Israel yasema picha za CCTV zaonyesha mateka ndani ya hospitali ya Gaza ya Al-Shifa

Wanajeshi wa Israel wametoa video inayoonyesha walioshikwa mateka wakipelekwa katika hospitali kubwa zaidi ya Gaza baada ya mashambulizi mabaya ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba.

Msemaji wa jeshi alisema mmoja wao - mwanajeshi - aliuawa huko.

Cpl Noa Marciano, 19, aliuawa baada ya kupelekwa katika hospitali ya Al-Shifa akiwa na majeraha madogo, alisema.

Israel ilisema handaki limepatikana kwenye eneo na kudai kuwa ni kituo cha kusimamia operesheni za kijeshi cha Hamas. Hata hivyo, Hamas wanakanusha hilo.

BBC haijaweza kuthibitisha video hiyo ambayo iliwasilishwa kwenye kikao cha habari na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) siku ya Jumapili.

"Leo asubuhi tuliijulisha familia ya Noa kwamba kulingana na tulichogundua, alitekwa nyara hadi kwenye nyumba salama karibu na Shifa," Daniel Hagari, msemaji mkuu wa IDF aliwaambia waandishi wa habari.

"Wakati wa mashambulizi ya anga ya IDF katika eneo hilo, gaidi wa Hamas aliyekuwa akimshikilia Noa aliuawa na yeye akajeruhiwa, lakini si jeraha la kutishia maisha. Noa alipelekwa ndani ya hospitali ya Shifa, ambapo aliuawa na gaidi mwingine wa Hamas."

Hamas hapo awali ilidai kuwa Marciano aliuawa katika shambulio la anga la Israel, ambalo IDF ilisema lilitokea tarehe 9 Novemba.

Hagari kisha alicheza kanda za CCTV ambazo alisema zilikuwa ni za asubuhi ya tarehe 7 Oktoba - siku ambayo Hamas ilianzisha mashambulizi yake ya kushtukiza kusini mwa Israeli ambapo Waisraeli 1,200 waliuawa na zaidi ya 240 kuchukuliwa mateka.

Video hiyo ilionyesha mateka wawili wakiletwa katika hospitali kubwa na ya kisasa zaidi ya Gaza.

Wanaume wenye silaha wanaweza kuonekana kwenye video ya CCTV ambayo imeandikwa tarehe 7 Oktoba. Mmoja wa mateka anaonekana kusitasita - mwingine anaonyeshwa akiwa kwenye machela.

IDF imekuwa chini ya shinikizo kuthibitisha madai yake kwamba Hamas iliendesha kituo cha kusimamia operesheni za kijeshi chenye shughuli nyingi chini ya eneo kubwa la matibabu kaskazini mwa eneo hilo.

Ikijibu video hiyo iliyotolewa na Israel, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza ilisema haikuweza kuthibitisha ukweli wa picha hizo.

Wizara hiyo pia ilisema ni Israel iliyochukua jukumu kamili la kuzorotesha na kusambaratisha kabisa huduma za afya huko Gaza.

Awali, IDF ilitoa video ambayo ilisema ilionyesha handaki la mita 10 (futi 33) chini ya ardhi ambalo lina urefu wa 55m hadi kwenye mlango uliofungwa na kuimarishwa vizuri.

Ilisema hii sasa ni sehemu ya ushahidi "unaothibitisha wazi" majengo mengi katika hospitali hiyo "yametumiwa na Hamas kama maficho, miundombinu yenye shughuli za kigaidi".

Video ya hivi punde bado sio ushahidi ambao umeahidiwa wa aina ya operesheni kubwa na ngumu inayoonyeshwa kwenye kompyuta ambayo IDF ilitoa hapo awali ikionyesha kile inachoamini kuwa kituo chochote cha Hamas chini ya ardhi huko Al-Shifa kinaweza kuonekana kuwa hivyo.

Marekani imesema pia ina taarifa za kijasusi kwamba Hamas imetumia hospitali katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na Al-Shifa, kama vituo vya kusimamia operesheni za kijeshi na maghala ya silaha.

Israel imerejelea ujasusi wa Marekani kuthibitisha madai yao ya kuwepo kwa makao makuu katika jengo hilo lakini matumizi ya Wamarekani yanaashiria neno ambalo linaweza kupendekeza operesheni ndogo.

Israel inaamini kuwa inajenga uthibitisho wenye nguvu na iko makini kuwasilisha ushahidi wakati inapoupata.

Wakati washirika wa Israel wameunga mkono kampeni yake ya kijeshi ya kulipiza kisasi, ambayo inasema inalenga kuondoa Hamas, wameelezea kusikitishwa sana na madhara ya mashambulizi hayo kwa raia.

Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema idadi ya waliofariki Gaza tangu wakati huo imefikia 12,300. Zaidi ya watu 2,000 wanahofiwa kuzikwa chini ya vifusi.

Serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa familia za mateka. Wanataka afanye zaidi kuwakomboa wale wanaoshikiliwa na Hamas.

Siku ya Jumamosi, waandamanaji wakitoa wito kwa serikali ya Israel kuweka kipaumbele katika kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka walitembea kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem kabla ya kufanya maandamano nje ya makazi ya Bw Netanyahu.

Waziri mkuu, hata hivyo, anaonekana kutokatishwa tamaa katika misheni yake.

Anasema lengo lake la kwanza la vita ni kuwaangamiza Hamas; pili kurudisha mateka; na tatu kuondoa tishio kutoka Gaza.

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Seif Abdalla