au katika miaka 20."
Lakini Bw Pfeffer anaamini mawazo ya waziri mkuu yanaweza kuwa tofauti. "Nadhani kuna nafasi nzuri kwamba Netanyahu, tofauti na wakuu wake wa kijasusi, anaamini katika ujumbe; yuko katika hisia ya Churchill."
Kufikia Jumapili jioni, ripoti zilianza kuonekana kwenye vyombo vya habari vya Marekani, kila moja ikinukuu vyanzo vyao, kwamba Rais Trump alikuwa amepinga kura ya turufu katika siku za hivi karibuni mpango wa Israeli wa kumuua kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei. Gumzo lilianza wakati Reuters ilipotangaza taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ikinukuu maafisa wawili wa Marekani ambao hawakujulikana.
Watu wa Israeli waliohojiwa juu ya malengo yao, kutoka kwa waziri wa mambo ya nje Gideon Sa'ar hadi Mkuu wa Baraza la Usalama la Kitaifa Tzachi Hanegbi, wamesisitiza lengo lao sio uongozi wa kisiasa wa Iran. Lakini Hanegbi aliongeza - "lakini dhana ya 'kwa sasa' ni halali kwa muda mfupi."
Mwishowe, mtari wa mchezo huu wa mwisho utaundwa na mwendo wa makabiliano hatari na yasiyotabirika, na Rais wa Marekani asiyetabirika.
"Mafanikio au kutofaulu kunafafanuliwa kwa kiasi kikubwa na iwapo Marekani inaweza kuvutwa," anatathmini Daniel Levy, Rais wa mradi wa Marekani wa Mashariki ya Kati na mshauri wa zamani wa serikali ya Israeli. "Ni Marekani pekee inayoweza kuleta hili kwa wakati unaofaa katika siku za usoni kwa kubainisha matokeo ya ukomo."
Picha za juu na : Anadolu kupitia Getty, ATEF SAFADI/EPA - EFE/REX/Shutterstock
BBC InDepth Ni wavuti na programu ya uchambuzi bora, na mitazamo mipya ambayo inapinga mawazo na kuripoti kwa kina juu ya maswala makubwa ya siku. Na tunaonyesha maudhui ya kuchochea fikira kutoka kote BBC Sounds na iPlayer pia.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi