'Nilijifungua njiani na kuendelea kutembea ili kuepuka ghasia'

Na Mercy Juma

BBC News

.

Baada ya Watoto wake watatu kuuawa , mtangazaji aliyekuwa mjamzito alitoroka vita katika jimbo la Darfur kwa miguu and kujifungua mvulana katika eneo la mpakani kuelekea Chad.

''Nilijifungua barabarani. Hakukuwa na wakunga na mtu wa kunisaidia.. Kila mtu alikuwa akitoroka kuokoa nafsi yake''.

‘’Mtoto alitoka , nikamfunga kwenye nguo, Sikufikiria kitu chengine chochote. Niliendelea kutembea hadi Adre’’, Arafa Adoum alisema nilipokutana naye katika kambi ya wakimbizi ya makumi ya maelfu ya watu kandokando ya mji wa Chad.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema kwamba alikuwa ametembea katika jua kali kwa takriban kilomita 25 kutoka mji wa nyumbani kwao wa El Geneina akiwa na watotoi wake wanne wa kike , huku mumewe wake akitumia njia ndefu Zaidi kufika katika kambi hiyo.

‘’Nilipowasili katika mpaka nilijipata nimechoka hadi nilipojifungua’’ , Mrs Adoum alisema akiongexzea kwamba alimtaja mwanawe jina la mtume Muhamed.

Aliacha maiti ambazo hazijazikwa za wavulana wake wengine - wenye umri wa miaka mitatu, saba na tisa - baada ya kusema waliuawa na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) na wanamgambo washirika wa Kiarabu katikati ya vita vinavyoendelea nchini Sudan tangu Aprili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Darfur ndilo eneo lililoathirika zaidi, huku RSF na wanamgambo wakishutumiwa kwa kujaribu kuanzisha ukuu wa Waarabu katika kanda hiyo kwa "kuwaangamiza" Waafrika weusi - ikiwa ni pamoja na wale wa jamii ya Massalit ya bi Adoum.

Ndio maana vita vya muda mrefu vya ,El Geneina - kihistoria ngome ya mamlaka ya Waafrika weusi huko Darfur, na mji mkuu wa jadi wa ufalme wa Massalit - vimekuwa vibaya.

"Tulijaribu kujilinda, lakini walikuwa wakitumia silaha kubwa sana," alisema Sheikh Mohammed Yagoub, mhubiri wa Kiislamu mwenye ushawishi na kiongozi wa Massalit, ambaye pia amekuwa mkimbizi huko Adré.

"Katika eneo letu kwa siku moja, tulipoteza [watu] 82 ndani ya saa tatu," aliongeza.

RSF ilikanusha kuhusika na mapigano hayo, lakini ilisema kuwa Darfur ilikuwa ikishuhudia kuzuka tena kwa mzozo wa zamani kati ya makundi ya Waarabu na Massalit.

Akizungumza , Bi Adoum alisema wanawe watatu waliuawa katika chuo kikuu cha El Geneina - ambapo walikuwa wakikimbilia - baada ya kushambuliwa kwa makombora na RSF na Janjaweed, wanamgambo wa Kiarabu wanavyojulikana.

"Watoto hao watatu walipigwa na makombora na kupoteza maisha hapo hapo," Bi Adoum alisema.

Watu kadhaa wa familia yake kubwa pia waliuawa, alisema, ikiwa ni pamoja na baba mkwe wake, ambaye "alivunjwa miguu yake yote miwili", sikio lake moja lilikatwa, na kisha "wakafyatua risasi kadhaa, na kummaliza".

Bi Adoum na mumewe kisha walikimbia pamoja na binti zao wanne, lakini alichukua njia za mkato ili kuepuka kupita katika vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na RSF kwa kuwa wanajeshi hao walikuwa - kulingana na wakimbizi wengi - wakiwaua wanaume na wavulana wa Massalit, wakati mwingine kwa kuwamwagia petroli na kuwachoma moto.

Wanandoa hao walikutana tena katika kambi ya wakimbizi, ambapo mume wake alimzaa Mohamed kwa mara ya kwanza - mtoto ambaye wanamwona kuwa baraka baada ya kupoteza watoto watatu wa kiume.

.
Maelezo ya picha, Mgogoro wa kibinadamu uliosababishwa na mzozo huko Darfur umevuta hisia chache duniani

Mke wa sheikh, Rakhiya Adum Abdelkarim, aliniambia kwamba yeye pia alikuwa mjamzito, lakini alipoteza mtoto wake siku moja baada ya Adré kuwasili kwa mguu - matembezi ambayo yalimuacha akiwa na njaa, mchovu na dhaifu.

"Nilianza kutokwa na damu. Kisha nikaanza kuumwa na kichwa, na muda wote huo damu ilikuwa ikitoka. Kisha, alfajiri, mtoto aliwasili," alisema.

Hospitali ya moja sehemu za shambani imeanzishwa huko Adré na shirika la hisani, lakini bi Abdelkarim hakufanikiwa kufika hapo kwa matibabu.

Hospitali imejaa wagonjwa - wengi wao wakiwa wanawake, watoto wachanga, na watoto, ambao baadhi yao wana majeraha ya risasi.

Mmoja wa wagonjwa hao, Naima Ali, alisema yeye na mtoto wake wa miezi tisa walipigwa risasi na mpiga risasi wa kuvizia wa RSF wakati wakitoroka kijijini kwao.

Mvulana huyo alikuwa amefungwa mgongoni mwake, wakati risasi ilipompata mguuni, na "mimi upande wangu wa mwili, wakiikosa figo yangu.

"Sote tulikuwa tukivuja damu na hakuna mtu aliyekuwa akitusaidia," alisema, akionyesha kwamba yeye pia aliendelea kukimbia kwa miguu hadi alipofika kambini.

.
Maelezo ya picha, Naima Ali na mwanawe sasa wako salama katika hospitali ya muda huko Chad

Ili kukomesha ukatili huo, mataifa manne ya Afrika Mashariki yametaka kikosi cha kulinda amani cha kanda kutumwa nchini Sudan, huku Rais wa Kenya William Ruto akieleza wasiwasi wake kwamba nchi hiyo "inaangamizwa", na tayari kuna dalili za mauaji ya kimbari huko Darfur.

Vikosi vyaa pamoja vyaa kulinda amani vyaa Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) viliondoka Darfur mwaka 2021, takriban miaka 18 baada ya vita, vilivyosababisha vifo vya takriban watu 300,000, kuzuka kwa mara ya kwanza katika eneo hilo.

Mzozo huo ulisababisha ghadhabu duniani, ambapo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilimfungulia mashtaka mtawala wa wakati huo wa Sudan Omar al-Bashir kwa tuhuma za mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, jambo ambalo alilikanusha.

Wakati wanajeshi hao wa kulinda amani walipojiondoa, Umoja wa Mataifa ulisema uamuzi huo unalenga "kuipa serikali ya Sudan mamlaka kuchukua jukumu la kudumisha amani katika eneo hilo".

Lakini tangu kujiondoa kwao, Sudan imekumbwa na mapinduzi, na kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katikati ya mwezi wa Aprili baada ya majenerali wake wawili wenye nguvu - mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti - kutofautiana.

Ugomvi wao umezusha mzozo huko Darfur, na kuwalazimu zaidi ya watu 160,000 kutoka jamii ya Massalit kukimbilia Chad. Haijabainika ni watu wangapi wameuawa katika eneo hilo, huku makadirio ya chini kabisa ya vifo vya El Geneina ikifikia 5,000.

Kulingana na Chama cha Wafamasia Wataalamu wa Sudan, idadi hiyo ni kubwa zaidi. Inasema miili 11,000 imezikwa katika makaburi ya halaiki mjini humo, huku baadhi ya wakimbizi wakiambia BBC kuwa wameona maiti zikitupwa mtoni.

RSF pia ilivamia jiji la Zalingei, nyumbani kwa jumuiya ya Fur, na kuzunguka miji miwili mikubwa katika eneo hilo, Fasher na Nyala.

Watu wengi wa Darfuri wanahofia hii ni hitimisho la mpango wa muda mrefu wa kubadilisha eneo hilo lenye mchanganyiko wa kikabila kuwa eneo linalotawaliwa na Waarabu.

Wanasema kwamba El Geneina - pamoja na miji na vijiji vingine vingi - vimeondolewa wakazi wake wengi, na majengo na miundombinu - ikiwa ni pamoja na hospitali na vituo vya maji - kuharibiwa.

Unaweza pia kusoma
.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimefunzwa vyema na vinamiliki silaha za kutosha

"Kinachotokea ni kibaya zaidi kuliko kile kilichotokea mwaka 2003," sheikh alisema, akionyesha kwamba watu maarufu zaidi wa Massalit - ikiwa ni pamoja na madaktari na wanasheria - wameuawa.

Bi Adoum - mtangazaji katika Radio El Geneina ambayo sasa haipo - alibahatika kunusurika, wakati RSF ilipovamia ofisi ya shirika hilo katika siku za mwanzo za vita.

"Waliingia ndani na kuvunja vifaa vyote na kupora walichoweza," alisema.

Sasa Bibi Adoum anaishi katika kibanda, kilichojengwa kwa vijiti na vipande vya nguo, bila kujua kama ataweza kurudi nyumbani.

"Tulikuja kama wakimbizi. Wengi walikufa njiani. Lakini ilitubidi kuendelea kusonga mbele," alisema, huku akimshika mtoto wake wa wiki tatu mikononi mwake.

Mkimbizi mwingine alikataa kurudi tena, akisema: "Nitarudi kwa nani? Nimekuwa hapa kwa wiki na harufu ya maiti zinazooza kwenye mitaa ya El Geneina imekataa kuondoka puani mwangu."

.