Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wapenzi wa LGBT: 'Wazazi wangu walikuwa tayari kuniua'
Manoj mwenye umri wa miaka 17 – alizaliwa mwanamke – nusura auwawe siku alipoiambia familia yake kwamba alijihisi ni mwanaume na anavutiwa na wanawake. Anasema wazazi wake walikataa kumkubali, walimfunga mikono na miguu, wakampiga vibaya na kumfungia kwenye kona ya nyumba. Baba yake alitishia kumuua.
"Mateso yalikuwa makali sana," anasema. ‘’Wazazi wangu walikuwa tayari kuniua kulinda heshima yao."
Kwa mwanamke wa kijijini kutaka haki ya kujitambulisha kama huntha wa kiume, kunaweza kumletea matatizo.
Manoj anasema alitolewa shule katika mojawapo ya majimbo maskini kaskazini mwa India, la Bihar - na kuolewa kwa lazima na mwanamume mara mbili ya umri wake.
"Nilifikiria hata kujiua, lakini mpenzi wangu alisimama nami. Kwamba niko hai, na tuko pamoja, na hakukata tamaa nami," anasema.
Sasa ana miaka 22, anaishi maisha ya kujificha kwa mwaka mmoja sasa. Manoj na mpenzi wake, Rashmi, wanasubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama ya Juu, kuhusu ombi lao la haki ya kisheria ya kuoana.
India iliharamisha mapenzi ya jinsia moja mwaka 2018, na ndoa za watu wa jinsia moja bado hazijatambuliwa. Mwaka huu Mahakama ya Juu ilisikiliza maombi 21 ya kuomba kuhalalishwa na uamuzi unatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Ombi la Manoj na Rashmi, liliwasilishwa kwa pamoja na ombi la wanandoa wawili na wanaharakati wanne wa LGBTQ+, linadai ndoa ni njia ya kuondokana na ukatili wa kimwili na kiakili ambao wao wanafanyiwa na familia zao.
"Kutambuliwa kisheria uhusiano wetu ndiyo njia pekee ya kuondokana na maisha haya ya hofu," Manoj anasema.
India ina watu waliobadili jinsia nusu milioni, kwa mujibu wa sensa ya mwisho ya mwaka 2011, idadi ambayo wanaharakati wanaamini ni ndogo sana.
2014, Mahakama ya Juu iliamua kwamba huntha watambulike kama jinsia ya tatu. Miaka mitano baadaye, India ilipitisha sheria inayokataza ubaguzi katika elimu, ajira, huduma za afya na kufanya uhalifu dhidi yao, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kingono, kihisia na kiuchumi.
Vurugu za Familia
"Unyanyasaji wa ndani ya familia huwa unafichwa, iwe dhidi ya mke, watoto, au watu huntha, lakini upo,’' anasema mwanasheria – mfimenia anayeishi Mumbai, Veena Gowda.
Bi Gowda alikuwa sehemu ya jopo lililojumuisha jaji mstaafu, mawakili, wanataaluma, wanaharakati na wafanyakazi wa kijamii lililosikiliza ushuhuda wa unyanyasaji wa kifamilia uliowakumba watu 31 kutoka jamii ya LGBTQ+.
Miezi michache baada ya ndoa yake ya kulazimishwa, Manoj alijaribu kuungana tena na Rashmi, lakini alifuatiliwa na mume wake, ambaye aliwatishia kuwanyanyasa kingono wote wawili.
Walitorokea kituo cha karibu cha reli na kupanda treni iliyokuwa ikiondoka lakini anasema walipatikana na kurudishwa nyumbani kwa vipigo vipya. Manoj alifungiwa tena na simu yake ya mkononi kuchukuliwa.
"Alikuwa akilazimishwa kutia saini 'barua ya kujiua' ambayo ilinilaumu mimi kwa kifo chake," Rashmi anasimulia.
Baada ya Rashmi kuwasiliana na kikundi cha wanawake wa LGBT na kitengo cha polisi wanawake, ndipo waliweza kupata ulinzi na kutoroka familia ya Manoj. Walihamia katika makazi ya serikali ya watu huntha lakini ilibidi waondoke kwani Rashmi hakuwa katika kundi la waliobadili jinsia. Manoj pia aliweza kupata talaka.
Maisha mapya
Koyel Ghosh, msimamizi mkuu wa Sappho for Equality, jumuiya ya kwanza ya haki za wapenzi ya jinsia moja na huntha mashariki mwa India, iliyoanza miongo miwili iliyopita.
Wanakumbuka siku ambayo walipokea simu mwaka 2020 - ya wenza wawili ya kuomba msaada - ambao walikuwa wamekimbilia mji mmoja mashariki mwa India. Katika safari hiyo walilazimika kulala njiani kwa masiku saba.
"Tuliwakodishia sehemu na kukaa kwa miezi mitatu na kutafuta kazi kwani ndiyo njia pekee ya kujenga maisha mapya," Koyel anasema.
Kando na unyanyapaa wa kijamii, unyanyasaji wa kifamilia, kuvurugwa kwa elimu zao na ndoa za kulazimishwa, watu wengi huntha wanatatizika pia kupata ajira za uhakika.
Kulingana na uchunguzi wa huntha 900 huko Delhi na Uttar Pradesh, uliofanywa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu mnamo 2017; 96% walinyimwa kazi au kulazimishwa kuwa omba omba na kuingizwa katika biashara ya ngono.
Saphho ameanzisha makazi kusaidia wanandoa waliotoroka kujenga upya maisha yao. Wanandoa 35 wamehifadhiwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Ni kazi ngumu. Koyel hupokea simu tatu hadi tano kila siku na mara kwa mara huwasiliana na mawakili ili kupata msaada.
"Nimepokea vitisho vya kuuawa, kuzongwa na makundi ya watu vijijini, upinzani katika vituo vya polisi kwa sababu pia niko wazi kuhusu utambulisho wangu na hawawezi kukubaliana nayo," Koyel anasema.
Asif, mwanamme huntha na mpenzi wake, Samina, walipowasiliana na Koyel, walikuwa kwenye kituo cha polisi katika kijiji kimoja mashariki mwa India. Samina anadai askari walimwita towashi na kusema alipaswa kufa badala ya kuweka hadharani uhusiano wake.
Wao ni marafiki wa utotoni waliogeuka kuwa wapenzi. Wamekimbia familia zao mara mbili kabla lakini walirudishwa. Hii ilikuwa nafasi yao ya mwisho kutoroka na walihitaji kupata msaada.
"Alipowasili Koyel ndipo polisi walipoacha maneno yao machafu. Afisa mkuu aliwakosoa askari wake kwa chuki zao na kutojua sheria kama watumishi wa umma," Samina anasema.
Sasa wanaishi kwa usalama katika jiji kubwa, wanandoa hao wamefungua kesi pamoja na Manoj na Rashmi katika Mahakama Kuu.
"Tuna furaha sasa. Lakini tunahitaji cheti cha ndoa, ili kuzuia unyanyasaji," Asif anasema.
"Ikiwa Mahakama ya Juu haitatusaidia, tunaweza kufa. Hatutakubalika kama tulivyo, tutabaki kukimbia, daima tunaogopa kutengwa," anasema.
Majina yao yamebadilishwa ili kulinda utambulisho wao.