Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump amesema Marekani inafanya kazi kwa karibu na Iran

Trump anasema Iran haitarutubisha urani, na Marekani itashirikiana na Tehran "kuchimba na kuondoa 'chembechembe' zote za Nyuklia.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Serikali tupunguze matumizi makubwa ya mafuta- Rais Samia

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameelezea athari ya vita vya Iran kwa dunia nzima ikiwemo Tanzania, hususan katika kupanda kwa bei ya mafuta na upungufu wa mafuta.

    Aidha amesema kutangazwa kusitishwa kwa vita hivyo na kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz ni jambo la faraja.

    ''Hii inatupa matumaini makubwa sana kama serikali na ile kuruhusu tu meli za awali za Ufaransa,za Japan.....kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka kidogo sasa hii inatupa matumaini.'' Alisema.

    Lakini hata hivyo, amechukua hatua pia kupunguza matumizi makubwa ya mafuta yaliyopo serikalini kwa kuanzia kwanza na ofisi yake.

    "Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa ya mafuta, magari ni mengi, safari zetu ni nyingi niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta, kwa kuanza na ofisini kwangu ninapotembea kuanzia sasa wote nitawaingiza kwenye kibasi''.

    Aidha amesema upandaji wa bei ya mafuta umekuwa ukienda sambamba na kupanda kwa bei za bidhaa, hivyo amewataka wananchi kuwa watulivu.

    Maelezo zaidi:

  2. Madagascar yatangaza hali ya dharura kutokana na uhaba mkubwa wa mafuta unaohusishwa na vita vya Iran

    Madagascar imetangaza hali ya dharura kwa muda wa wiki mbili kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta uliosababishwa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Mamlaka zimesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kikao cha baraza la mawaziri Jumanne, kutokana na hofu kwamba hali hiyo inaweza kusababisha vurugu za kijamii.

    Kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, ambacho hutegemea mafuta kuzalisha sehemu kubwa ya umeme wake, kinategemea uagizaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati na usambazaji unatarajiwa kuathirika kwa muda, licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa wiki mbili kulikotangazwa usiku.

    Mwaka jana, kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme na maji nchini Madagascar kulisababisha maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo baadaye yaligeuka kuwa machafuko ya kisiasa na kusababisha jeshi kuchukua madaraka.

    Haijulikani wazi hatua mahsusi ambazo serikali inapanga kuchukua, lakini imesema sasa ina mamlaka ya kuimarisha sekta ya umeme, kupunguza usumbufu zaidi, kudhibiti matumizi, na kuhakikisha huduma za umma zinaendelea.

    Unaweza kusoma;

  3. Meli zaripotiwa kupita katika Mlango bahari wa Hormuz

    Kampuni ya kufuatilia meli, MarineTraffic imeonesha leo asubuhi kwamba kumekuwa na “dalili za awali za shughuli za meli” katika Mlango bahari wa Hormuz baada ya njia hiyo kuzuiwa kwa kiasi kikubwa na Iran.

    Shirika hilo linaeleza kuwa meli mbili zimepita katika mlango huo, moja inayomilikiwa na Ugiriki na nyingine iliyosajiliwa Liberia.

    BBC haijathibitisha taarifa hizi.

    Upitishaji wa meli katika mlango huo umekuwa chanzo cha mvutano katika wiki za hivi karibuni, na ingawa mpango wa muda mrefu kuhusu njia hiyo bado haujafahamika, makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa usiku kucha yanaitaka Iran kuufungua tena.

    Baadhi ya nchi zilikuwa tayari zimefikia makubaliano na Iran ili meli zao ziendelee kutumia njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa kimataifa zikiwemo Pakistan, India na Ufilipino.

    Nchi nyingine zilikuwa zimeshambuliwa katika maeneo karibu na mlango huo, pamoja na maeneo mengine katika Ghuba.

    Unaweza kusoma;

  4. Trump amesema Marekani inafanya kazi kwa karibu na Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amechapisha kwenye mtandao wa Truth Social, akisema kwamba Marekani itafanya kazi na Iran, "ambayo tumebaini imepitia mabadiliko makubwa ya utawala!"

    Trump anasema Iran haitarutubisha urani, na Marekani itashirikiana na Tehran "kuchimba na kuondoa 'chembechembe' zote za Nyuklia zilizo ardhini. (B-2 Bombers).

    "Sasa, na imekuwa, chini ya Ufuatiliaji mkali wa Satilaiti". Anaongeza: "Hakuna kilichoguswa tangu tarehe ya shambulio. Tunazungumza, na tutazungumza, kuhusu unafuu wa Ushuru na Vikwazo na Iran.

    Vipengele vingi kati ya 15 tayari vimekubaliwa."

    Unaweza kusoma;

  5. Mlinda lango Raya ataisaidia Arsenal kurejea kwenye mstari?

    David Raya ndiye kipa bora zaidi duniani, kulingana na wachezaji wenzake wa Arsenal.

    Kipa huyo wa Gunners aliokoa mipira minne katika mchezo wake wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Sporting, huku Kai Havertz akifunga bao la ushindi dakika za mwisho.

    Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania ameweka rekodi ya kufungwa mabao 22 katika mechi 41 katika mashindano yote msimu huu.

    Arsenal ilisafiri hadi Sporting na kiwango cha Raya dhidi ya Sporting kilionyesha kwa nini mchezaji huyo wa miaka 30 ndiye nambari moja kwa Gunners.

    Raya ameweka rekodi ya kutofungwa mabao mengi kuliko kipa yeyote katika ligi tano bora barani Ulaya, akiwa amefungwa mabao 22 tu katika mashindano yote mbele ya Yann Sommer wa Inter.

    Kipa huyo wa zamani wa Brentford amekuwa maarufu sana Arsenal na ni sehemu ya kundi la uongozi wa timu hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mwenyekiti wa tume ya AU aunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran

    Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ameunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, akielezea kama hatua muhimu kuelekea kupungua kwa mzozo wa kiuchumi na utulivu wa kikanda.

    Mahmoud Ali Youssouf alisema makubaliano hayo, yaliyotangazwa na waziri mkuu wa Pakistan, yanaonesha "uongozi unaostahili pongezi na kujitolea kwa pamoja" katika kupunguza mvutano kati ya pande hizo mbili na washirika wao.

    Alisema maendeleo hayo yanaendana na wito wa muda mrefu wa Umoja wa Afrika wa kuzuia na kusuluhisha migogoro kwa amani.

    Mwenyekiti wa AU pia alisifu jukumu la wapatanishi, ikiwa ni pamoja na Oman, Uturuki na Misri, ambao juhudi zao za kidiplomasia zilisaidia kupata usitishaji mapigano.

    Bw. Youssouf alionya kwamba athari za mgogoro huo zimeonekana zaidi ya eneo la karibu, ikiwa ni pamoja na kote Afrika, ambapo usumbufu wa usambazaji wa mafuta duniani umesababisha ongezeko kubwa la bei za mafuta na mfumuko wa bei.

    Kote barani, athari hizo zimeenea. Reuters inaripoti kwamba usumbufu wa mnyororo wa usambazaji unaohusishwa na mgogoro huo pia umeathiri masoko ya mbolea, huku bei zinazoongezeka na uhaba zikitishia uzalishaji wa kilimo katika nchi kadhaa za Afrika.

    Hii imezua wasiwasi kuhusu mavuno ya chini ya mazao na kuongezeka kwa ukosefu wa uhakika wa chakula, hasa katika nchi zinazotegemea uagizaji kutoka nje.

    Wachambuzi wanasema mataifa mengi ya Afrika yanategemea sana mbolea inayoagizwa kutoka nje, sehemu kubwa ikihusishwa na masoko ya nishati duniani na njia za usafirishaji zinazoweza kuathiriwa na mvutano wa kijiografia.

    Kadiri bei zinavyopanda, wakulima mara nyingi hupunguza matumizi, jambo ambalo linaweza kupunguza mavuno na kupanda kwa bei za chakula.

    Mwenyekiti wa Tume ya AU alielezea kuunga mkono mazungumzo ya Islamabad na akazitaka pande zote kudumisha kasi kuelekea azimio la kudumu, akisema diplomasia inabaki kuwa njia pekee inayofaa ya kutatua migogoro ya kimataifa.

  7. Zaidi ya vifo 1500 vimeripotiwa nchini Lebanon, Israel ikiapa kuendelea na mashambulizi

    Tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi mmoja uliopita, zaidi ya watu 1,530 wameuawa nchini Lebanon, baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya kuwalenga wapiganaji wa Hezbollah, Shirika la habari la AFP limeripoti.

    Idadi hiyo ya vifo kulingana na AFP ilitolewa na wizara ya afya ya Lebanon, ambayo inajumuisha vifo vya wanawake 102 na Watoto 130. Zaidi ya watu 4,812 wamejeruhiwa.

    Licha ya kusitishwa kwa mapigano nchini Iran, Israel imesisitiza kuwa makubaliano hayo hayajumuishi Lebanon na wataendelea kulenga kundi la Hezbollah.

    Katika wiki kadhaa zilizopita, Israel imewatuma wanajeshi wake kusini mwa Lebanon na kudhibiti eneo karibu na mto Litani, Israel ikiapa kuwa lazima iondoe tishio la Hezbollah.

    Mapema leo Israel imetekeleza mashambulizi kusini mwa Lebanon.

    Pia unaweza kusoma :

  8. Falme za kiarabu “ilishinda” vita hivyo

    Mshauri wa rais wa Falme za Kiarabu amesema kuwa taifa hilo “lilipata ushindi” baada ya kushambuliwa mara kadhaa na Iran tangu kuanza kwa vita hivyo.

    “Tulishinda kupitia ulinzi wa kitaifa wa kihistoria uliolinda uhuru, heshima, na kutunza mafanikio yetu baada ya kuchokozwa,” alisema Anwar Gargash.

    “Leo, tunasonga mbele tukikabiliana na mazingira magumu kwenye ukanda wetu tukiwa na nguvu zaidi, uelewa zaidi, na uwezo thabiti wa kushawishi mustakabali wa siku za usoni.”

    Wizara ya ulinzi ya taifa hilo imekuwa ikichapisha taarifa ya jinsi imekuwa ikidungua makombora ya Iran.

    Hapo jana katika taarifa waliyoitoa, tangu kuanza kwa vita hivyo wameweza kudundua ndege zisizo na rubani 2221, makombora ya majini 26 na makombora ya kibalistiki 520.

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Oman, ameipongeza Pakistan kwa juhudi zao za kuhakikisha mkataba huo unaafikiwa na kusema kuwa anatumai utakuwa wa kudumu.

    Pia unaweza kusoma;

  9. "Tutafanya kila tuwezalo kuunga mkono usitishaji mapigano" - Keir Starmer

    Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema `watafanya kila wawezalo kuhakikisha makubaliano ya kusitisha vita kwa muda nchini Iran yanadumu`

    "Tumepokea vyema makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa na yataleta afueni kwa ukanda huo na kote duniani` alisema Starmer

    "Pamoja na washirika wetu tutaunga mkono makubaliano hayo ya kusitisha vita hadi suluhu ya kudumu ipatikane na Mlango Bahari wa Hormuz ufunguliwe`

    Ofisi ya Waziri huyo mkuu imetangaza kuwa atasafiri kukutana na viongozi wa mataifa ya Ghuba na kutangaza atakavyounga mkono makubaliano ya kusitisha vita.

    Katika mikutano na viongozi wa kikanda, atasisitiza uungwaji mkono usioyumba wa Uingereza na hitaji la azimio la kidiplomasia la muda mrefu ili kuhakikisha usitishaji mapigano unapelekea makubaliano ya kudumu.

    Pia atashiriki katika mazungumzo kuhakikisha Mlango Bahari wa Hormuz unasalia wazi.

    Pia unaweza kusoma :

  10. Wairani wakusanyika mjini Tehran baada ya tangazo la kusitishwa mapigano

    Raia wa Iran wamekusanyika katika mji mkuu wa taifa hilo, Tehran, wakiwa wamebeba bendera ya taifa na mabango yenye picha ya Kiongozi Mkuu Mojtaba Khamenei.

    Raia wa Iran wamejitokeza katika barabara za mji wa Tehran baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda.

    Kusitishwa kwa vita hivyo kwa muda kumepokelewa kwa hisia mseto miongoni mwa raia wa Iran.

    Kuna afueni kwa sababu viwanda vya nishati havitashambuliwa tena, lakini kwa wale ambao wanapinga utawala wa taifa hilo, hawajalipokea vyema.

    Soma zaidi:

  11. Tumepata 'ushindi kamili' - Trump

    Rais Donald Trump wa Marekani amesema hakuna shaka kwamba Marekani imepata "ushindi kamili" baada ya kukubaliana kuhusu kusitisha vita kwa wiki mbili na Iran.

    Katika mahojiano na Agence France Presse baada ya tangazo lake, alisema kwamba urani iliyorutubishwa ya Iran "itajadiliwa kikamilifu" chini ya makubaliano hayo.

    "Vinginevyo nisingekubali," Trump alisema, bila kutoa maelezo yoyote kuhusu kile ambacho kingetokea kwa Iran.

    Alipoulizwa kama angerudi kutoa tena vitisho kama vya awali vya kuharibu mitambo ya nishati na madaraja ya Iran ikiwa makubaliano hayo yangevunjika, alichosema tu ni: "Utalazimika kufuatilia hili."

    Trump, ambaye anatarajiwa kusafiri hadi China mwezi ujao kukutana na mwenzake wa China Xi Jinping, alisema: "Nasikia hivyo" alipoulizwa kama Beijing ilihusika katika kumfanya mshirika wake mkuu Tehran kujadiliana kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Soma zaidi:

  12. Iran yajiona mshindi baada ya kustahimili vita dhidi ya Marekani na Israel

    Serikali ya Iran na vyombo vya habari vya taifa hilo vinasema kuwa makubaliano ya kusitisha mashambulizi kwa muda ni ushindi mkubwa kwa utawala wa taifa hilo.

    Katika taarifa iliyotolewa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Iran imesema imeafikia karibu malengo yake yote ya vita hivyo na kuwa adui wake amepata pigo la kihistoria.

    Ikumbukwe kwamba vita hivyo vilianza na kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa taifa hilo Ali Khamenei na viongozi wengine wakuu wakijeshi na hii ilikuwa tishio kubwa kwa utawala wa Iran.

    Iran inajiona mshindi kwa kuweza kustahimili vita vilivyoanzishwa na Israel na Marekani kwa zaidi ya siku 30.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Israel yaunga mkono rasmi usitishaji mapigano lakini 'haujumuishi Lebanon'

    Israel imetoa taarifa rasmi kuhusu kusitisha mapigano na Iran.

    Hii hapa kamili:

    Chapisho kamili:

    Israel inaunga mkono uamuzi wa Rais Trump wa kusimamisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa wiki mbili ikiwa Iran itafungua mara moja Mlango Bahari na kusimamisha mashambulizi yote dhidi ya Marekani, Israel na katika nchi za eneo hilo.

    Israeli pia inaunga mkono juhudi za Marekani kuhakikisha kwamba Iran sio tena tishio la nyuklia, kombora na ugaidi kwa Marekani, Israeli, majirani wa Kiarabu wa Iran na ulimwengu.

    Marekani imeiambia Israeli kwamba imejitolea kufikia malengo haya, ambayo pia ni ya Marekani, Israeli na washirika wa kikanda wa Israeli, katika mazungumzo yajayo.

    Usitishaji mapigano wa wiki mbili haujumuishi Lebanon.

    • Katika muktadha: Hapo awali, Waziri Mkuu wa Pakistani Shehbaz Sharif alisema kusitisha mapigano kulihusisha Lebanon.

    Soma zaidi:

  14. Israel haijatoa taarifa yoyote mpaka sasa kuhusu usitishaji wa mapigano

    Hadi sasa, Israel haijatoa taarifa rasmi kuhusu tangazo la kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran. Haijulikani ni kwa kiwango gani Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alihusika katika maamuzi ya Rais Donald Trump.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye amekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran, amesema makubaliano ya usitishaji wa mapigano yanajumuisha pia nchi ya Lebanon, ambapo Israel ina vikosi vya ardhini.

    Viongozi wa Israel wamekuwa wakisema hawataondoka Lebanon hadi tishio kutoka Hezbollah liondoke. Hata hivyo, hakuna ishara kwamba Israel imekubali kusitisha operesheni zake Lebanon au sehemu nyingine.

    Kama vita vitamalizika kwa msingi wa “mapendekezo 10 kutoka Iran” yaliyotajwa na Trump, itachukuliwa kuwa ni mafanikio ya kimkakati kwa Tehran. Hata hivyo, wanasiasa wa mrengo wa kulia wanaomuunga mkono Netanyahu wanaweza kupinga makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano, hasa kama yanahusisha Lebanon, na hivyo kumweka Netanyahu njia panda kisiasa nchi hiyo ikiingia kwenye uchaguzi Mkuu mwaka huu.

  15. Bei ya mafuta duniani yashuka baada ya tangazo la Trump la usitishaji wa mapigano

    Bei ya mafuta duniani imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki mbili.

    Mapema Jumanne, pipa moja la mafuta uliouzwa kwenye masoko ya kimataifa ulikuwa na thamani ya dola 103.42, huku mafuta ya Marekani yakiwa karibu na dola 103.25 kwa pipa. Hata hivyo, bei bado iko juu kuliko kipindi cha kabla ya mzozo kuanza Februari 28.

    Mtaalamu wa uchumi wa nishati kutoka Japan, Ichiro Kutani, alisema kushuka kwa ghafla kwa bei kunahusiana moja kwa moja na tangazo la Trump. Hata hivyo, bei haiwezi kurudi katika kiwango chake cha awali cha takribani dola 70 kwa pipa kwa sababu ya uharibifu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati.

    Wakati huo huo, masoko ya hisa barani Asia yamepanda: Nikkei 225 ya Japan imeongezeka kwa takribani 4% na ASX 200 ya Australia kwa karibu 3%.

  16. Pakistan yasifu ‘hekima’ ya Marekani na Iran baada ya kusitishwa mapigano mara moja

    Pakistan, ambayo ni mpatanishi katika mzozo wa Marekani na Iran, imesifu hatua ya nchi hizo mbili kukubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili.

    Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema pande zote zimeonyesha “hekima na uelewa mkubwa” kwa kukubali hatua hiyo, akiongeza kuwa zimeendelea kushiriki kwa njia chanya katika juhudi za kuleta amani na utulivu.

    Amesema usitishaji wa mapigano umeanza kutekelezwa mara moja, huku akizialika pande zote mbili jijini Islamabad Ijumaa kwa mazungumzo zaidi yanayolenga kufikia makubaliano ya kudumu.

    Kauli hiyo a Pakistan ilitolewa dakika chache kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kufikia makubaliano.

  17. Marekani na Iran zakubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema amekubali kusitisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa muda wa wiki mbili, kufuatia pendekezo la wapatanishi katika mgogoro huo.

    Trump alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya mazungumzo na viongozi wa Pakistan, akiwemo Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, ambao waliomba muda zaidi kwa juhudi za kidiplomasia.

    Katika ujumbe wake, Trump alisema hatua hiyo inahusishwa na kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz kwa usalama, njia muhimu ya biashara ya mafuta duniani.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi amesema Iran iko tayari kusitisha mapigano iwapo mashambulizi dhidi ya nchi hiyo yatakomeshwa, ikiashiria makubaliano ya masharti kati ya pande hizo mbili.

    Wakati huo huo, Pakistan imesema usitishaji wa mapigano umeanza kutekelezwa mara moja, hatua inayochukuliwa kama nafasi kwa pande zote kupunguza mvutano.

    Trump pia amesema Marekani imepokea mapendekezo ya masuala 10 kutoka Iran, akiyataja kuwa ni msingi unaoweza kufanyiwa kazi kupitia mazungumzo, huku akieleza kuwa tofauti nyingi zilizokuwepo tayari zimepunguzwa.

    Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vilianza Februari 28 na vimeathiri masoko ya kimataifa, hasa bei ya mafuta.

    Unaweza kusoma;

  18. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 08/04/2026.