Matokeo ya uchaguzi Marekani 2024: Mzaliwa wa Kenya ashinda kiti cha ubunge katika uchaguzi wa Marekani

Chanzo cha picha, Huldah Momanyi/Facebook
Na Dinah Gahamanyi
BBC News Swahili
Mmarekani mzaliwa wa Kenya, Huldah Momanyi ameweka historia kwa kujinyakulia kiti katika Baraza la Wawakilishi katika jimbo la Minnesota.
Momanyi, 39, anakuwa mwanasiasa wa kwanza mzaliwa wa Kenya kushikilia wadhifa wake nchini Marekani.
Momanyi alikuwa akigombea kiti hicho kupitia kiti cha Chama cha Democratic-Farmer-Labor (DFL).
Alishinda asilimia 64.78 ya kura, na kupata kiti katika wadi ya 38A ya Minnesota, ambayo inajumuisha sehemu za kusini magharibi mwa Brooklyn Park na Osseo.
Wilaya 38A ni eneo lenye watu wa asili tofauti, na takriban asilimia 66 ya wakazi wanajitambulisha kama watu wa rangi, sehemu kubwa yao wakiwa wahamiaji Waafrika.

Chanzo cha picha, Huldah Momanyi/Facebook
Katika mchujo wa chama cha Democratic, alipata ushindi kwa asilimia 51.28 ya kura, akimshinda mgombea mwenza Wynfred Russell.
Ushindi wake wa kiti hicho unawakilisha hatua muhimu katika kuongezeka kwa uwakilishi wa wahamiaji wa Kiafrika katika siasa za Marekani.
Maono ya Momanyi kwa Seneti ya Jimbo la Minnesota yanahusu masuala muhimu kama vile usalama, makazi sawa na huduma ya afya inayoweza kufikiwa.
Huldah Momanyi ni nani?
- Momanyi alizaliwa katika Kaunti ya Nyamira , Kisii Magharibi mwa Kenya mwaka 1985 kwa wazazi na Tabitha na Philip Momanyi.
- Alihamia Marekani pamoja na wazazi wake akiwa na umri wa miaka tisa.
- Alipata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Betheli, Minnesota.
- Huldah Momanyi ni mama wa watoto wawili

Bi momanyi anafurahia uamuzi wake wa kuingia katika siasa kwa kujitolea kwake kuinua jamii yake na kutetea mahitaji yao katika michakato ya kutunga sheria.
Ameazimia kushughulikia maswala muhimu yanayoathiri wapiga kura wake, akizingatia makazi ya bei nafuu, ufikiaji sawa wa elimu na huduma ya afya, na kuunda fursa za kiuchumi kwa idadi tofauti ya watu anaowawakilisha.
''Ninataka kutumikia jamii hii kama mwakilishi waka kutokana na hisia kubwa ya shukrani kwa fursa ambazo jamii hii na serikali hii imeipa familia yangu na mimi mwenyewe. Nimeshuhudia uzuri wa utofauti na nguvu ya umoja. Pia nimeshuhudia mapambano na ushindi wa wale ambao walitafuta maisha bora hapa Minnesota, kama familia yangu ilivyofanya ...Matarajio yetu ya pamoja yanapaswa kuongoza sera zetu'', aliiambia BBC baada ya kushinda kiti uwakilishi cha baraza la bunge la Minnesota.












