WARIDI WA BBC: Mama kwanini ulinizaa hivi?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Unapobeba ujauzito, ni neema tu ya Mungu na kila mzazi maombi yake na matumaini huwa ni hatua zote kwenda salama hadi wakati wa kujifungua.

Lakini jiulize, inakuwaje, wakati umepata mtoto na badala ya jamii kufurahia, inakugeuka na kuanza kukusema na minong'ono kusikika kila unapojitokeza.

Ndani ya Waridi wa BBC, Asha Juma amezungumza na Phresha Kagonya Musamula aliyejifungua mtoto ambaye ni huntha pamoja na mwanawe Dalton Musamula ambaye awali alikuwa anafahamika kama Diana Musamula.

Phresha ambaye katika makala hii tutamtambulisha kama mama Dalton, anasema alibeba ujauzito wa mwanawe kama mtoto mwingine yeyote, lakini baadaye alianza kugundua kuwa mtoto anabadilika.

"Nilijifungua Dalton akiwa msichana, nikamaliza siku tatu, akaanza kubadilika sehemu zake za siri," anasema mama Dalton.

Mama huyo ameongeza kuwa hili lilimkosesha usingizi na kuzunguka kila aliposikia anaweza kupata usaidizi angalau mtoto wake arejee kuwa sawa.

Takwimu za sensa za kuhesabu idadi ya watu nchini Kenya mwaka 2019 ilirekodi rasmi watu 1,524 waliotambuliwa kama huntha.

Changamoto alizokumbana nazo

Hadi kufikia hapo, ilikuwa dhahiri kwamba Dalton ni huntha na haya ni maumbile, tofauti na ilivyokuwa kwenye fikra za mama Dalton kwamba anaweza kubadilisha hali hiyo.

"Nilitembea sana na Dalton nikitafuta usaidizi, lakini ikashindikana na hapo ndipo nilipogundua kuwa mtoto wangu ni huntha," anasema mama Dalton.

Kwa mama huyo ilikuwa mara ya kwanza sio tu kumuona mtoto akiwa na mabadiliko ya aina hiyo lakini pia kujua kwamba kuna wale ambao hujulikana kama huntha.

"Ilikuwa siku yangu ya kwanza kuona huntha na ni hali iliyonitoa machozi sana kwa sababu ilifanya maisha yangu yakawa kwenye hatari," amesema mama Dalton.

Kulingana na yeye kumzaa mtoto huntha kulifanya akapitia aibu na mateso katika eneo ambalo alikuwa ameolewa.

Kwa uelewa waliokuwa nao, walidhani kuwa chanzo cha mama Dalton kumpata mtoto kama huyo ni kwa sababu alitembea nje ya ndoa yake kwa kuwa ndani ya familia yao walidai hawajawahi kupata mtoto kama huyo.

"Walianza kunitenga na kunong'ona kila waliponiona," Mama Dalton anakumbuka.

Lakini bahati nzuri ni kuwa, alikozaliwa, wazaze wake wakiwa bado wako hai, walimkubali na mwanawe na kumweleza kwamba hilo ni jambo la kawaida ingawa hakuna anayesema hadharani.

Pia, mama Dalton alirejea hospitali kueleza kile alichokiona na hapo ndipo walipomfahamisha kwamba kuna watoto wengine ambao ni huntha wake akiwa mmoja wao.

Lakini kigumu zaidi ni pale ambapo mtoto wake aliyeamua kukua naye kila hatua alipoanza kuuliza maswali magumu.

"Dalton alikuwa akiniuliza, mama kwanini ulinizaa hivi? Alikuwa akilia kila wakati, ni mimi peke yangu ndio uliona unizae hivi, "mama Dalton anakumbuka.

Anasema wakati huo alikuwa akimuarifu mtoto wake kwamba ni mapenzi ya Mungu yeye kuwa jinsi alivyo.

Ila licha ya kwamba changamoto ni nyingi, lakini kama mzazi aridhie hali ya mtoto wake, ndilo aliloona kuwa mtihani mkubwa zaidi.

Mama huyo anasema ilimchukua muda mrefu moyo wake kukubali hali anayokumbana nayo kwa kuwa hakuna aliyetaka kuwa karibu na mtoto wake.

"Ni vigumu, hata kukubali hali yenyewe ni vigumu kwa sababu si kitu ambacho nilikuwa nakitarajia maishani mwangu, lakini nilikuja kukubali kwa sababu ni Mungu ndiye anayeumba" anasema mama Dalton.

"Nilikaa sana, ndiyo nije kukubali hali hii. Nilikuwa nikilia katika maisha yangu yote. Ilikuwa kama kidonda kisichopona," Mama Dalton anasema.

Anaongezea kuwa hali ya mtoto wake imemfanya hata hana marafiki.

Jinamizi la kujitambua

Dalton Musamula ambaye awali alijulikana kama Diana anasema alianza kabisa kujua kuwa yeye ni tofauti na wototo wengine wakati alipokuwa anabalehe.

"Nilianza kuona nina utofauti kwa mwili wangu na mtu wa kawaida ama mwanamke au mwanamume," Dalton anasema.

"Mimi nilililewa kama msichana lakini kila nikijiangalia nikawa nimeanza kuwa kama mvulana," anaongeza Dalton.

Mwili wa Dalton ulibadilika na bado hakuna ambaye alielewa kuwa ilipofikia yeye sio Diana tena.

"Mimi sio tu nilimuona mama hanielewi, kuna kipindi ambapo niliona kila mtu hanielewi. Na singeweza kuwalaumu kwa sababu hakika hakuna aliyekuwa ananielewa. Wao waliegemea sana upande wa kuwa mimi ni msichana kwa sababu wamenilea kama msichana," Dalton anakumbuka.

"Na wakati huo mabadiliko niliokuwa napitia yalikuwa ya mtoto wa kiume kabisa," amesema Dalton.

Alikuja kubaini kabisa kinachoendelea mwilini mwake alipomaliza mtihani wa darasa la nane.

Mama Dalton anasema mtoto wake alipita mtihani na kupata shule ya bweni ya wasichana lakini mwili wake ulianza kubadilika kwa haraka sana.

Wakati nikifanya mahojiano na Dalton nilitaka kujua, aliishi na wanafunzi wenzake namna gani hasa ukizingatia kwamba amesoma shule zaidi ya 10 kwa sababu kila alipokuwa akigunduliwa shuleni kwamba hayuko kama watoto wengine, alifukuzwa na kumlazimu ahamie shule nyingine.

"Mama alikuwa akiniambia, hakikisha ukiwa shuleni unaenda haja ukiwa peke yako, watoto wengine wasikuone," Dalton anasema.

Lakini anaongeza kuwa siku ambayo hataisahau ni pale alipodhalilika shuleni.

"Niligundulika kuwa mimi ni huntha, walimu waliniita, wakanitoa nguo afisini na walipohakikisha kuwa mimi ni huntha, walinifukuza,"Dalton anasema.

Nani alizungumza na Dalton kumuelezea huntha ni nani?

"Kusema kweli sikuwa na mtu wa kunikalisha na kunielezea nilivyo, nilibaki peke yangu. Hata wakati nilipoamua kuwa mvulana, sikuwa na Baba wa kunielezea mtoto wa kiume anafaa kuwa vipi," Dalton anasema.

"Nikiwa shule ya upili nilikuwa nimejijua na nikaamua kuwa sasa nitajitokeza kama mvulana, na pia watoto walikuwa wananikejele na hilo ndio lilinipa nguvu ya kufunguka kabisa kuhusu hali yangu na kujitokeza kama Dalton kwa kujiamini," anasema.

Dalton aliamua kuchua hatua na kuanza kufanya uchunguzi zaidi kuhusu huntha, sio tu kwa ajili yake lakini pia kwa wengine kama yeye watakaokuja na kutaka kufahamu mengi zaidi.

Dalton anasema kuna mahali dunia ilimuelewa vibaya.

"Pale ambapo hakuna mtu anayetaka kuamini kwamba huntha wako. Hasa wakati ambapo nimeenda sehemu kupeleka stakabadhi zangu halisi. Ingawa leo mimi ni mwanamume, bado zina jina ni Diana, na kila anayeziona stakabadhi zangu na muonekano wangu ulivyo, huishia kuwa na maswali mengi zaidi ya majibu," Dalton anasema.

Ushauri

Aidha, mama Dalton anasema mtu anapokuwa na ujauzito ni vyema kukubali chochote kile utakachozaa kwa sababu mwenye kuumba ni Mungu. Na pia kwa mwenye mtoto kama wake asimfiche.

"Mzazi kama mimi mwenye mtoto kama huyu wangu, asimtupe kwa sababu amekataliwa. Hayo ni mapito na Mungu akikupa mtoto huwa anajua kwa nini amekupa," Anasema mama Dalton.

Kenya inaendeleza juhudi za utambuzi wa kisheria na kijamii wa watu wa jinsia tofauti, huku hatua zilizopigwa hivi majuzi zikilenga kujumuisha huntha kama "jinsia" ya tatu katika usajili rasmi wa cheti za kuzaliwa.

Katika sajili ya waliozaliwa mwaka 2024, watoto 41 walitambuliwa kama ambao hawakuwa na jinsia ambayo ingeweza kutambuliwa ama mvulana au msichana.

Hisia ni kwamba kuna uwezekano wa kuwa na wengine ambao bado hawajatambuliwa rasmi.

Hata hivyo, ingawa hatua zimeanza kupigwa hata kama ni kwa mwendo wa kobe, bado changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na ubaguzi, kutengwa na pia kupata huduma umma.

Vile vile, wazazi bado wanaona aibu kutambua watoto wao kama huntha wakihofia changamoto zinazowakodolea macho.

Lakini, Dalton anasema matarajio yake ni kwamba iko siku itafika na ajione yuko huru, anashiriki kwenye kupiga kura na kuingia popote bila kuulizwa maswali na kushukiwa vibaya.