Sudan: Kuna nini Wad Madani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Mohamed Osman na Amal Saeed
- Nafasi, BBC News Arabic
Asubuhi ya tarehe 15 Disemba, zaidi ya wanajeshi kumi na wawili waliokuwa kwenye magari ya kijeshi walishambulia Wad Madani, mji wa pili kwa watu wengi nchini Sudan baada ya mji mkuu, Khartoum.
Wanajeshi hao walikuwa wa Kikosi cha Kusaidia Wanajeshi (RSF), kikundi cha kijeshi ambacho tangu Aprili kimekuwa kikipigana na jeshi la Sudan.
Siku tatu baadaye, RSF ilitangaza kuwa wanaudhibiti mji wa Wad Madani.
Mapigano hayo yamewakosesha makazi zaidi ya watu 300,000, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IMO).
Wengi wao walikuwa wamekimbia kutokana na mapigano katika eneo la Khartoum miezi michache tu iliyopita.
Kwa nini Wad Madani ni muhimu sana kwa pande zinazopigana Sudan?
Mji wa kimkakati

Chanzo cha picha, Getty Images
Mji wa Wad Madani, mji mkuu wa mkoa wa jimbo la Al-Jazira, uko kilomita 175 kaskazini mashariki mwa Khartoum. Makazi ya watu 700,000, pia imekuwa ikipokea zaidi ya watu 86,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na RSF.
Jiji hilo ni nyumbani kwa kitengo cha kwanza cha wanajeshi wa jeshi la Sudan, ambacho kilifanya kitendo cha kuuchukua mji wa Wad Madani kuwa ushindi mkubwa kwa RSF.
Al-Jazira inapakana na majimbo matatu makuu yanayodhibitiwa na jeshi, White Nile, Senar, na Gadaref.
"Hatua hii inatoa fursa kwa RSF kuchukua majimbo hayo pia," anasema Abdullah Mohamed Ahmed, jenerali mstaafu wa Sudan na mtaalam wa kijeshi.
"Maeneo ya kijeshi na silaha ambazo RSF wamezikamata Wad Madani zitatumika kama maeneo mapya ya kuajiri na mafunzo. Na kama njia ya kuelekea maeneo mapya."
Wad Madani pia ni eneo lenye vituo vya afya vya kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na kitengo kikubwa zaidi cha matibabu ya saratani nchini Sudan.
Mji huo hapo awali ulikuwa kama kitovu cha mashirika mengi ya misaada yaliyokimbia Khartoum baada ya vita kuanza miezi minane iliyopita.
Lakini tangu kuchukuliwa kwa Wad Madani, nao wamelazimika kuondoka, wakihamia miji mbalimbali ya jirani.
Wimbi jipya la kuyakimbia makazi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, katika wiki iliyopita zaidi ya watu 300,000 wamekimbia Wad Madani na maeneo jirani.
Khadija, mama wa watoto watano, alikimbia kutoka kwenye mapigano huko Khartoum miezi saba tu iliyopita. Hatimaye mambo yalianza kuwa shwari kwake na kwa familia yake, hadi wiki iliyopita.
Mapigano yalipozuka Wad Madani, alijua lazima ahame tena.
"Niliwachukua watoto wangu na kuingia kwenye basi dogo ili kufikia kituo cha basi kilicho karibu," alisema.
“Kutoka hapo, tulichukua gari jingine ili tutoke nje ya jiji. Nilimpa dereva senti ya mwisho niliyokuwa nayo."
Khadija anasema aliona mamia ya familia wakiondoka kwa miguu, wakiwa wamebeba mizigo yote waliyoweza.
Baada ya kufika katika jiji la Sanar, takribani kilomita 100 kusini mwa Wad Madani, Khadija anasema hali wanayokabiliana nayo sasa ni mbaya zaidi kuliko ile ya Wad Madani.
"Tunakaa katika shule katika vitongoji vya jiji. Hakuna chakula au maji. Tunapaswa kulala chini," anasema.
"Angalau katika makazi ya Wad Madani, tulikuwa na chakula na huduma ya matibabu."
Watu waliobaki

Chanzo cha picha, Getty Images
Vipi wale waliochagua kukaa Wad Madani?
Abd-Elhamid (si jina lake halisi), profesa wa chuo kikuu anayeishi kaskazini mwa jiji, aliiambia BBC kuwa anakataa kuondoka nyumbani kwake.
"Nimekulia Wad Madani na sitatoka. Hata iwe hatari kiasi gani," anasema.
Abd-Elhamid anasema kulikuwa na nyakati za kutatanisha baada ya kuwasili kwa vikosi vya RSF katika kitongoji chake.
Profesa huyo anadai kuwa wanajeshi sasa wako "kila mahali" huko Wad Madani, wakiwa wamejenga vituo vya ukaguzi katika barabara kuu na kuzunguka vituo vyote vya serikali.
"Baadhi ya wapiganaji wao wameanza kupora kutoka kwenye magari na nyumba za watu walioachwa," anasema Abd-Elhamid.
Pia anadai, wapiganaji wa RSF wamewakamata wale wanaoaminika kuwa wafuasi wa Rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir. Bashir aliondolewa madarakani na mapinduzi ya kijeshi mwaka 2019.
“Maduka yamefungwa, hospitali hazina huduma na hakuna jeshi wala polisi. Ni wapiganaji wa RSF pekee walio hapa," anasema Abd-Elhamid.
"Wad Madani ni mji uliosalia mtupu."
Je, hali ya mzozo ikoje kwa sasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu mapigano yalipozuka mwezi wa Aprili, si jeshi la Sudan wala RSF waliopata ushindi mnono.
RSF inadhibiti karibu 70% ya mji mkuu, Khartoum, pamoja na majimbo manne kati ya mitano huko Darfur, na hivi karibuni, jiji la Wad Madani.
Wakati jeshi linatawala kaskazini na mashariki mwa nchi na karibu 30% ya mji mkuu.
Majaribio kadhaa ya kisiasa ya kujadili usitishaji vita wa kudumu yamewekwa mezani na Saudi Arabia, Umoja wa Afrika na Marekani katika kipindi cha miezi minane iliyopita, lakini hakuna lililofanikiwa.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Maryam Dodo Abdallah












