Shambulio la shule Uganda: 'Nyimbo za Injili zilikatizwa na mayowe'

t
Maelezo ya picha, Mary Masika, anayeishi mkabala na shule hiyo anasema mara nyingi alikuwa akiwasikia wanafunzi wakiimba kabla ya kulala

Na Ashley Lime & Anne Okumu

BBC News, Mpondwe

Wanafunzi nchini Uganda walikuwa wakiimba nyimbo za injili kabla ya shambulio baya la wanamgambo wa Kiislamu siku ya Ijumaa, mwanamke anayeishi mkabala na shule hiyo anasema.

"Kisha nikasikia mayowe," Mary Masika aliambia BBC. Shambulio hilo baya la Mpondwe lilisababisha vifo vya takriban watu 40.

Wanamgambo wenye uhusiano na Islamic State wamelaumiwa kwa shambulio hilo.

Kundi la Allied Democratic Forces (ADF) liliundwa miaka ya 1990 na kuchukua silaha dhidi ya Rais Yoweri Museveni, kwa madai ya kuwatesa Waislamu.

Wapiganaji wake wanaishi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shule ya Sekondari ya Mpondwe Lhubiriha iliyoshambuliwa Ijumaa iko karibu na mpaka.

Bi Masika anasema yeye na wakaazi wengine wameingiwa na hofu kutokana na shambulio hilo lililochukua takriban dakika 90.

Maelezo ya video, Shambulio la shule Uganda:Nilijipaka damu mwili wote ili kujificha

Onyo: Ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuhuzunishwa nayo

"Sijaweza kula wala kulala tangu wakati huo," aliambia BBC kwa Kiswahili.

Wanafunzi kwa kawaida huimba kabla ya kulala - na mwanzoni yeye na binti yake walifikiri kelele iliyokatiza nyimbo zao mwendo wa saa 22:00 (20:00 GMT) iliashiria kwamba walikuwa na furaha.

Lakini muda mfupi baadaye ikawa wazi kuwa kuna jambo la kutisha lilikuwa likiendelea katika shule hiyo, ambayo ilikuwa na wanafunzi wapatao 60 wanaoishi humo ndani.

Waasi wa ADF walikuwa wameingia kwenye mabweni na kuyachoma moto na kutumia mapanga kuua na kuwalemaza wanafunzi.

Familia moja huko Mpondwe ilifanya mazishi siku ya Jumapili kwa baba na mwana waliouawa katika shambulio hilo - mlinzi Elphanas Mbusa mwenye umri wa miaka 47 na Masereka Elton mwenye umri wa miaka 17.

th
Maelezo ya picha, Hurubana Kimadi Onesmus alipoteza mtoto wake wa kiume, mlinzi wa shule, na takriban mmoja kati ya wajuu zake - haijulikani ikiwa mwingine ametekwa nyara.

Mwana wao mwingine, Brian Muhindo mwenye umri wa miaka 15 ambaye pia alikuwa akisoma shule hiyo, hayupo. Hawajui kama ni miongoni mwa wavulana sita waliotekwa nyara au mmoja wa wale ambao miili yao haiwezi kutambuliwa kwa sababu wamechomwa vibaya sana.

Hurubana Kimadi Onesmus aliambia BBC kuwa alipata ugumu kuelewa jinsi wavamizi hao walivyoweza kujipenyeza katika shule ambayo mwanawe, mlinzi wa usalama, alifanya kazi na wajukuu zake walikuwa wakisoma.

"Kuna uwepo mkubwa wa kijeshi katika eneo hilo," mzee huyo wa miaka 69 alisema.

th
Maelezo ya picha, Timu ya BBC ilipewa dakika chache kupiga picha eneo la tukio shuleni huko Mpondwe

Sasa kuna ulinzi mkubwa shuleni - na timu ya BBC ilipewa dakika chache tu kupiga picha za majengo yaliyoteketea.

Lilikuwa tukio lenye kuhuzunisha na kukasirisha.

Damu nyingi zilizokauka bado ziko chini nje ya bweni la wasichana hao - walishambuliwa kwa mapanga na wengine kupigwa risasi na kufa walipokuwa wakikimbia.

Bweni la wavulana lilikuwa limefungwa - ama walikuwa wamekataa kuwafungulia waasi au walifungiwa ndani na wao. Wanamgambo hao walimwaga mafuta kwenye jengo hilo na kuliteketeza.

Ndani ,harufu ya kifo haieleweki - vitanda vimepunguzwa kuwa wavu wa waya na vipande vya nyama bado vimekwama kwenye vyuma.

th
Maelezo ya picha, Haijabainika ikiwa milango ya bweni la wavulana ilifungwa na wale waliokuwa ndani au waasi

Bi Masika alisema kuelekea mwisho wa shambulio hilo, mwendo wa saa 23:30, alimsikia mmoja wa washambuliaji akizungumza kwenye lango lake na kumuuliza mpiganaji mwenzake kama "kazi imekamilika".

Walikuwa wakizungumza kwa Kiswahili - lugha inayotumika katika eneo hilo - na baadaye wakaanza kupiga kelele "Allahu Akbar", kumaanisha "Mungu ni mkuu".

Alisema baada ya nyimbo hizi mmoja wao aliongeza: "Tumefaulu kuyumbisha nchi ya Museveni."

th

Chanzo cha picha, AFP

Katika kujibu, Rais Museveni aliapa kutuma wanajeshi zaidi katika Milima ya Rwenzori, ambayo iko kando ya mpaka kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akisema: "Hatua yao ... ya woga, ya kigaidi ... haitawaokoa."

Eneo linalozunguka Mpondwe linaonekana kuwa na mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu. Baadhi ya waliohudhuria mazishi siku ya Jumapili walikuwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya Kiislamu.

Mazishi mengine ya wanafunzi waliouawa katika shambulio hilo yalifanyika katika vijiji kote kanda, huku watu wengi wakiwa wamepigwa na butwaa na kuumizwa na ukatili wa shambulio hilo.

.