Binti wa tajiri wa almasi India mwenye miaka 8 awa mtawa
By Geeta Pandey, BBC News, Delhi

Chanzo cha picha, RUPESH SONAWANE
Devanshi Sanghvi mwenye umri wa miaka minane angeweza kukua na kuendesha biashara ya mamilioni ya dola za almasi. Lakini binti wa mfanyabiashara tajiri wa almasi wa India sasa anaishi maisha yasiyo ya starehe - akiwa amevalia nguo nyeupe, bila viatu na anakwenda nyumba hadi nyumba kutafuta msaada.
Yote hiyo ni kwa sababu wiki iliyopita, Devanshi, binti mkubwa kati ya mabinti wawili wa Dhanesh na Ami Sanghvi, aliachana na maisha ya ulimwengu na kuwa mtawa.
Sanghvis ni miongoni mwa Wajaini milioni 4.5 wanaofuata Ujaini - mojawapo ya dini kongwe zaidi duniani, ambayo ilianzia India zaidi ya miaka 2,500 iliyopita.
Wasomi wa kidini wanasema idadi ya Wajaini wanaokataa maisha ya vitu ama mali za ulimwengu imekuwa ikiongezeka kwa kasi kwa miaka mingi, ingawa visa vinavyohusisha watoto wadogo kama Devanshi si vya kawaida.
Sherehe ya Jumatano iliyopita katika mji wa Surat katika jimbo la magharibi la Gujarat, ambapo Devanshi alichukua "diksha" - kwa maana ya viapo vya kujitoa - mbele ya watawa wakuu wa Jain, nailihudhuriwa na makumi ya maelfu ya watu.
Akiwa ameongozana na wazazi wake, alifika ukumbini katika eneo la Vesu jijini humo, akiwa amejipamba kwa vito vya thamani na akiwa amevalia hariri nzuri. Alivaa taji la almasi kichwa kwake. Baada ya sherehe, alisimama pamoja na watawa wengine, wakiwa wamevalia sare nyeupe ambayo pia ilifunika kichwa chake kilichonyolewa.
Katika picha, anaonekana akiwa ameshika ufagio ambao sasa atautumia kuwaondoa wadudu anapopita njiani ili kuepuka kuwakanyaga kimakosa.

Chanzo cha picha, RUPESH SONAWANE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu wakati huo, Devanshi amekuwa akiishi katika Upashraya - nyumba ya watawa ambapo watawa wa Jain wanaishi. "Hawezi tena kukaa nyumbani, wazazi wake si wazazi wake tena, yeye ni Sadhvi [mtawa] sasa," anasema Kirti Shah, mfanyabiashara wa almasi anayeishi Surat ambaye ni rafiki wa familia na pia mwanasiasa wa chama cha Bharatiya Janata.
"Maisha ya mtawa wa Jain ni magumu sana. Sasa atalazimika kutembea kila mahali, hawezi kamwe kupanda usafiri wa aina yoyote, atalala kwenye shuka nyeupe sakafuni na hawezi kula baada ya jua kuzama," aliongeza.
Sanghvis anatoka dhehebu pekee la Jain ambalo linaruhusu watawa watoto - madhehebu mengine matatu yanakubali watu wazima tu.
Wazazi wa Devanshi wanajulikana kuwa "ni watu wa dini sana" na vyombo vya habari vya India vimewanukuu marafiki wa familia hiyo wakisema kwamba msichana huyo "alikuwa na mwelekeo wa maisha ya kiroho tangu alipokuwa mtoto mchanga".
"Devanshi hajawahi kutazama televisheni, sinema au kwenda kwenye maduka makubwa na mikahawa," gazeti la Times of India liliripoti. "Kuanzia umri mdogo, Devanshi amekuwa akisali mara tatu kwa siku na hata kufunga akiwa na umri wa miaka miwili," gazeti hilo liliongeza.
Siku moja kabla ya sherehe ya kuachwa kwake, familia ilikuwa imeandaa maandamano makubwa ya sherehe huko Surat. Maelfu walitazama tamasha hilo huku ngamia, farasi, mikokoteni ya ng’ombe, wapiga ngoma wacheza-dansi na waigizaji wakitoa burudani.
Devanshi na familia yake waliketi kwenye gari lililovutwa na tembo, huku umati wa watu ukiwamwagia maua ya waridi.

Chanzo cha picha, RUPESH SONAWANE
Maandamano pia yalipangwa katika mji wa Mumbai na mji wa Antwerp huko Ubelgiji, ambapo Sanghvis wana biashara zao. Ijapokuwa kuna uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya Jain kwa matukio hayo, lakini kujikana ama kujiondoa au kujitenga kwa Devanshi kumesababisha mjadala mkubwa, huku wengi wakiuliza kwa nini familia haikungoja awe mtu mzima kabla ya kufanya maamuzi muhimu kama hayo kwa niaba yake.
Bw Shah, ambaye alialikwa kwenye sherehe ya diksha lakini akakaa mbali kwa sababu wazo la mtoto kuukana ulimwengu linamkosesha raha, alisisitiza kuwa "hakuna dini inayopaswa kuruhusu watoto kuwa watawa".
"Yeye ni mtoto, anaelewa nini kuhusu haya yote?" Aliuliza. "Watoto hawawezi hata kuamua ni mkondo gani wa kusoma chuoni hadi wawe na umri wa miaka 16. Wanawezaje kufanya uamuzi kuhusu jambo ambalo litaathiri maisha yao yote?"
Kwa nini vijana hawa wanaikana dunia? Mtoto anayeukana ulimwengu anapofanywa kuwa mungu na jamii kusherehekea, yote yanaweza kuonekana kama sherehe kubwa kwake, lakini Prof Nilima Mehta, mshauri wa masuala ya ulinzi wa watoto mjini Mumbai, anasema "shida ya kunyimwa vitu muhimu atakayopitia mtoto itakuwa kubwa sana" . "Maisha kama mtawa wa Jain ni magumu sana," anasema.
Wanajamii wengine wengi pia wameelezea kutofurahishwa na mtoto kutengwa na familia yake katika umri mdogo. Na tangu habari zilipoibuka, wengi wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuikosoa familia hiyo, wakiwashutumu Sanghvis kwa kukiuka haki za mtoto wao.
Bw Shah anasema lazima serikali ijihusishe na kukomesha tabia hii ya watoto kuukana ulimwengu. Lakini kuna uwezekano mdogo sana kutokea - ambapo nilifika kwenye ofisi ya Priyank Kanungo, mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kulinda Haki za Mtoto (NCPCR), kuuliza ikiwa serikali ingefanya lolote kuhusu suala la Devanshi. Ofisi yake ilisema haitazungumzia suala hilo kwa sababu ni "suala nyeti".

Chanzo cha picha, RUPESH SONAWANE
Wanaharakati, hata hivyo, wanasema kuwa haki za Devanshi zimekiukwa. Kwa wale wanaosema kwamba mtoto anajinyima raha "kwa hiari yake mwenyewe", Prof Mehta anadokeza kuwa "ridhaa ya mtoto si ridhaa ya sheria".
"Kisheria miaka 18 ni umri ambapo mtu hufanya uamuzi huru. Hadi wakati huo uamuzi kwa niaba yake hufanywa na mtu mzima - kama vile wazazi wake - ambaye anapaswa kuzingatia ikiwa ni kwa manufaa yake. "Na ikiwa uamuzi huo unamnyima mtoto elimu na burudani, basi ni ukiukwaji wa haki zake."
Lakini Dk Bipin Doshi, ambaye anafundisha falsafa ya Jain katika Chuo Kikuu cha Mumbai, anasema "huwezi kutumia kanuni za kisheria katika ulimwengu wa kiroho". "Wengine wanasema mtoto hajapevuka vya kutosha kufanya maamuzi hayo, lakini kuna watoto wenye uwezo mzuri wa kiakili ambao wanaweza kufikia mafanikio makubwa kuliko watu wazima wakiwa na umri mdogo. Vile vile kuna watoto ambao wana mwelekeo wa kiroho, kwa hiyo kuna ubaya gani kama watakuwa watawa?" anauliza.
Kando na hilo, Dk Doshi anasisitiza, Devanshi haumizwi kwa njia yoyote. "Anaweza kunyimwa burudani ya kitamaduni, lakini ni muhimu kwa kila mtu? Na sikubali kwamba atanyimwa upendo au elimu - atapata upendo kutoka kwa kiongozi wake na atajifunza uaminifu na kutojihusisha na ulimwengu. Je, hilo sio jambo zuri?"
Dk Doshi pia anasema kwamba iwapo Devanshi atabadilisha mawazo yake baadaye na kufikiria kwamba "alichukua uamuzi mbaya kwa kuongozwa na kiongozi wake", anaweza kurudi ulimwenguni wakati wowote.

Chanzo cha picha, RUPESH SONAWANE
Kwa nini basi usimwache aamue akiwa mtu mzima, anauliza Prof Mehta. "Akili za vijana zinaweza kuguswa na katika miaka michache, anaweza kufikiri kuwa haya sio maisha anayotaka," anasema, akiongeza kuwa kumekuwa na matukio ambapo wanawake wamebadili mawazo yao mara tu wanapokuwa watu wazima.
Prof Mehta anasema miaka michache iliyopita alishughulikia kisa cha mtawa kijana mdogo wa Jain ambaye alitoroka kituo chake kwa sababu alikuwa ameumia sana.
Msichana mwingine ambaye alijinyima raha akiwa na umri wa miaka tisa alizua kashfa ya aina yake mwaka wa 2009 baada ya kufikisha umri wa miaka 21 na kutoroka na kuamua kuolewa na aliyekuwa mpenzi wake.
Hapo awali, malalamiko pia yaliwasilishwa kortini, lakini Prof Mehta anasema mageuzi yoyote ya kijamii ni changamoto kwa sababu ya hisia zinazohusika.
"Watoto wanateseka chini ya dini zote, lakini changamoto ni lukuki," anasema, akiongeza kuwa familia na jamii zinahitaji kuelimishwa kuwa "mtoto si mali yako".












