Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mmoja wa wanafunzi wa Tanzania waliotekwa Israel amefariki
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili
Mmoja kati ya wanafunzi wawili wa Tanzania waliotekwa nyara na wapiganaji wa Hamas wakati wa uvamizi wao Israel amefariki dunia.
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa Clemence Felix Mtenga, mwanafunzi mwenye miaka 22, ndiye aliyefariki. Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo yan je ya Tanzania, hata hivyo haijaeleza amefariki lini, wapi na mazingira ya kifo chenyewe.
Mtenga alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao serikali ya Israeli hapo awali ilithibitisha kuwa wametekwa na Hamas baada ya shambulio la Oktoba 7.
Serikali ya Tanzania imeeleza katika taarifa hiyo kuwa inaendelea kuwasiliana na Israeli juu ya taarifa za Mtanzania mwengine Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu mashambulizi hayo.
Jumla ya watu 230 walichukuliwa mateka huku wengine 1,200 wakifariki dunia katika mashambuli hayo. Kwa mujibu wa Israel, mateka hao – ambao walipelekwa katika ukanda wa Gaza – wanatoka katika nchi 25, ikiwemo raia mmoja wa Afrika Kusini ambaye hadi sasa hajatambulika. Mpaka sasa ni mateka wanne tu ndio walioachiwa huru.
Marehemu Mtenga pamoja na Mollel walikuwa ni miongoni mwa vijana 260 wa Tanzania waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Israel.
Wote wawili waliwasili Isreali mwezi Septemba, wiki chache kabla ya mashambulizi ya Hamas, na programu yao ya masomo ilikuwa ya urefu wa miezi 11.
Baada ya taarifa za kutekwa kwake kuthibitishwa mwezi uliopita, dada wa Mtenga aliiambia BBC Swahili kuwa familia nzima ilikuwa na hofu, lakini hata hivyo walikuwa na matumaini kuwa ataokolewa.
“Hakuna mtu anayeweza kulala vizuri…tunaamini kwa huruma za Mungu kuwa atarudi kwetu salama. Tunamsubiri kwa hamu na tunamuombea usiku na mchana awe katika hali salama,” Neema Mtenga, dada wa marehemu Clemence aliiambia BBC hayo mwezi uliopita.
Kulingana na taarifa ya wizara, tayari serikali imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati.
Aidha imewahakikishia raia wake wanaoishi katika mataifa ya kigeni ikiwemo wanafunzi waliopo katika masomo nchini Israel kuwa kupitia ubalozi wake uliopo mjini Tel Aviv, nchini Israel, itaendelea kuwasiliana na mamlaka ya taifa hilo kuhakikisha kuwa Watanzania wote waliopo nchini humo wako salama.
Taarifa ya Serikali ya Israel ilisemaje?
Siku chache zilizopita serikali ya Israel ilithibitisha utambulisho wa watu wawili kutoka Tanzania walioaminika kushikiliwa na Hamas tangu shambulio la Oktoba 7 dhidi ya jamii za kusini mwa Israel, karibu na mpaka na Gaza.
Katika Taarifa hiyo Israel iliwataja wawili hao kuwa Joshua Loitu Mollel na Clemence Felix Mtenga waliokuwa nchini Israel kama sehemu ya programu ya mafunzo ya kilimo
Taarifa hiyo ya Israel ilisema: "Walitekwa nyara na magaidi wa Hamas na wanazuiliwa mateka huko Gaza, "Tafadhali ungana nasi kuwaombea warudi salama na mara moja."
Katika mitandao ya kijamii habari hii ilipokelewa na mshtuko mkubwa miongoni mwa Watanzania wengi nchini humo.
Kwa mfano aliyejiita @mankyr0 alitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuwarudisha nyumbani Watanzania wote waliopo katika eneo lenye vita