Kwa nini ukataji wa mibuyu umezua mjadala Kenya

Na Ambia Hirsi

Tangu jadi, mti wa mbuyu umekuwa ukitumika kama sehemu ya kuendeleza maombi na tambiko kwa jamii tofauti katika eneo la Pwani ya Kenya.

Hata hivyo siku za hivi karibuni mjadala umeibuka baada ya kubainika kuwa miti hiyo imekuwa ikikatwa au kung'olewa kuuzwa nje ya nchi katika hali ya kutatanisha ambayo imewatia wasiwasi wanamazingira nchini.

‘’Huu ni uharamia wa kibiolojia’’ baadhi yao walinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani wakisema.

Pia wanadai hakuna mashauriano wala uchunguzi uliofanywa kutathmini athari za ukataji miti hiyo kwa mazingira.

Kufuatia malalamishi hayo ya umma Kenya imefutilia mbali leseni iliyotolewa kwa kampuni ya kigeni ya kung'oa na kuuza nje miti ya mbuyu kutoka eneo la pwani.

Kampuni ya Georgia ilinunua miti minane mikubwa kutoka kwa wakulima wa ndani.

Idhini ya kung'oa mibuyu, ambayo inaweza kuishi hadi miaka 2,500, haikuzingatia vigezo vinavyohitajika, Waziri wa mazingira Soipan Tuya alisema.

Ni nini kilifanyika?

Idara ya Misitu nchini Kenya (KFS) ilitoa kibali cha kung'olewa kwa miti hiyo kufuatia idhini ya Mamlaka ya kitaifa ya kulinda Mazingira,Nema kupitia ripoti ya tathmini ya athari za mazingira (EIA), huku serikali ya Kaunti ya Kilifi ikitoa vyeti vya asili na vibali vya kuvuna Oktoba 2.

Baadhi ya wakulima katika eneo la Kilifi pwani ya Kenya waliripotiwa kutaka kusafisha ardhi yao ili kupanda mahindi.

Wengine wakiripotiwa kuonyesha nia ya kufanya biashara, baada ya mamlaka husika kutoa cheti cha kuendesha mpanga huo.

Waliuza miti iliyokua katika ardhi yao ya kibinafsi kwa kati ya $800 (£670) na $2,400, gazeti la Guardian la Uingereza liliripoti.

Haijulikani miti hiyo ilikuwa na umri gani, lakini picha zinazoshirikiwa mtandaoni zinaonyesha miti iliyong'olewa yenye vigogo na matawi makubwa ya miti.

Mamlaka ya kitaifa ya Kulinda Mazingira (Nema) badaye imewasilisha kesi mahakamani kupinga mchakato huo baada ya kugundua miti hiyo ilikuwa ya kuuzwa nje ya nchi.

Mratibu wa mradi wa uhifadhi wa eneo la Pwani Francis Kagema ambaye pia ni mmoja wa wahifadhi wanaopinga kung'olewa au kukatwa kwa miti hiyo alinukuliwa Gazeti la Daily Nation nchini Kenya akisema: "Huu ni unyakuzi kwa sababu hiyo ni rasilimali yetu ya kibaolojia. Mtu anang'oa na kuipeleka nchi nyingine. Hatujui ni nani aliyeruhusu hilo na mchakato uliohusika kwa sababu hapakuwa na mashauriano,”

Bw Kagema alitoa wito kwa Nema na Huduma ya Ukaguzi wa Afya ya Mimea (Kephis) kufafanua jinsi wageni hao waliruhusiwa kuingilia rasilimali asili ya Kenya.

"Tunahitaji kujua kilichotokea kwa sababu huwezi kwenda Marekani, kung'oa mti na kuja nao Kenya. Nani atakuruhusu kufanya hivyo?"aliongeza kusema

Serikali imechukua hatua gani

Katika taarifa ya kufuta leseni ya kampuni hiyo ya kigeni, Wazara ya Kilimo ilisema kwamba mchakato huo unahitaji "kufanywa kwa njia ya uwazi na mpango wa kugawana faida na jamii pia kuwekwa wazi".

Kwa sasa wizara hiyo imeiagiza mamlaka ya uchukuzi na misitu kufuta kibali cha kilichoruhusu usafirishaji wa miti hiyo kutoka sehemu iliyokatwa pamoja na usafirishaji wake nje ya nchi, huku ikisubiri kutathminiwa upya kwa mkataba huo.

"Tumekubaliana kwamba miti ya mbuyu isisafirishwe nje ya nchi hadi makubaliano kati ya wahusika yaratibiwe ipasavyo," Waziri wa Mazingira na Misitu Soipan Tuya alisema.

Alisema wizara pia itawachukulia hatua watu watakaobainika kutofuata taratibu.

Tovuti ya habari ya UK Guardian iliripoti mwezi Oktoba kwamba miti ya mbuyu iliyokatwa ilikuwa imewekwa kwenye vizimba vya chuma huko Kilifi na ilikuwa inalindwa na maafisa wa usalama wakati ikisubiri kusafirishwa nje ya nchi.

Miti hiyo iliripotiwa kuhamishiwa kwenye bustani ya mimea huko Georgia. Pia kuna soko kubwa la mibuyu huko Australia na Afrika Kusini.

Kuna wasiwasi kwamba kuondolewa kwa mbuyu kunaweza kuwa na athari mbaya ya kiikolojia kwani aina nyingi za wadudu, wanyama watambaao na ndege hutegemea miti kwa makazi.

Faida za mbuyu

  • Mbuyu unaweza kustahimili hali mbaya ya hewa.
  • Hukua katika baadhi ya maeneo ya tropiki na mbuyu unasemekana kuwa mti unaotoa maua kwa muda mrefu zaidi duniani.
  • Hutoa maua meupe ambayo huchanua usiku, na matunda yake yanayoweza kuliwa yanaweza kuwa na urefu wa futi moja.
  • Ubuyu pia ina vitamini C nyingi na inaweza kutumika kutengeneza juisi, miongoni mwa matumizi mengine.
  • Mafuta yanyopatikana kwenye mbegu za ubuyu hutumiwa kutengeneza vipodozi na sabuni na mafuta ya mwili.