Kwanini kifo cha mwanablogu Albert Ojwang kimewatia polisi wa Kenya mashakani?

Albert Ojwang, alikuwa na mke na mtoto mmoja

Chanzo cha picha, Albert Ojwang / Facebook

Maelezo ya picha, Albert Ojwang, alikuwa na mke na mtoto mmoja
    • Author, Wycliffe Muia, Barbara Plett Usher & Brian Waihenya
    • Nafasi, BBC News, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

"Kijana wangu aliuliwa kama mnyama," alisema Meshack Ojwang, kabla ya kububujikwa na machozi mbeli ya wanahabari nje ya kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi, Kenya.

Mwnawe wa kipekee Albert Ojwang alikamatwa katika kijiji cha Kakoth, karibu na mji Homa Bay, magharibi mwa Kenya siku moja kabla - Jumamosi Juni 7, 2025 - alipokuwa akila chakula na mke wake Nevnina Onyango.

Mmoja kati ya maafisa watano waliokamatwa aliimbi afamilia hiyo kwamba alituhumiwa kumtukana mkuu wa pilisu katika mitandao ya kijamii.

"Tuliwauliza polisi kama atakuwa salama, kwa sababau tumewahi kusikia visa vya vya baadhi ya watu kutekwa," Bi Onyango aliiambia BBC. "Walituhakikishia kwamba yupo kwenye mikono salama, kiasi cha hata kutupatia nambari zao za simu kwa ajili ya mawasiliano."

Wakati Bw Ojwang alipofikishwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central mwedo wa saa tatu unusu usiku wa Jumamosi aliruhusiwa kumpigia simu mke wake.

"Tulipozungumza, aliniambia: 'Ingawa nina msongo wa mawazo, usiwe na wasiwasi. Tutakutana hivi karibuni.'Nadhani hiyo ndio iliyokuwa kauli yake ya mwisho," alisema.

Lakini baba yake alikuwa na wasiwasi akaamua kusafiri takriban 350km kumfuatilia mwanawe jijini Nairobi - alichukua hati ya miliki ya ardhi ya familia yake kama dhamana endapo atahitajika kufanya hivyo.

Anasema aliwasili Nairobi alifajiri ya Jumapili na kulipopambazuka akaelekea katika kituo cha polisi kumjulia hali mwanawe. Baada ya kusubiri kwa saa kadhaa hatimaye aliambiwa kuwa mwanawe amefariki kutokana na majeraha ya kujidhuru mwenyewe.

Alisimulia kwa mshangao jinsi alivyouona mwili wa mwanawe Albert Ojwang akiwa amesimama kando ya wakili wake: "Alikuwa natokwa na damu puani na alikuwa na majeraha usoni na sehemu zingine mwilini. Pia hakuwa na shati, kwa hakiki hivi sivyo nilivyomuwasilisha kwa polisi siku ya jumamosi."

Jamaa za marehemu wakililia nje ya makafani baada ya kuuona mwili wa Albert Ojwang - Jumamosi Juni 14, 2025.

Chanzo cha picha, Hassan Lali / BBC

Maelezo ya picha, Wazzai wa Albert Ojwang wamelemewa na machungu ya kumpoteza mwana wao wa pekee
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maelezo anayotoa kuhusiana na kile kichomsibu na hatua yake ya kutosalia kimya imewagusa Wakenya ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuangazia suala hilo na hatimaye hashtag ya #JusticeForAlbertOjwang ikaanza kusambaa kwa kasi, wito wa uchunguzi ukitolewa.

Kenya ina historia ya ukatili wa polisi, lakini kisa cha Albert Ojwang kimelishangaza taifa - sio mazingira yaliyozunguka kifo chake mikononi mwa polisi, lakini pia madai yaliyofuata kwamba polisi walijaribu kula njama ya kuficha kilochojiri.

Bunge liliwataka wakuu wa usalama ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Polisi, Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Waziri wa Usalama na Masuala ya ndani na Mamlaka Huru ya inayosimamia Huduma ya Polisi (IPOA) kuhojiwa.

Ni vigumu kuelewa jinsi mhitimu wa Shahada ya Elimu mwenye umri wa miaka 31 angeweza kufa katika mazingira ya kikatili namna hiyo.

Ni wazi kuwa babake, ambaye aliwahi kufanya kazi yauchimbaji mawe kusini-mashariki mwa Kenya, alijivunia kwamba mwanawe alikuwa mtiifu licha ya kukulia katika mazingira magumu.

"Hawezi kamwe kumuumiza mtu yeyote mtandaoni au kumduru kimwili," David Bwakali, mwanafunzi mwenzake wa zamani katika Shule ya Sekondari ya Kituma, aliambia gazeti la Daily Nation nchini Kenya.

Albert Ojwang, shabiki wa soka wa Manchester United, alikuwa akifundisha masomo ya kidini, historia na raga katika shule ya Mwatate kusini-mashariki mwa pwani ya Kenya.

Alikuwa amehudumu kwa mihula michache tu mwaka jana kwa sababu alikuwa ameajiriwa kwa kandarasi ya kibinafsi kupitia bodi ya usimamizi ya shule.

Hili ni jambo la kawaida kwa walimu wapya - hakuwa amemaliza muda mrefu kutoka Chuo Kikuu cha Pwani - na mipango kama hiyo inaelekea kutolipwa vizuri.

Bw Bwakali alisema rafiki yake alikuwa amewasiliana naye hivi majuzi ili kujadili jinsi alivyotarajia kupata kazi kama mwalimu wa shule ya umma.

Na ulikuwa wakati wa kusisimua kwa Bw Ojwang, ambaye aliishi katika mji wa pwani wa Malindi, kwani yeye na mkewe mwenye umri wa miaka 26 walikuwa wamerejea nyumbani kwao Homa Bay kwa ziara ya muda mefu ili aweze kutambulishwa rasmi kwa familia yake.

Walisafiri kwenda nyumbani kwao mwezi wa Aprili na walikuwa wameenda wakihalalisha ndoa yao kulingana na mila za jamii ya Wajaluo.

Sehemu ya mila hizi ilihusisha kurekebisha "simba" - au pedi ya bachelor ndani ya nyumba ya baba yake - kuwa nyumba inayofaa kwa wanandoa na mtoto wao wa miaka mitatu George.

Alikuwa akiwasaidia wazazi wake kwa kufanya kazi za shambani kwenye shamba la ekari mbili la familia hiyo - na yeye na mkewe walikuwa wakipanga mipango ya maisha yao ya baadaye na kuhitimu kwa Bi Onyango kama mfanyakazi wa afya.

Bw Ojwang pia alikuwa akijaribu kujikimu kimaisha kama muandaaji wa maudhui ya kidijitali - na alikuwa sehemu ya vuguvugu la vijana kwenye mitandao ya kijamii wakiangazia mada kama vile masuala ya kisiasa na kijamii.

Hiki ndicho kilichosababisha kifo chake.

Nevnina Onyango, mjane wa Albert Ojwang

Chanzo cha picha, Hassan Lali / BBC

Maelezo ya picha, Nevnina Onyango, mjane wa Albert Ojwang

Haijabainika ilikwa na wafuatiliaji wangapi katika mtandao wa X kwa sababu akaunti yake ilifutwabaada ya kukamatwa kwake, lakini washawishi wenzake mitandaoni walisema alikuwa na uwepo mkubwa mtandaoni na mara nyingi alishiriki katika kampeni za mitandao ya kijamii.

Alitumia jina la kisiri - jambo ambalo si la kawaida kwa Wakenya mtandaoni kutokana na msako wa hivi majuzi dhidi ya upinzani wa vijana.

Wanaharakati wamehusisha kifo chake na mwelekeo mpana wa kutoadhibiwa kwa polisi, wakitoa mfano wa vifo ambavyo havijasuluhishwa vya zaidi ya vijana 60 wakati wa maandamano ya kupinga nyongeza ya ushuru mwaka jana.

"Kifo cha Ojwang si tukio la pekee bali ni inazua kumbukumbu ya kusikitisha wa kutoadhibiwa na tabia ya uhuni ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS)," Mkurugenzi shirika la kutetea haki la MUHURI na mtetezi maarufu wa haki za binadamu, Khelef Khalifa, aliambia vyombo vya habari vya ndani.

Lakini jambo lisilo la kawaida katika kesi ya Albert Ojwang ni jinsi uchunguzi wa kina ulivyofanywa kwa haraka. Aidha, siku mbili za vikao vya bunge vilivyopeperushwa kwa njia ya televisheni zimemaanisha kuwa Wakenya wamesikia wenyewe maelezo ya kutatanisha kuhusu kile kilichosababisha kifo chake.

Alipofika mbele ya bunge Jumatano iliyopita, mkuu wa polisi Douglas Kanja alilazimika kubatilisha taarifa ya awali ya polisi iliyosema kuwa Bw Ojwang alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika seli yake na kukimbizwa hospitalini, ambapo alifariki kutokana na majeraha ya kichwani baada ya kujigosha kichwa chake ukutani.

Uchunguzi wa mwili wake ulioamriwa na IPOA ulifutilia mbali uwezekano kwamba mwanablogu huyo alijiua.

Mkuu wa polisi aliomba msamaha na kwa kutoa maelezo "kupotosha" akilaumu maafisa wake kwa dosari hiyo.

Aliendelea kusema kuwa kukamatwa kwa Bw Ojwang kumetokana na machapisho ya kashfa mtandaoni yanayomlenga naibu wake, Eliud Lagat - ambaye amejiondoa kupisha uchunguzi.

Bw Lagat alisema kuwa alikuwa akifanya hivyo kwa "nia njema" ya majukumu yake kama Naibu Mkuu wa Polisi na kwamba atatoa usaidizi wowote awezao katika uchunguzi wa kifo cha mwanablogu huyo.

Kulingana na taarifa ya Bw Kanja bungeni, nyadhifa hizo kwenye X zilidai kuwa Bw Lagat alikuwa akiendesha shughuli za ufisadi katika polisi kwa kuwaweka maafisa wanaoaminika katika idara maalum na zamu za trafiki "kudhibiti vyanzo vya mapato na mtiririko wa kijasusi".

Taarifa ya Bw Kanja ilieleza kwa kina machapisho mbalimbali likiwemo lililodai Bw Lagat alikuwa akichunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na picha yake na maneno "Mafia Cop".

Kulingana na taarifa ya Inspekta Jenerali wa Polisi bungeni, Bw Lagat alikuwa amewasilisha malalamishi kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI tarehe 4 Juni kuhusu machapisho yanayomharibia sifa mtandaoni.

Siku iliyofuata wakati EACC ilithibitisha kwamba hakukuwa na uchunguzi wowote kuhusu Bw Lagat, polisi waliendelea na kile kilichochukuliwa kuwa "kesi mbaya" chini ya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao.

Bw Kanja alisema Mamlaka ya Mawasiliano ilitafutwa kuhusu akaunti mbili zilizounganishwa na machapisho hayo. Hatua ambayo ilipelekea kukamatwa kwa mhusika mnamo Juni 5, ambaye alifichua kwamba yeye na wengine wanne walihusika katika kampeni hiyo - mmoja akiwa Albert Ojwang.

Siku mbili baadaye, polisi walimtafuta Bw Ojwang hadi kijijini kwao magharibi mwa Kenya.

Kifo cha Albert Ojwang kumesababisha maandamano makubwa

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha, Kifo cha Albert Ojwang kumesababisha maandamano makubwa

Katika ushuhuda wake, Makamu Mwenyekiti wa IPOA Anne Wanjiku alitoa maelezo ya kushangaza kuhusu saa chache za mwisho za maisha ya Bw Ojwang.

Alisema mashahidi wawili, waliokuwa katika seli jirani, waliiambia IPOA kwamba walisikia mayowe usiku aliofariki.

Wachunguzi wa IPOA wanadai kuwa fundi alilipwa $30 (£22) ili kukatiza kamera za CCTV katika kituo hicho.

Baada ya vikao vya Bunge kukamilika, maafisa wawili wa polisi walikamatwa kuhusiana na kifo cha Bw Ojwang.

IPOA, inayowasilisha kesi hiyo, ilisema afisa mdogo PC James Mukhwana aliwaambia wachunguzi nia ilikuwa "kumtia adabu" Bw Ojwang, sio kumuua.

Alisema afisa anayesimamia kituo hicho, Samson Talam, alipigiwa simu na Bw Lagat na agizo hilo na kumpa askari huyo dola 15 za kuwalipa wafungwa wawili ili wampige Bw Ojwang.

Bw Talam, kupitia kwa mawakili wake, amekanusha madai hayo na Bw Lagat hajazungumza lolote.

Chini ya sheria za Kenya, watu walio chini ya ulinzi wa polisi wana haki ya ulinzi mahususi, ikijumuisha haki ya uwakilishi wa kisheria na mawasiliano na mawakili au watu wanaomuunga mkono.

Familia ya Bw Ojwang ingali inatatizika kupokea hasara yao.

"Sikuamini hadi nilipouona mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti," alisema Bi Onyango, akiambia BBC kuwa ulikuwa na dalili za kuteswa. Ilikuwa kama "vitu ambavyo tunaviona tu kwenye sinema... sijawahi kuona mwili kama huo. Ilikuwa inavunja moyo sana," alisema.

Rais William Ruto, ambaye aliahidi kukomesha historia ya Kenya ya ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela alipoingia mamlakani mwaka wa 2022, amesema kwamba amepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko makubwa, akisema: "Tukio hili ni la kusikitisha, lililofanyika mikononi mwa polisi, ni la kuvunja moyo na halikubaliki."

Aliwataka polisi kushirikiana kikamilifu ili kufanikisha "uchunguzi wa haraka, wa uwazi na wa kuaminika".

"Natarajia ukweli utabainika kuhusu yaliyompata Ojwang kwa wakati ufaao na haki itapatikana," aliongeza kusema.

Meshack Ojwang baba yake Albert Ojwang

Chanzo cha picha, Hassan Lali / BB

Maelezo ya picha, Meshack Ojwang baba yake Albert Ojwang

Hata hivyo takriban visa 160 vya mauaji ya washukiwa na kutoweka kwa watu katika mazingira ya kuatatnisha viliripotiwa kote nchini Kenya mwaka jana, kulingana na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC).

Mwenyekiti wa IPOA Ahmed Issack Hassan aliwaambia Wabunge alipohojiwa Alhamisi wiki iliyopita kwamba takriban watu 20 walifariki wakiwa mikononi mwa polisi katika muda wa miezi minne pekee iliyopita.

"Katiba yetu iko kama gazeti ambalo tuna soma leo na kesho tunasahau," babake Bw Ojwang aliambia BBC.

Mjane wa Bw Ojwang anasema kwa huzuni kuwa: "Sijui kitakachofuata, kwa sababu alikuwa mwenzi na rafiki yangu wa karibu... hayupo. Ninahisi kuwa gizani."

Lakini kama baba mkwe wake, Bi Onyango anaamini kuwa kisa hicho ambacho kimezua maandamano kinaweza kuleta mabadiliko makubwa.

"Nadhani kifo cha Albert kinapaswa kutufumbua macho, maana kimetuonyesha baadhi ya mambo yanayotokea kwenye seli ambayo labda hatuyajui.

"Ninawaomba Wakenya wenzangu kusimama kidete kuzungumzia suala hili, ili kila aliyehusika awajibishwe."

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi