Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Kusitisha mapigano na Iran ni ushindi wa muda mfupi kwa Trump unaoweza kumgharimu"
Rais wa Marekani Donald Trump, amechapisha kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa Marekani na Iran karibu wanafikia "tamati" katika makubaliano ya amani, na kuwa amekubali kusitisha mashambulizi kwa wiki mbili ili kuruhusu mazungumzo yafanyike.
Trump alikuwa ameipa Iran hadi Jumanne jioni saa za Marekani kufikia makubaliano, vinginevyo Marekani ifanye mashambulizi mabaya kwa kulenga miundombinu ya uchukuzi na nishati nchini humo.
Sasa ni kusubiria na kufuatilia kuona iwapo Iran itasitisha mashambulizi yake na kukubali kufungua Mlango Bahari wa Hormuz na kuruhusu meli kupita.
Hatua hii haikuwa inatarajiwa itaafikiwa hivi karibuni baada ya tishio la Trump la kuiharibu Iran na kuirudisha "enzi za kitambo."
Haijulikani iwapo tishio la Trump liliishinikiza Iran kuafikia makubaliano ya kusitisha mashambulizi ambayo awali ilikuwa imekataa. Ila kile ambacho kiko wazi ni mabadiliko katika semi za Trump, baada ya kuitishia Iran siku mbili zilizopita kuwa "ataiangamiza kabisa".
Na iwapo makubaliano ya kusitisha vita kwa wiki mbili yataleta amani ya kudumu, vita vya Iran na matamshi ya Trump, yamebadili mtazamo wa Marekani kwa dunia.
"Hii haituwakilishi sisi"
Taifa ambalo wakati mmoja lilijulikana kudumisha amani ya dunia, limetikisa utaratibu wa kimataifa. Rais ambaye amekuwa akikiuka kanuni na desturi katika siasa za taifa lake, sasa anafanya hivyo katika jukwaa la dunia.
Wawakilishi wa chama cha Democrat walikashifu vikali matamshi ya Trump, wengi wakitaka aondolewe madarakani.
"Ni wazi kuwa maamuzi ya rais yameendelea kudorora na hafai kutuongoza" alisema mbunge Joaquin Castro kwenye ukurasa wake wa X.
Chuck Schumer seneta wa chama cha Democrat alisema kuwa kiongozi yeyote wa Replican ambaye hakupiga kura kumaliza vita dhidi ya Iran "atawajibikia madhara yote."
Austin Scott, Mbunge wa Republican kutoka Georgia na mwanachama wa Kamati ya huduma za kijeshi bungeni, alikosoa vikali vitisho vya Trump kuhusu kuiangamiza Iran kabisa
"Kauli za rais hazisaidii," aliliambia shirika la BBC, "na sikubaliani nazo."
Seneta wa Wisconsin Ron Johnson, ambaye mara nyingi humuunga mkono Trump, alisema itakuwa "kosa kubwa sana" kwa Trump kuendelea na kampeni yake ya kutekeleza mashambulizi . Mbunge wa Texas Nathaniel Moran aliandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba haungi mkono "uharibifu wa Iran."
"Hili halituwakilishi," aliandika, "na haliendani na misingi ambayo imeiongoza Marekani kwa muda mrefu."
Hata hivyo, White House huenda ikajibu kwamba mbinu hiyo ilifanikiwa.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akitangaza kusitishwa kwa mapigano, Donald Trump alidai kwamba Marekani ilikuwa "imetimiza na hata kuzidi" malengo yake yote ya kijeshi kwenye vita hivyo dhidi ya Iran.
Si suluhu ya kudumu
Jeshi la Iran limedhoofishwa pakubwa. Ingawa utawala wa Kiislamu bado uko madarakani, viongozi wake wengi wameuawa.
Ila malengo ya Marekani katika vita hivyo ni ya kutilia shaka. Hatma ya madini ya Urani na mpango wa nyuklia wa Iran bado haijulikani. Taifa hilo bado lina ushawishi wa makundi yenye silaha ukanda huo kama Wahouthi wa Yemen.
Katika taarifa baada ya Marekani kutangaza kusitisha mashambulizi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Aragchi alisema kuwa "Iran itasitisha mashambulizi yake ya kujilinda na kufungua Mlango Bahari wa Hormuz" aliongezea kuwa Marekani imekubali mapendekezo yenye vipengele kumi ya Iran kumaliza vita hivyo.
Mpango huo unajumuisha jeshi la Marekani kuondoka katika ukanda huo, Iran kuondolewa vikwazo, fidia ya vita, na kuruhusu Tehran kuendelea kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz.
Haijulikani iwapo Trump atakubali mapendekezo haya yote na huenda mchakato wa mazungumzo ukawa mrefu.
Ila kwa sasa hii inawasilisha ushindi wa kisiasa kwa Trump, alitoa onyo kali ambalo limezaa matunda. Ila kusitisha mapigano kwa muda si suluhu ya kudumu.
Athari ya muda mrefu ya vita hivi bado haijatathminiwa.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula