Boti kuzama Cape Verde: 'Ndugu yangu alikufa kwa ndoto ambayo sote tunayo'

Chanzo cha picha, MAMOUR BA
Ndugu wa mwanaume aliyefariki baada ya mashua iliyobeba makumi ya wahamiaji kuzama karibu na visiwa vya Cape Verde, ameiambia BBC - walikuwa wakijaribu kwenda Uhispania.
Zaidi ya watu 60 wanahofiwa kufariki kwenye boti hiyo iliyokuwa baharini kwa zaidi ya mwezi mmoja. Wengi wao walitokea Senegal.
"Kila mtu ameshituka. Alikuwa nguzo ya familia yetu," Mamour Ba anasema kuhusu kakake Cheikhouna.
Lakini mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 27 anasema, atajaribu tena safari hiyo yeye mwenyewe kwani maisha ni magumu nchini Senegal.
Ba, ni mwanafunzi kutoka mji mdogo wa wavuvi wa Fass Boye, mji wa pwani kati ya mji mkuu, Dakar, na mji wa kihistoria wa St Louis.
Ndugu zake watatu na mmoja binamu walikuwa kwenye mashua iliyosafiri kuelekea Ulaya tarehe 10 Julai kutoka Fass Boye ikiwa na watu 101.
"Walitaka kufika Uhispania. Walisema wanataka kuondoka na sikuweza kuwaambia wasifanye hivyo kwa sababu walikuwa wameshafanya maamuzi." Alidhani wote wamekufa, hadi alipopigiwa simu kutoka Cape Verde siku ya Jumatano baada ya kuokolewa.
Walikuwa miongoni mwa watu 38, wakiwemo watoto, waliookolewa. Picha zinaonyesha wakisaidiwa kufika ufuoni, wengine kwenye machela katika kisiwa cha Sal. Watu wengine 60 wanahofiwa kupotea baharini.
Njia ya kuelekea Ulaya

Visiwa hivyo viko karibu kilomita 600 (maili 372) kutoka pwani ya Afrika Magharibi na ndio njia wanayopita wahamiaji kuelekea Visiwa vya Canary, eneo la Uhispania linaloonekana na wengi kama njia ya kuelekea Ulaya.
Ba anasema bado hajui undani wa safari ya jamaa zake, kwani walikuwa wamechanganyikiwa sana: "Hawakuwa na nguvu ya kueleza kilichotokea, walisema tu: 'Tuko hai.' Walikuwa dhaifu sana."
Wakati mazungumzo yakiendelea, aligundua kuwa si wote walionusurika. “Kaka yangu mmoja, Ibrahima, alitumia simu ya mmoja wa madaktari kunipigia kutoka Cape Verde."
"Alituambia kaka yetu mwingine Cheikhouna alipotea baharini, nilishituka. Tulikuwa na ukaribu sana, alikuwa mpiganaji kweli. Alikuwa ameoa na watoto wawili."
"Siku alipoondoka alinishika mikono na kusema, Kaka lazima niende.'
"Alikuwa kaka yangu, alikuwa rafiki yangu."
Safari ya Hatari

Chanzo cha picha, LUIS COSTA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya habari za mkasa huo kuenea huko Fass Boye, ambako wengi wa waliokuwa kwenye boti hiyo walitokea, hasira zilizuka siku ya Jumatano. Wengine walichoma moto nyumba ya Meya, wakikerwa na mamlaka kuhusu ukosefu wa fursa kwa vijana.
Kuchanganyikiwa huku ni jambo ambalo Ba analifahamu sana - amejaribu takribani mara mbili kuondoka Senegal.
"Hakuna cha kufanya hapa. Kwa hivyo niliamua kujaribu kuhamia Ulaya kupitia Morocco," alisema, akizungumzia jaribio lake la kwanza wakati wa mwaka wake wa tatu chuo kikuu. Hata hivyo, mambo hayakwenda sawa, na alilazimika kurudi nyumbani.
Lakini alidhamiria kukamilisha ndoto yake ya kuhamia Ulaya - alijaribu tena, wiki chache zilizopita, mwishoni mwa Juni, akiwa na Cheikhouna. Ila jaribio hilo lilishindwa. Safari ya mwisho ya Cheikhouna lilikuwa ni jaribio lake la pili.
"Sisi ni wavuvi, tunafanya kazi siku nzima na hatupati pesa. Alitaka tu kulisha familia yake na kuwa na maisha bora."
Ba anajua ni hatari kupanda boti nyingine kuelekea Ulaya, lakini inategemea fedha.
"Sina pesa za kuchukua ndege. Ni bora kulipa dola za kimarekani 480, kwenda Uhispania kuliko kutumia mamilioni kujaribu kufika huko kwa ndege."
Anasema haogopi kuzama. "Wengine wamefanya safari hii na wamezama lakini siogopi. Ni hatari ambayo niko tayari kuichukua. Hata kama kungekuwa na mashua tayari kwenda leo, ningepanda."













