Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Salif Keïta: Nguli wa muziki Afrika anayeunga mkono mapinduzi ya Mali
Mshtuko. Kuchanganyikiwa. Kutoamini. Hizi ni baadhi ya hisia miongoni mashabiki wa muziki wakati Salif Keïta - anayejulikana kama Sauti ya Dhahabu ya Afrika - alipoteuliwa kuwa mshauri maalumu wa kiongozi wa mapinduzi ya Mali, Kanali Assimi Goïta.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 73 anaweza kuwa amestaafu na kufichwa na wasanii nyota wa siku hizi wa Afrobeats, lakini alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kizazi kilichoweka muziki wa Kiafrika kwenye ramani ya kimataifa.
Baada ya miaka 50 ya mafanikio katika tasnia ya muziki, anaendelea kuwa na ushawishi, kupendwa na kujulikana sana. Keïta huchanganya muziki wa kitamaduni wa Mandé na jazz, blues na mitindo ya muziki wa Magharibi. Aliteuliwa mara kadhaa kwenye tuzo za Grammy.
Ana ualbino - na amefanya kampeni bila kuchoka dhidi ya ubaguzi. Mwaka 2005, mwanamuziki huyo alianzisha Wakfu wa Salif Keïta Global ili kuongeza ufahamu juu ya ualbino na kuzungumzia dhana potofu iliyopo katika baadhi ya nchi za Kiafrika kwamba ualbino ni dalili mbaya.
Watu wenye ualbino mara nyingi huepukwa na kuonewa - kama Keïta ilivyokuwa kwake utotoni - na katika baadhi ya nchi, kama Burundi na Tanzania, wanauawa au kukatwa sehemu za mwili na kutumika katika matambiko.
Ndoto ya Keïta akiwa mtoto ni kuwa mwalimu - lakini alinyimwa fursa hiyo na kuambiwa "atawatisha Watoto."
Keïta amechangisha fedha katika matamasha yake na kuchangia mapato ya mauzo ya rekodi zake kwa taasisi yake ili kusaidia matibabu ya watu wenye ualbino - ambao wako kwenye hatari zaidi ya saratani ya ngozi na macho kutoona.
Kwa nini Keïta amekubali uteuzi wa kuwa mshauri maalumu wa masuala ya kitamaduni - kwa mwanajeshi ambaye ameongoza mapinduzi mawili - ya kwanza Agosti 2020 na ya pili Mei 2021?
Keïta na Siasa za Mali
Miaka mitatu iliyopita, kulikuwa na uungwaji mkono mkubwa kwa utawala wa kijeshi wa Mali wakati ulipotwaa mamlaka baada ya maandamano makubwa dhidi ya Rais wa wakati huo Ibrahim Boubacar Keïta, ambaye hana uhusiano wowote na mwanamuziki huyo.
Watu walichoka na uongozi dhaifu, ufisadi, matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa usalama uliosababishwa na makundi ya Kiislamu.
Nyota huyo wa muziki alimkosoa sana mwendazake rais aliyepinduliwa Ibrahim Boubacar Keïta (IBK). Mwaka 2019, video ya Keïta, akizungumza kwa lugha ya Kibambara ilisambaa.
Alimtaka rais kusimama dhidi ya mkoloni wa zamani, Ufaransa, ambayo wakati huo ilikuwa na wanajeshi nchini Mali wakipambana na wapiganaji wa Kiislamu. Keïta alimtaja Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kama "mtoto" - na akaishutumu Ufaransa kwa kufadhili wanajihadi.
Pia, ameelezea mashaka yake kuhusu demokrasia ya Magharibi kufanya kazi katika nchi za Afrika.
"Demokrasia si jambo zuri kwa Afrika," aliliambia gazeti la Guardian la Uingereza mwaka 2019. "Ili kuwa na demokrasia, watu wanapaswa kuelewa demokrasia, na jinsi gani watu wanaweza kuelewa wakati asilimia 85 ya watu nchini hawajui kusoma na kuandika?"
Keïta alipendekeza kuwa wa-Afrika wanahitaji "dikteta mkarimu." Nchini Mali, 82% ya watu wanaliamini jeshi "kwa kiasi fulani" au "sana." Kwa hivyo Keïta anaonekana kukubaliana na hali ya umma kwa kuunga mkono utawala wa kijeshi.
Keïta alihudumu katika Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC) - lililoundwa Disemba 2020 na viongozi wa mapinduzi kama sehemu ya kile walichokiita mpito kwa utawala wa kiraia.
"Huu ni wakati muhimu kwa Mali," Keïta aliambia shirika la habari la Bloomberg wakati huo. "Ni muhimu sana turekebishe makosa ambayo yamefanywa huko nyuma."
Katika kile ambacho serikali ya kijeshi itaona ni mafanikio, Benki ya Dunia ilisema Julai - uchumi wa Mali umeonekana "kustahimili" licha ya mfumuko wa bei wa chakula, uzalishaji wa pamba kuathiriwa na uvamizi wa vimelea na vikwazo vilivyowekwa na Jumuiya ya Afrika Magharibi Ecowas – ili kulazimisha viongozi wa mapinduzi kuachia madaraka.
Lakini mafanikio ya kiusalama bado ni madogo. Kundi la ufuatiliaji la Acled lilieleza kuwa ghasia za mwaka 2022 zilifikia kiwango cha juu zaidi ambacho hakijawahi kurekodiwa.
Wanajeshi wanatawala bunge la mpito. Pia, lipo kundi la mamluki la Urusi Wagner, ambapo serikali ya kijeshi inasema kundi hilo linasimamia usalama wa Mali na litakuwa na ufanisi zaidi kuliko wanajeshi wa Ufaransa ambao wameondoka. Wakati huo huo vikosi vya Umoja wa Mataifa navyo vinapunguza shughuli zake.
Kupandishwa Cheo
Tarehe 31 Julai, Keïta alijiuzulu katika barala la mpito NTC - alitaja "sababu binafsi" huku akisisitiza kwamba atabaki kuwa "mshirika asiye na shaka" wa wanajeshi.
Uamuzi wake ulizusha uvumi nchini Mali kwamba alikuwa akijaribu kujitenga na utawala wa kijeshi, hasa kwa vile ilikuwa ndiyo kwanza umepitisha katiba mpya ambayo inaupa nguvu utawala wa kijeshi.
Lakini tarehe 11 Agosti Keïta alikubali kupandishwa cheo - wadhifa wa mshauri maalumu wa masuala ya kitamaduni.
Kanali Goïta alimteua katika wadhifa huo ili kujaribu kukuza umaarufu wake kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika ifikapo Februari mwaka ujao. Kuna uvumi mkubwa kwamba kiongozi huyo mchanga atajigeuza kuwa mwanasiasa wa kiraia, na kugombea urais.
Wakati Sauti ya Dhahabu ya Afrika inapochukua jukumu la kuwa mshauri maalumu wa Kanali Goïta, swali ni: Je, Keita atakuwa mwimbaji wa kusifu au atatoa ushauri wa busara na muhimu ambao tumezoea mwanaharakati huyo akitoa dhidi ya ubaguzi?