Madaktari wanaohudumu vitani: 'Tulipiga picha hii, tukihofia kuwa itakuwa ya mwisho'

Doctors in el-Fasher's Saudi Hospital performing a caesarean using light from mobile phones

Chanzo cha picha, Mudathir Ibrahim Suleiman

    • Author, Gladys Kigo
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Dkt Mustafa Ali Abdulrahman Ibo na wenzake kwa ujasiri walifanya upasuaji huku mashambulizi yakiongezeka katika hospitali ya mwisho iliyobaki huko el-Fasher, mji ambao umekuwa ukizingirwa na wapiganaji kwa miezi tisa iliyopita katika mkoa wa Darfur magharibi mwa Sudan.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita hospitali hiyo imerekodi vifo 28 na zaidi ya majeruhi 50 miongoni mwa wafanyakazi wake na wagonjwa kutokana na mashambulizi makali. Hii ni idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyorekodiwa katika kipindi cha mwezi mmoja tangu kuanza kwa harakati za mapigano katika eneo linaloizingira hospitali hiyo.

"Mashambulizi ya hivi karibuni yanayolenga hospitali ya Saudia yameongezeka kwa kiasi kikubwa, yamekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku," Dkt Ibo, ambaye ni mzaliwa wa Darfur ambaye ameishi katika mji wa el-Fasher tangu mwaka 2011, aliiambia BBC.

Alisema siku ya kutisha zaidi ilikuwa wakati timu ya madaktari walikuwa wakifanya upasuaji wa dharura wakati makombora yalipoanza tukio ambalo alilitaja kuwa ni uzoefu wa karibu wa kifo aliowahi kuushuhudia maishani mwake.

"Kombora la kwanza liligonga ukuta wa hospitali ... [kisha] lingine liligonga chumba cha upasuaji cha uzazi, vifusi vya jengo viliharibu jenereta ya umeme, umeme ukakatika na kutuingiza katika giza kamili," alisema.

Timu ya upasuaji haikuwa na chaguo ila kutumia tochi kwenye simu zao kumaliza operesheni ya saa mbili.

Sehemu ya jengo ilikuwa imeanguka na chumba kilikuwa kimejaa vumbi vipande vya makombora vilivyotawanyika kila mahali

Dkt Khatab Mohammed, ambaye alikuwa akiongoza upasuaji huo, alielezea hatari hizo.

"Hali ilikuwa mbaya, mazingira hayakuwa mazuri tena," daktari huyo mwenye umri wa miaka 29 aliiambia BBC.

"Baada ya kuhakikisha usalama wetu na usalama wa mgonjwa, tulimsafisha na kubadilisha nguo zetu za upasuaji kwa kuwa nguo zetu zilikuwa zimejaa vumbi na tuliendelea na upasuaji," alisema, akiongeza kuwa mgonjwa angeweza kufa kutokana na matatizo.

Baada ya kufanikiwa kujifungua mtoto, madaktari walimhamisha mama na mtoto mchanga hadi chumba kingine ili kupata nafuu na kisha wakakusanyika kupiga picha ya pamoja.

Ilikuwa ni ushahidi wa kuishi kwao, lakini Dkt Mohammed aliongeza: "Nilidhani inaweza kuwa picha yetu ya mwisho, nikiamini kwamba kombora lingine lingegonga sehemu moja na sote tutakufa."

Waliendelea kufanya operesheni mbili zaidi za kuokoa maisha siku hiyo.

Unaweza pia kusoma:
A group of medics at Saudi Hospital in el-Fasher in scrubs smile as they stand for a group photo after successfully performing two-hour emergency caesarean under bombardment. Dust from the shell damage can be seen on the floor

Chanzo cha picha, Mudathir Ibrahim Suleiman

Maelezo ya picha, Baada ya kufanikiwa kufanya upasuaji wa dharura wa uzazi wa saa mbili chini ya mabomu, madaktari waliomba kupigwa picha ya kumbukumbu ya tukio
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Madaktari hawa wengi wao wakiwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha el-Fasher - wamebaki huko tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilipoanza Aprili 2023.

Mzozo huo umelikumba jeshi dhidi ya vikosi vya kijeshi vya Rapid Support Forces (RSF) na umesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni 12 kuyakimbia makazi yao.

Mahasimu hao wawili walikuwa washirika, wakiingia madarakani kwa pamoja katika mapinduzi, lakini wakashindwa kutokana na mpango wa kimataifa wa kuelekea utawala wa kiraia.

Mwaka mmoja baada ya vita hivyo, el-Fasher ilianza kuzingirwa. Ni mji pekee ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi katika jimbo la Darfur, ambako RSF imeshutumiwa kwa kufanya mauaji ya maangamizi ya kikabila dhidi ya jamii zisizo za Kiarabu.

RSF ilianza kuishambulia el-Fasher kutoka pande tatu na kukata njia za usambazaji huduma muhimu za kijamii.

Katika ripoti iliyotolewa mwezi uliopita, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema mapigano hayo yamesababisha vifo vya raia 780 na wengine zaidi ya 1,140 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa majeruhi wa moto.

Mapigano hayo yamelazimisha hospitali nyingine zote katika mji wa el-Fasher kufungwa.

Hospitali ya Kusini, ambayo ilisaidiwa na shirika la misaada ya matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF), ilikuwa kituo kikuu cha afya katika mji huo kinachoshughulikia majeruhi wa vita.

Ilikuwa karibu na mstari wa mbele wa mapigano na ilivamiwa mwezi Juni na wapiganaji wa RSF, ambao pia walipora dawa na vifaa na kuwashambulia wafanyakazi.

Hospitali ya Saudia, ambayo inaendeshwa na Wizara ya Afya na kufadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, Umoja wa Mataifa na MSF, imebobea katika masuala ya uzazi na magonjwa ya uzazi ambayo sasa inatoa huduma zote za matibabu ni sehemu pekee katika jimbo la Darfur Kaskazini yenye uwezo wa upasuaji.

g

Chanzo cha picha, Mudathir Ibrahim Suleiman

Maelezo ya picha, Wafanyikazi katika hospitali hiyo wanafanya kisichowezekana kuokoa maisha" -Mudathir Ibrahim Suleiman, Mkurugenzi wa tiba katika hospitali ya Saudia

Huku kukiwa na uhaba wa vifaa vya matibabu na wafanyakazi, hospitali ya Saudia inakabiliwa na "hali ya kukatisha tamaa ambayo inakiuka sheria zote za kibinadamu na kimataifa na maadili", mkurugenzi wake wa matibabu, Mudathir Ibrahim Suleiman, mwenye umri wa miaka 28, aliiambia BBC.

Alikumbuka jinsi hali ilivyokuwa ya kutisha wakati wa milipuko ya hivi karibuni: "Wanawake wajawazito, watoto na wafanyakazi walikuwa katika mshtuko na uoga mkubwa baadhi ya watu walijeruhiwa walipokuwa wakitolewa nje ya vifusi.

"Hali zote za sasa zinatusukuma kufikiria kusitisha kazi zetu, lakini wanawake na watoto hawana sehemu nyingine ya kuokoa maisha yao isipokuwa hospitali hii," alisema.

"Wafanyakazi wa hospitali wanafanya kazi ngumu kuokoa maisha."

Mambo yote ya kawaida ya maisha yametoweka kabisa el-Fasher, hasa katika sehemu za kaskazini na mashariki. Chuo kikuu, kwa mfano, kinafanya kazi kupitia mafunzo ya mtandaoni, na vituo vya mitihani vimeanzishwa katika miji salama kama mji wa Kassala mashariki mwa Sudan.

Pamoja na njaa na ukosefu wa usalama, mji huo pia umekosa watu. Karibu nusu ya idadi ya watu wametafuta hifadhi katika kambi ya Zamzam, ambako inakadiriwa kuwa watu 500,000 sasa wanaishi katika hali ya njaa.

Hospitali ya Saudia pia inahudumia kambi hiyo, huku MSF ikiendesha magari ya kubebea wagonjwa ili kuleta wagonjwa wa dharura.

Lakini pia hivi karibuni wameanza kuishambuliwa, ikiwa ni pamoja na tukio la mapema mwezi huu wakati mtu mwenye silaha alipopiga risasi kwenye "gari la wagonjwa lililo na nembo ya MSF na bendera".

"Tumeshtushwa na shambulio hili baya dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu wanaofanya kazi ya kuokoa maisha ambapo inahitajika sana," Michel Olivier Lacharité wa MSF alisema katika taarifa.

A bomb shelter in the compound of el-Fasher's Saudi Hospital - it shows corrugated iron sheets covered with orange soil and sand bags.

Chanzo cha picha, Mudathir Ibrahim Suleiman

Maelezo ya picha, Bomu lililotegwa katika eneo la hospitali ya Saudi Arabia

Dkt Ibo alikiri kuwa ni wenzake wanaomfanya aendelelee kuhudunu katika hospitali hiyo, kuna madaktari 35 na wauguzi 60 katika hospitali ya Saudia - ambao walimfanya aende huko.

"Tunapoteza watu kila siku, na ofisi na vyumba vinaharibiwa, lakini kutokana na uamuzi wa wafanyakazi vijana, tunaendelea kuvumilia.

"Tunapata ujasiri wetu kutoka kwa watu wa el-Fasher sisi ni watoto wao na wahitimu wa Chuo Kikuu cha el-Fasher."

Mashirika ya misaada yanaonya kuwa jimbo la Darfur kuna moja ya dharura mbaya zaidi ya afya ya mama na mtoto, huku baadhi ya maeneo pia yanalengwa katika mashambulizi ya anga na jeshi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na kufuatwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Afya lazima iheshimiwe hata katika vita," afisa wa mawasiliano wa WHO nchini Sudan Loza Mesfin Tesfaye aliiambia BBC.

Dr Mohammed, ambaye asili yake ni kutoka jimbo la White Nile nchini Sudan lakini alikuja el-Fasher kusoma udaktari mwaka 2014, pia anatoa pongezi kwa timu yake, ambao wamepuuza fursa nyingi za kukimbia.

"Nafsi zetu zilikataa kuwaacha watu wa mji huu - hasa kutokana na hali mbaya tunayoshuhudia kila siku."

Madaktari wote, ambao waliwasiliana kupitia mazungumzo na maelezo ya sauti kwenye WhatsApp, walisikika wakisema:

"Tumedhamiria kuendelea kuokoa maisha ya watu, kutoka mahali popote kadri tunavyoweza, hata chini ya ardhi au chini ya kivuli cha mti, tunaomba vita vimalizike na amani ishinde," alisema Dk Ibo.

Maelezo ya ziada na mwandishi wa habari wa Sudan Mohammed Zakaria

Map
Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi