Kwa nini Iran inayaona makubaliano yake na Marekani kuwa ni ushindi?

    • Author, Khasheyar Joneidi
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Serikali ya Iran na vyombo vya habari vya serikali vinasema makubaliano ya kusitisha mapigano kati yake na Marekani ni ushindi mkubwa kwa utawala huo.

Taarifa iliyotolewa na Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran inasema Iran imefanikiwa katika malengo yake karibu yote katika vita hivi, na adui ameshindwa.

Mwanzoni mwa vita, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu Ali Khamenei na majenerali wakuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu waliuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israeli.

Mapigano haya yalitoa tishio la kuanguka kwa utawala huo, na kwa Iran yalikuwa ni mapambano ya kunusurika.

Kwa hivyo, wanajiona kuwa washindi kwa sababu wamenusurika katika vita hivi vya Marekani na Israeli vilivyodumu kwa zaidi ya siku 30. Kwa hivyo, kauli hii ya Iran ya ushindi ina umuhimu wake.

Wiki mbili zijazo

Huku mazungumzo yakiendelea tena, ni lazima ikumbukwe kwamba kuna kutokuaminiana kukubwa kati ya Marekani na Iran.

Mwaka uliopita, Iran na Marekani zimefanya mazungumzo mara mbili, na mara zote mbili, vita vilizuka katikati ya mazungumzo.

Haijalishi Iran inajionyesha kuwa imeshinda kwa kiasi gani kupitia vyombo vya habari vya serikali, lakini iko katika hali dhaifu sana.

Jeshi lake limepata hasara kubwa, uchumi wake uko katika hali ngumu, na chama tawala kina uhusiano mbaya sana na upinzani. Zaidi ya hayo, umma hauna maoni chanya kuhusu serikali.

Katika siku za hivi karibuni, serikali imewaua baadhi ya watu waliokamatwa wakati wa maandamano ya Januari.

Ushawishi wa serikali kwa umma umepungua. Iko katika hali ngumu sana, lakini madai yake ya ushindi ni magumu kwa Marekani kuyakubali.

Marekani inasema imekubali kusitisha mapigano kwa sharti kwamba usafiri wa baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz uendelee bila kukatizwa.

Iran inasema inataka udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa sababu ya eneo lake la kijiografia, na hicho ndicho kipaumbele chao kikubwa kwa sasa.

Kutakuwa na mazungumzo magumu sana kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinasema Marekani imekubali kuruhusu urutubishaji wa urani nchini Iran.

Lakini Marekani imesema inataka kusiwe na aina yoyote ya urutubishaji wa urani nchini Iran.

Wiki mbili zijazo zitakuwa ngumu sana.

Maoni ya Wairani

Ulikuwa ni usiku mrefu kwa Wairani. Wengi waliogopa kwamba vitisho vya rais wa Marekani, Donald Trump vingesababisha mabomu makubwa, na kulenga mitambo ya umeme, barabara na madaraja.

Kila mtu alikuwa akisubiri tarehe ya mwisho, ambayo ilikuwa ni asubuhi Jumatano jijini Tehran.

Usitishaji mapigano ulitangazwa jijini Tehran usiku, lakini watu wengi walikuwa bado macho.

Mkataba huo umepokewa kwa maoni tofauti.

Katika siku chache zilizopita, watu wamekuwa wakinunua mboga, vyakula na mishumaa, pamoja na kuhifadhi maji, wakihofia kukatika kwa umeme.

Sasa wamefarijika kiasi kwamba mitambo ya umeme haitashambuliwa.

Kwa upande mwingine, wengi wanaopinga utawala huo waliamini kwamba vita hivyo, pamoja na vitisho na hasara zake zote, vingesababisha mabadiliko ya utawala. Lakini hilo halikutokea.

Sasa wanapaswa kukabiliana na utawala ambao umejeruhiwa katika vita, na ambao uchumi wake pia umeporomoka.

Serikali ya huko sasa ina hasira zaidi kuliko hapo awali, na huenda isiwe mkarimu hata kidogo kwa wapinzani wake.