'Liverpool bado inahitaji wachezaji makinda'

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Phil McNulty
- Nafasi, BBC Michezo
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kusonga mbele kwa Liverpool na kubeba taji la 20, kunaleta ishara nzito kwa wapinzani wao ambao lazima sasa wajaribu kuliondoa taji hilo la Ligi Kuu ya Uingereza kutoka vichwani mwao msimu ujao.
Kocha wa sasa wa Liverpool, Arne Slot alimrithi Jurgen Klopp.
Liverpool ilimsajili mlinda mlango wa Valencia raia wa Georgia, Giorgi Mamadashvili kwa thamani ya pauni milioni 29 msimu uliopita wa joto ili acheze msimu ujao, lakini mchezaji pekee aliyewasili alikuwa winga wa Juventus, Federico Chiesa kwa uhamisho wa pauni milioni 10.
Liverpool sasa watakwenda katika msimu wa mapumziko wa joto, na timu yao ya kuajiri, chini ya mkurugenzi wa michezo Richard Hughes, kwa maandalizi ya kuongeza wachezaji wa uzani wa juu.
Walinda lango
Kipa wa Brazil Alisson Becker ana umri wa miaka 32, sio mzee kwa umri wa kuwa golikipa. Ukiondoa jambo lisilotarajiwa, atakuwa chaguo la kwanza kwa msimu ujao.
Giorgi Mamardashvili atakuwa mshindani wake pale atakapo kuja.
Hilo lina maana Caoimhin Kelleher ataondoka. Kutakuwa na timu nyingi zinazomhitaji kulinda lango baada ya kuthibitisha ubora kwenye Ligi Kuu.
Safu ya ulinzi
Kuna maswali kwenye safu ya ulinzi, haswa katika nafasi ya mabeki wa pembeni. Hata uamuzi wa Virgil van Dijk kusaini mkataba mpya unaweza usizuie kuongezwa kwa beki wa kati.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trent Alexander-Arnold anatarajiwa kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho huru, naye Andrew Robertson ana umri wa miaka 31, kuna tetesi kuwa beki wa kushoto wa timu ya Bournemouth ya Hungary, Milos Kerkez atawasili kama mrithi wake.
Kiungo wa zamani wa Liverpool na timu ya England Danny Murphy ameiambia BBC Sport: "Van Dijk anabaki na atakuwa mhimili mkuu, hivyo iwapo kutakuwa na nyongeza inategemea mtazamo wa Arne Slot kuhusu Joe [Gomez] na Jarell Quansah. Dakika walizocheza msimu huu ni chache sana, kwa hivyo naamini anahitaji kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi."
"Virgil anakaribia umri wa miaka 34 kwa hivyo watataka kupata mtu ambaye atacheza mechi nyingi. Van Dijk akijeruhiwa hakuna mtu wa kucheza nafasi yake.
"Kumekuwa na uvumi juu ya kusajiliwa Dean Huijsen kutoka Bournemouth, wengine ni Micky van de Ven kutoka Spurs, Marc Guehi kutoka Crystal Palace na Jarrad Branthwaite wa Everton.
"Kama wana uhakika Gomez atakuwa fiti wanaweza wasitumie bajeti kuwasajili hao. Uimara wa Van Dijk katika umri wake, na uimara wa Ibrahima Konate pia, imekuwa sababu kubwa kwa nini Liverpool wamekuwa wazuri sana, lakini nadhani beki wa kati atatafutwa."
Kipaumbele cha Liverpool katika safu ya ulinzi kinaonekana kuwa beki wa kushoto, lakini kuibuka kwa Conor Bradley mwenye umri wa miaka 21 kumeleta kile kinachoonekana kama mbadala bora wa beki wa kulia iwapo Alexander-Arnold ataondoka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungo mkabaji
Kipaumbele kikubwa cha Liverpool msimu uliopita wa kiangazi kilikuwa kutafuta 'namba sita,' jambo ambalo liliwafanya kuchanganyikiwa wakati mchezaji wa Real Sociedad, Martin Zubimendi alipokataa ofa ya pauni milioni 52.
Slot aliondoa mshangao kwa kumtumia Mholanzi mwenzake Ryan Gravenberch katika nafasi hiyo.
Murphy anasema. "Ikiwa utakwenda nje na kutumia pesa kununua kiungo mkabaji, atataka kucheza badala ya Gravenberch. Lakini yeye, bila shaka amekuwa mchezaji bora zaidi wa safu ya kiungo katika Ligi ya Premia msimu huu.
"Kama anafanya vizuri, usimuondoe, nitashangaa kuona Liverpool wakileta mchezaji mpya katika nafasi hiyo.
"Kama ningekuwa Slot, ningemsihi Wataru Endo abaki. Nadhani ni mbadala mzuri. Anaweza kufanya kazi nzuri sana na anapendwa na mashabiki."
Ni mwisho wa Darwin Nunez?
Darwin Nunez amecheza misimu mitatu kamili Liverpool tangu akamilishe uhamisho pauni mlioni 85 kutoka Benfica – ni mchezaji wa kutegemewa.
Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amewekwa pembeni na Slot, ambaye pia amemkosa hadharani kuhusu tabia yake.
Mashabiki wa Liverpool hawajawahi kupoteza imani na Nunez, wanapenda mtindo wake wa kutumia nguvu, lakini inaonekana kama wakati wake umekwisha.
Murphy alisema: "Nadhani Darwin amepata nafasi nyingi. Lakini ni wazi kwa Slot kuwa huyo sio mchezaji wake pendwa. Nitashangaa ikiwa Darwin atabaki Liverpool."
"Nafasi yake pengine inaweza kutendewa haki na Jonathan David kutoka klabu ya Lille, ambaye yuko huru. Ukimtazama akicheza anaonekana kuwa na sifa za Ligi Kuu. Ana nguvu, mwepesi, mmaliziaji mzuri na rekodi ya kufunga huko Lille kwa misimu minne sasa na ana miaka 25 pekee."
Na Murphy ana pendekezo lingine karibu na nyumbani, nalo ni mchezaji wa West Ham United Mohammed Kudus.
Anasema: "Kudus ni hodari, mwenye ustadi na anaweza kucheza kama namba '10' au kushoto au kulia. Ana nguvu na ana kasi kubwa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapinzani wa Liverpoll
Kuporomoka kwa Manchester City kutoka viwango vya juu vya mataji manne mfululizo ya Ligi ya Premia na changamoto ya Arsenal kuliacha milango wazi kwa Liverpool.
Ingawa matarajio ya Liverpool kuongeza nguvu zaidi kwa timu ili kushinda mataji zaidi, Murphy anasema kutakuwa na maandalizi makali kutoka kwa wapinzani wao msimu ujao.
Alisema: "Ni ushindi wa mshtuko kwa washindani ambao labda hawakuona Liverpool ikifanya hivi na kikosi walichokuwa nacho.
"Ninashuku Mikel Arteta na Pep Guardiola walikaa msimu uliopita wa kiangazi na kusema 'Nafurahi Liverpool haijatumia pesa yoyote'.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












