Muswada wa Fedha Kenya: Serikali yaondoa mapendekezo ya ushuru kwa bidhaa muhimu

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili, Nairobi

Serikali ya Kenya Kwanza imetupilia mbali mapendekezo makuu ya ushuru ambayo yamezua taharuki miongoni mwa Wakenya katika wiki za hivi majuzi.

Tangazo hilo lilijiri baada ya Rais William Ruto kuandaa mkutano wa kundi la wabunge katika Ikulu ya Nairobi, Jumanne.

Katika kikao na wanahabari baada ya mkutano huo , timu ya Ruto ilisema mapendekezo hayo yalitupiliwa mbali kufuatia zoezi la ushirikishwaji wa umma ambalo lilishuhudia Wakenya wakiibua upinzani dhidi ya mapendekezo hayo.

Miongoni mwa zilizopunguzwa ni ushuru wa mkate, gari na ushuru wa mazingira.

Yaliyobadilishwa katika mswada

Baadhi ya marekebisho yaliyofanywa katika mswada huo ni haya ;

1. Asilimia 16 ya VAT kwa mkate kuondolewa.

2. VAT kwenye usafirishaji wa sukari pia kuondolewa.

3. VAT kwenye huduma za fedha na miamala ya fedha za kigeni pia imeondolewa.

4. Hakuna ongezeko la uhamisho wa pesa kwa simu.

5. Asilimia 2.5 ya Ushuru wa Magari pia imeondolewa

6. Ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya mboga kuondolewa

7. Kodi za Mfuko wa Nyumba na Bima ya Afya ya Jamii zitakatwa kodi ya mapato. Hii inamaanisha kuwa ushuru hautavutia ushuru wa mapato.

8. Ushuru wa Mazingira utatozwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Kwa hivyo, bidhaa zinazotengenezwa nchini hazitatozwa ushuru huo.

9. Kwa hiyo, bidhaa zinazotengenezwa nchini, ikiwa ni sodo ,diapers, simu, kompyuta, magurudumu ya magari, hazitatozwa ushuru huo

10. Kiwango cha juu cha usajili wa VAT kimeongezwa kutoka KSh5 milioni hadi KSh8 milioni. Kwa hivyo hii inamaanisha kuwa biashara nyingi ndogo hazitahitaji tena kujiandikisha kwa VAT.

11. Matumizi ya ETIMS, yameondolewa kutoka kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo kwa mauzo ya chini ya Ksh. milioni 1

12. Ushuru wa bidhaa utatozwa kwa mayai , vitunguu na viazi vinavyoagizwa kutoka nje ili kuwalinda wakulima wa ndani.

13. Ushuru wa bidhaa kwa vinywaji vyenye kileo sasa utatozwa ushuru kwa msingi wa kiwango cha pombe na sio kiasi. Kadiri kiwango cha pombe kilivyo juu ndivyo ushuru wa bidhaa utakavyozidi. Kwa hivyo, watengenezaji wa pombe wanatarajiwa kutengeneza pombe salama na ya bei nafuu.

14. Msamaha wa michango ya pensheni kuongezeka kutoka Ksh. 20,000 kwa mwezi hadi Ksh. 30,000 .

Kukamatwa kwa waandamanaji

Awali polisi waliwakamata makumi ya waandamanaji katika mitaa ya Nairobi huku baadhi ya Wakenya wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Mswada wa Sheria ya Fedha umezua malalamiko makubwa ya umma, huku wakosoaji wakisema kuwa utaweka mzigo wa kifedha usiofaa kwa raia ambao tayari wanakabiliana na matatizo ya kiuchumi.

Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kawaida waliwakamata waandamanaji waliokuwa wakikusanyika katika maeneo mbalimbali ya mikutano katikati mwa jiji na Nairobi.

Wakenya waliojaribu kukusanyika katika sehemu mbali mbali za jiji walikamatwa na polisi .

Walipelekwa hadi katika vituo mbalimbali vya polisi jijini huku polisi wakiimarisha doria karibu na Nairobi.