'Kufa au kupona': Juhudi za mtu huyu kutaka kufika visiwa vya Canary

- Author, Blanca Munoz, Chris Alcock & Mame Cheikh Mbaye
- Nafasi, BBC Africa Eye
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mkulima wa Senegal Mouhamed Oualy hajawahi kwenda baharini, lakini anakaribia kuanza safari ya hatari ya baharini, ambayo imegeuza Bahari ya Atlantiki kuwa kaburi la watu wengi.
"Watu wa mashua wameniita, walisema nijitayarishe. Ninawaomba mniombee, wakati umefika,” anasema.
BBC Africa Eye imefika katika ulimwengu wa siri wa wahamiaji wanaotarajia kufika Ulaya kupitia kivuko hatari kati ya Afrika Magharibi na Visiwa vya Canary vya Uhispania.
Na Bw Oualy anataka kuwa mmoja wa wahamiaji kufikia visiwa hivyo, wahamiaji ambao idadi yao imefikia kiwango cha juu zaidi.
Serikali ya eneo hilo inaonya kwamba kinachowangoja kwenye ufuo wa miamba wa visiwa hivyo ni mfumo "umezidiwa" na "katika hatua ya mwisho" - lakini hakuna kitakachozuia uamuzi wa Bw Oualy.
The regional government there warns that what awaits them on the rocky shores of the archipelago is a system “overwhelmed” and “at breaking point” - but nothing will dent Mr Oualy’s determination.
Akiwa amepanda kwenye mashua iliyojaa watu kupita kiasi, mtumbwi wa kitamaduni wa uvuvi wa mbao, Bw Oualy anaweza kuziona siku, hata wiki, kwa huruma ya mojawapo ya bahari hatari zaidi duniani.
Kutoka Senegal, ni makadirio ya umbali wa kati ya 1,000km (maili 600) na 2,000km kwenye bahari, kulingana na mahali unapotoka, karibu mara 10 ya umbali wa njia nyingine za wahamiaji kuvuka Bahari ya Mediterania.
Kupambana na dhoruba za bahari na mikondo ya bahari yenye nguvu, wahamiaji mara nyingi huishiwa na maji huku wakiugua ugonjwa mbaya wa mwendo na hofu kubwa.
Wakati wa usiku, wakiwa wamezungukwa na maji meusi, watu mara nyingi huzidiwa na hofu na upungufu wa maji mwilini.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mbali na pwani, katika eneo la mashariki la Senegal la Tambacounda, watoto wa Bw Oualy na familia kubwa hutegemea pesa kidogo alizopata kupitia kilimo.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40 hajawaona kwa karibu mwaka mmoja, baada ya kusogea karibu na mojawapo ya sehemu kuu za kuondoka kwenye ufuo huo.
Huko amekuwa akifanya kazi kama dereva wa pikipiki, na kukopa pesa kutoka kwa marafiki, kukusanya ada ya $1,000 (£765) ili kupanda mojawapo ya vyombo vinavyoondoka kuelekea Visiwa vya Canary.
Kwa kuhofia kuwa anaweza kutapeliwa, amekubaliana na wasafirishaji haramu kwamba atatoa tu pesa kamili ikiwa mashua itafanikiwa kufika.
"Hakuna anayejua nini kinaweza kunitokea katika maji haya. Pepo wachafu wa baharini wanaweza kuniua,” anaiambia BBC.
"Boti inaweza kupinduka, na kuua kila mtu. Ikiwa utaanguka ndani ya maji, untashikilia nini? Uwezekano pekee ni kifo, lakini lazima ujitose bila kujali.
Makumi ya boti zimetoweka na mamia ya maisha kwenye vyombo . Bila mifumo ifaayo ya urambazaji, baadhi ya vyombo huacha njia na hatimaye kupeperushwa hadi kuvuka Bahari ya Atlantiki, na kusogea hadi kwenye ufuo wa Brazili.
Iwapo Bw Oualy atanusurika katika safari hiyo, anatumai kujitafutia riziki ili kutunza familia yake kubwa, lakini anaweka mipango yake kwa siri ili kuepuka kuwatia wasiwasi.
Wakati Senegal ikirekodi utendaji thabiti wa kiuchumi katika muongo mmjota tangu 2010, zaidi ya theluthi moja ya nchi bado wanaishi katika umaskini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
"Nilifanya kazi yoyote ambayo unaweza kufikiria, lakini mambo hayakuwa sawa. Ikiwa huna pesa, haijalishi. Mimi ndiye tumaini lao pekee na sina pesa,” anasema.
Kama Bw Oualy, wahamiaji wengi katika njia hii ni Waafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaokimbia umaskini na migogoro, inayochochewa na mabadiliko ya tabia nchi.
Visiwa vya Canary vimekuwa lango kuu la wahamiaji na wakimbizi wanaotarajia kufika Ulaya, hasa baada ya nchi kama vile Italia na Ugiriki kuanzisha hatua za kukabiliana na njia nyingine zinazovuka bahari ya Mediterania kutoka Libya na Tunisia.
Takribani watu 40,000 walifika mwaka wa 2023, idadi kubwa zaidi katika miongo mitatu. Kufikia sasa mwaka huu, tayari zaidi ya 30,800 wamefika kwenye fukwe zake za kitalii, zaidi ya mara mbili ya idadi ya kipindi kama hicho mwaka jana.
Hali ya hewa inapoboreka Atlantiki, serikali ya Visiwa vya Canary inahofia kuwa hali "mbaya zaidi" bado inakuja.
Katika mahojiano ya kipekee na BBC Africa Eye, Fernando Clavijo, rais wa serikali ya Visiwa vya Canary, alielezea mfumo wa dharura "uliozidiwa kupita kiasi" ambapo waokoaji wa baharini, polisi na wa kujitolea wa Msalaba Mwekundu wamekuwa wakifanya kazi kuzidi uwezo wao.
"Matokeo yake ni kwamba watu wengi zaidi watakufa, hatutaweza kuwasaidia wahamiaji jinsi inavyostahili," anaeleza Bw Clavijo.
"Hivi sasa, Ulaya imeifunga bahari ya Mediterania, ambayo ina maana kwamba njia ya Atlantiki, ambayo ni hatari zaidi, imekuwa ya kukimbilia."
BBC ilizungumza na maafisa wa huduma za dharura za Uhispania, ambao waliomba kutotajwa majina walipoelezea changamoto zao.
Mmoja alisema: "Wafanyakazi hawawezi kuvumilia tena kushuhudia kifo na uharibifu."
Huko El Hierro, kisiwa kidogo zaidi cha visiwa hivyo, idadi ya wahamiaji ambao wamefika tangu kuanza kwa 2023 tayari imeongeza zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu wa eneo hilo hadi karibu 30,000.
Bw Clavijo anasema wenyeji hawawezi kutumia mabasi ya umma kwa sababu yote yanatumiwa kubeba wahamiaji, jambo ambalo anahofia linaweza kuchochea chuki dhidi ya wageni na kusababisha machafuko ya kijamii.
"Sote tutalazimika kuwajibika, kutoka kwa Umoja wa Ulaya hadi kwa serikali ya Uhispania, kwa sababu huwezi kuondoka Visiwa vya Canary vikikabiliwa na mzozo huu."
Katika miezi ya hivi karibuni, kuongezeka kwa kasi kwa wanaowasili kumechochea mjadala mkali wa kitaifa nchini Uhispania juu ya jinsi ya kukabiliana na uhamiaji usio wa kawaida, huku Canaries ikitoa wito wa msaada zaidi wa serikali kuwatunza wanaowasili, haswa watoto walio peke yao.
Huko Senegal, Bw Oualy hatimaye ameitwa na wasafirishaji haramu kujiunga na wahamiaji wengine katika maficho ya siri. Hatima yake sasa iko mikononi mwao.
"Tuko wengi, tumejaa. Kuna watu kutoka Mali na Guinea pia. Wanatupeleka kwenye boti ndogo za watu 10 hadi 15 hadi tunafika kwenye boti kubwa, ndipo tunaondoka,” anasema.
Ili kunusurika katika safari hiyo ndefu, Bw Oualy amechukua tu chupa chache za maji na biskuti chache.
Kwa siku mbili za kwanza, alikuwa mgonjwa wakati wote. Anasimama mara nyingi kwa sababu ya ukosefu wa nafasi na analala kwenye maji ya bahari yaliyochanganywa na mafuta.
Pia anaishiwa na maji na inambidi anywe kutoka baharini.
Baadhi ya watu kwenye mashua wanaanza kupiga mayowe na kuwa wazimu. Wafanyakazi huwaambia wengine wawashikilie ili wasianguke baharini au kuwasukuma wengine.
Kulingana na takwimu kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), njia ya Atlantiki inazidi kuwa safari mbaya zaidi ya wahamiaji duniani.
Inakadiriwa kuwa watu 807 wamekufa au kutoweka hadi sasa. mwaka 2024, ongezeko la 76% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Lakini idadi ya majeruhi huenda ikawa kubwa zaidi, kwa sababu ajali mbaya huwa hazirekodiwi kwenye njia hii.
"Kila baada ya dakika 45, mhamiaji hufa akijaribu kufikia ufuo wetu. Hii ina maana kuwa wasafirishaji binadamu wanazidi kuwa na nguvu zaidi, "anasema Bw Clavijo, akirejelea data kutoka kikundi cha haki za Uhispania cha Walking Borders.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu inakadiria kuwa wahalifu hutengeneza karibu $150m kwa mwaka kwenye njia hii.
"Wasafirishaji haramu ambao hupanga safari wamegundua kuwa hii ni kama biashara ya dawa za kulevya, na kuna uwezekano mdogo wa kugunduliwa," Luteni Antonio Fuentes, kutoka timu ya Guardia Civil ya Uhispania iliyoundwa kukabiliana na wasafirishaji haramu, anaambia BBC.
"Kwao, mhamiaji ni bidhaa tu. Wanabeba watu kama wanaweza kubeba madawa ya kulevya au silaha. Ni waathirika tu."
Ili kuelewa vyema mitandao hii ya uhalifu, BBC ilizungumza na mfanyabiashara mmoja raia wa Senegal anayeandaa safari za boti, ambaye aliomba kutotajwa jina.
"Ukichukua mashua kubwa, ambayo inaweza kubeba watu 200 hadi 300, na kila mmoja wao analipa karibu dola 500, tunazungumza juu ya pesa nyingi," anasema.
Alipopingwa kuhusu wajibu wake wa uhalifu kama mlanguzi, katika safari ambayo imeua watu wengi katika jamii yake, mfanyabiashara huyo hatubu na anaiambia BBC: "Ni uhalifu, yeyote anayekamatwa anapaswa kufungwa gerezani, lakini hakuna suluhu.
"Utaona watu waliokufa majini, lakini mashua zinaendelea."
Kwa siku tano, BBC haipokei habari zozote kutoka kwa Bw Oualy. Kisha, jioni moja, anapiga simu.
"Mota ilikuwa inapata joto na upepo ulikuwa mkali sana, baadhi ya wavuvi walipendekeza tuelekee Morocco. Lakini nahodha alikataa. Alisema ikiwa tungesonga polepole, tutakuwa Uhispania kufikia saa kumi na mbili asubuhi.
Ilikuwa imesalia chini ya siku moja kufika Visiwa vya Canary wakati injini ya meli ilipopata matatizo, na wengi wa wahamiaji, wakihofia upepo mkali walipoenda mbali zaidi katika Bahari ya Atlantiki, walimuasi nahodha wao.
“Kila mtu alianza kugombana na kutukanana. Nahodha alikubali na kurejea Senegal.”
Bw Oualy alinusurika safari hiyo, lakini alipata majeraha na matatizo makubwa ya kiafya kutokana na safari hiyo.
Ana maumivu ya mara kwa mara na anatembea polepole.
Baada ya mwaka mmoja kupanga safari hiyo, Bw Oualy amerejea katika hali ya awali, na sasa amerejea kwa familia yake na anahifadhi pesa za kutosha kwa ajili ya safari nyingine.
“Natamani kurudi na kujaribu tena. Ndiyo, uaminifu kwa Mungu, hiyo ndiyo imani yangu. Hayo ni bora kwangu. Nikifa, ni mapenzi ya Mungu.”
Ikiwa Bw Oualy atafika Ulaya, kuna uwezekano hataona familia yake kwa miaka mingi. Akifia baharini watakuwa wamempoteza milele.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












