Jinsi mgogoro kati ya wakulima katika Ukingo wa Magharibi unavyogombanisha Israeli na Marekani

Chanzo cha picha, Stuart Phillips
Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya walowezi watatu zaidi wa Israel na - kwa mara ya kwanza - vituo viwili vya kilimo, kama sehemu ya hatua mpya za Washington na London kukomesha uhamishaji wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa kimabavu.
Fares Samamreh anaweza asibebe bunduki, lakini ana nguvu kubwa duniani inayomtetea. Bado anapoteza pambano.
Mfugaji wa kondoo wa Kipalestina kwenye miteremko yenye jua kali ya Milima ya Hebron Kusini katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, vita vyake na jirani yake, mlowezi wa Israel anayeitwa Yinon Levy, vimezivuta Marekani na Uingereza katika mzozo huo.
"Yinon Levy alikuja hapa miaka mitatu iliyopita na kuanza kunisumbua," Fares alisema, kichwa chake kikiwa kimefunikwa na kipande cha pamba nyeupe, macho yake yakiwa na makengeza ya kudumu dhidi ya jua.
"Kabla ya vita [huko Gaza] ilikuwa ni jambo la kawaida; walikuja na ndege zisizo na rubani. Lakini siku chache baada ya Oktoba 7, ikawa mbaya. Wote walikuwa na bunduki. Walianza kuja kwetu mchana na usiku. Nina watoto wadogo. - baadhi yao wana miaka minne na mitano."
Fares alisema Yinon alikuwa mmoja wa kundi la walowezi wa ndani wa Israeli ambao walikuja mara kwa mara kuwasumbua kondoo wake kwa mbwa na silaha zao, na hata, anasema, kushambulia familia yake.

Chanzo cha picha, Stuart Phillips
"Waliharibu matangi ya maji, walifunga barabara, wanawafyatulia risasi kondoo," alisema. "Aliambia mke wangu tusipoondoka hapa, tutauawa sote."
Alisema wakati mke wake alipomjibu, Yinon Levy alimpiga kwa kitako cha bunduki yake.
Muda mfupi baadaye, Fares na familia yake waliondoka katika kijiji chao cha Zanuta. Wanaharakati wanasema ni moja ya jamii nne karibu na shamba la walowezi ambazo zimetelekezwa na wakaazi wao.
Yinon amekana kuwafanyia fujo Wapalestina katika eneo hilo - na kusema kuwa hakuwa na bunduki hadi hivi majuzi.
Lakini yeye ndiye mlengwa wa vikwazo kutoka Marekani na Uingereza.
Barabara ya kwenda kwenye shamba la Yinon ni moja kwa moja kutoka kwa kitabu cha picha cha watoto; njia nyembamba ambayo inarudi na kurudi juu ya kilima mwinuko, miteremko na mabonde yanayoshuka hadi upeo wa macho kila upande.
Hapo juu, kuna jumba kubwa la kifahari karibu na banda kubwa, lililojaa kondoo wanaolia na muziki wa pop kutoka kwa redio.

Chanzo cha picha, Stuart Phillips
"Tunalinda ardhi hizi ili kuhakikisha zinasalia chini ya umiliki wa Wayahudi," Yinon alisema. "Wakati kuna uwepo wa Wayahudi, basi hakuna uwepo wa Waarabu. Tunaweka jicho kwenye ardhi, kuhakikisha kwamba hakuna ujenzi usioidhinishwa unaofanyika."
Nchi nyingi zinachukulia makazi hayo, ambayo yamejengwa katika ardhi iliyotekwa na Israel mwaka 1967 katika Vita vya Mashariki ya Kati, kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel haikubaliani nayo. Viwanja vya walowezi pia ni haramu chini ya sheria za Israel.
Uingereza ilisema kuwa Yinon na mwanamume mwingine "wametumia uchokozi wa kimwili, kutishia familia kwa mtutu wa bunduki, na kuharibu mali kama sehemu ya juhudi zilizolengwa na zilizopangwa kuziondoa jamii za Wapalestina".
Yinon alikanusha madai hayo, na kusema kuwa serikali ya Israel ilikuwa upande wake.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tulimtumia Yinon video inayoonekana kumuonyesha kwenye ardhi ya Palestina, akiwakaribia wanaharakati akiwa na mbwa anayefoka. Alisema ilikuwa ya kupotosha, na kwamba alikuwa akilinda kondoo wake.
Tulimtumia video nyingine inayomuonyesha akiingia katika kijiji kingine cha Palestina akiwa na bunduki Oktoba mwaka jana. Alikataa kutoa maoni.
Vikwazo hivyo vilikuja baada ya kuongezeka kwa ghasia katika Ukingo wa Magharibi, kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas na vita vya Israel huko Gaza.
Umoja wa Mataifa unasema ghasia za walowezi wa Israel ni pamoja na mashambulizi ya kimwili na vitisho vya kuuawa, na kwamba idadi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao mwaka jana iliongezeka maradufu hadi 1,539 - huku zaidi ya asilimia 80 yao wakiondoka baada ya Oktoba 7.
Uingereza imesema Israel inashindwa kuchukua hatua, na imeelezea "mazingira ya kutokuadhibiwa kabisa kwa walowezi wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi".
Yinon alisema kuwa amepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa wa Israel.
Mmoja wa wanasiasa ambao waliunga mkono Yinon hadharani baada ya vikwazo hivyo alikuwa Zvi Sukkot wa chama cha kidini cha Uzayuni - ambaye mwenyewe ni mlowezi.

Chanzo cha picha, stuart Phillips
Alisema kuwa ghasia za walowezi ni "jambo la kando" na kwamba wale kama Levy walikuwa wahasiriwa wa matukio.
"Tunapokuwa na mfumo wa mahakama unaofanya kazi nchini Israel, hatutaki washirika wetu kusema, 'tutafanya kazi hiyo kwa ajili yenu," alisema.
"Kama kungekuwa na ushahidi dhidi ya Yinon Levy, angekuwa katika jela ya Israel. Je, Uingereza ni nani aje na kusema, 'sisi ni werevu kuliko ujasusi wa Israel'?"
Kamanda wa polisi wa Israel anayehusika na uchunguzi wa malalamiko katika Ukingo wa Magharibi aliiambia kamati ya bunge ya Bw Sukkot wiki hii kwamba nusu ya malalamiko yaliyowasilishwa kuhusu ghasia za walowezi huko ni ya uwongo, na kwamba yalitoka kwa "mashirika ya mrengo wa kushoto wenye itikadi kali huko Tel Aviv".
Kutokana na hali hii, vikwazo kwa walowezi wachache havijabadilisha sera za Israel katika Ukingo wa Magharibi, lakini vina athari za kifedha.
Akaunti ya benki ya Yinon ya Israeli ilifungiwa mwezi uliopita.
Baadhi ya wale walio chini ya vikwazo vya Marekani na Uingereza kwa sasa wametumia ufadhili wa watu wengi kufadhili miradi ya eneo lao - ikiwa ni pamoja na moja ya sinagogi na kituo cha elimu katika kituo kingine cha mlimani kiitwacho Moshe's Farm.
Mmiliki wake, Moshe Sharvit, aliwekewa vikwazo pamoja na Yinon Levy mwezi uliopita.
Vikwazo hivi vinaweza kuwa vya kiishara kuliko ushawishi, lakini vinaashiria kutofurahishwa na Marekani - kwa viongozi wa Israel, na kwa sehemu za chama cha Rais Biden cha Democratic ambao wamesikitishwa na picha za vita huko Gaza, katika mwaka wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya eneo la Yesha (walowezi), Shlomo Ne'eman, aliita "jambo la kuchukiza" na kusema Ukingo wa Magharibi ulikuwa unatumiwa kama lawama tu.
"Nafikiri zaidi ya kitu chochote kile, kinachochochea mwitikio wa Uingereza Marekani ni hofu ya shambulio moja la walowezi ambalo 'litatoka nje ya udhibiti'," Yehuda Shaul, mwanzilishi wa Kituo cha Ofek, kundi linalofanya kampeni ya kukomesha kuendelea kwa makaazi ya Israel.
Imetafsiriwa na Jason nyakundi












