Tetemeko la ardhi Uturuki: Nilizikwa hai na mwanangu mchanga

Imepita wiki moja tangu tetemeko kubwa la ardhi liikumbe Uturuki na Syria na kuua maelfu ya watu. Lakini katikati ya hali ya kukata tamaa, pia kumekuwa na hadithi za "miujiza". Huyu ni mmoja wao.
Necla Camuz alipojifungua mtoto wake wa pili wa kiume tarehe 27 Januari, alimpa jina Yagiz, kumaanisha "mtu jasiri".
Siku 10 tu baadaye, saa 04:17 kwa saa za huko, Necla alikuwa macho akimlisha mwanawe nyumbani kwao katika mkoa wa Hatay, kusini mwa Uturuki. Muda mfupi baadaye, walifukiwa chini ya vilima vya vifusi.
Necla na familia yake waliishi kwenye ghorofa ya pili ya jengo la kisasa la ghorofa tano katika mji wa Samandag. Lilikuwa ni "jengo zuri", anasema, na alijisikia salama pale.
Hakujua asubuhi hiyo kwamba eneo hilo lingesambaratishwa na tetemeko la ardhi, huku majengo yakiharibiwa kila kukicha.
"Tetemeko la ardhi lilipoanza, nilitaka kwenda kwa mume wangu ambaye alikuwa katika chumba kingine, naye alitaka kufanya hivyo," anasema.
"Lakini alipojaribu kuja kwangu na mtoto wetu mwingine, kabati la nguo liliwaangukia na haikuwezekana kwa wao kusogea"
"Tetemeko lilipozidi kuwa kubwa, ukuta ulianguka, chumba kilikuwa kinatikisika, na jengo lilikuwa linabadilika, liliposimama sikugundua kuwa nilikuwa nimeanguka ghorofa moja chini. Nilipiga kelele kuita majina yao lakini hakukua na jibu. "
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 33 alijikuta akilala chini na mtoto wake kifuani, akiwa bado ameshikwa mikononi mwake. Kabati lililoanguka karibu naye lilikuwa limeokoa maisha yao kwa kuzuia saruji kuwaponda.
Wanandoa hao walibaki humokwa karibu siku nne.
Siku ya kwanza
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akiwa amevaa nguo zake za kulalia chini ya vifusi, Necla hakuona chochote zaidi ya "giza tupu" kwa hiyo ilimbidi ategemee hisia zake nyingine kutambua kilichokuwa kikiendelea.
Kwa bahati, aliweza kubaini mara moja kwamba Yagiz alikuwa bado anapumua.
Kwa sababu ya vumbi, mwanzoni alijitahidi kupumua, lakini baadaye alimudu. Kulikuwa na joto katika kifusi.
Alihisi kana kwamba kulikuwa na vitu vya kuchezea vya watoto chini yake lakini hakuweza kujisogeza kukagua.
Zaidi ya kabati la nguo, ngozi laini ya mtoto wake mchanga, na nguo walizovaa, hakuweza kuhisi chochote isipokuwa saruji na uchafu.
Kwa mbali aliweza kusikia sauti. Alijaribu kupiga kelele kuomba msaada na kugonga kabati la nguo.
"Kuna mtu huko? Kuna mtu anaweza kunisikia?" aliita.
Hilo liliposhindikana, aliokota vipande vidogo vya kifusi vilivyokuwa vimedondoka karibu yake na kutumia vile kugonga kabati la nguo, akitumaini kwamba angesikika zaidi. Aliogopa kugonga uso wake ikiwa litaanguka.
Bado, hakuna aliyejibu.
Necla aligundua kuna uwezekano hakuna mtu angekuja.
"Niliogopa," anasema.
Maisha chini ya kifusi
Katika giza chini ya vifusi, Necla alipoteza hisia zote.
Hivi sivyo maisha yalivyopaswa kuwa.
"Unapanga mambo mengi unapokuwa na mtoto mpya, halafu... ghafla unakuwa kwenye kifusi," anasema.
Bado, alijua kwamba alipaswa kumtunza Yagiz, na aliweza kumnyonyesha katika mazingira hayo magumu.
Hakukuwa na chanzo cha maji au chakula ambacho angeweza kupata kwa ajili yake mwenyewe. Kwa kukata tamaa, alijaribu kunywa maziwa yake mwenyewe bila mafanikio.
Necla aliweza kuhisi sauti ya kitu kikichimba na kusikia hatua na sauti, lakini sauti hizo zilisikika kwa mbali.
Aliamua kutunza nguvu zake na kukaa kimya isipokuwa kelele kutoka nje zilikuja karibu.

Alifikiria mara kwa mara kuhusu familia yake, mtoto kwenye kifua chake, na mume na mtoto walipotea mahali fulani kwenye uchafu.
Pia alikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi wapendwa wengine walivyoendelea katika tetemeko la ardhi.
Necla hakufikiria angeweza kutoka kwenye vifusi, lakini uwepo wa Yagiz ulimpa sababu ya kubaki na matumaini.
Muda mwingi alilala, na alipoamka akilia, alikuwa akimlisha kimyakimya hadi atulie.
Kuokolewa
Baada ya zaidi ya saa 90 chini ya ardhi, Necla alisikia sauti ya mbwa wakibweka. Alijiuliza kama alikuwa anaota.
"Uko sawa? Gonga mara moja ndiyo," mmoja aliita kwenye kifusi. "Unaishi ghorofa gani?"
Alikuwa amepatikana.
Waokoaji walichimba ardhini kwa uangalifu ili kumpata, alipokuwa akimshikilia Yagiz.
Giza lilivunjwa na mwanga wa tochi ukimulika machoni mwake.
Timu ya uokoaji kutoka Idara ya Zimamoto ya Manispaa ya Istanbul ilipouliza Yagiz ana umri gani, Necla hakuweza kuwa na uhakika. Alijua tu kwamba alikuwa na umri wa siku 10 wakati tetemeko la ardhi lilipotokea.

Chanzo cha picha, EKREM IMAMOGLU
Baada ya kumkabidhi Yagiz kwa waokoaji, Necla alibebwa kwenye machela mbele ya watu walioonekana kuwa wengi. Hakuweza kutambua nyuso zozote.
Alipopelekwa kwenye gari la wagonjwa, alitafuta uthibitisho kwamba mwanawe mwingine pia alikuwa ameokolewa.
Alipofika hospitalini, Necla alilakiwa na wanafamilia waliomwambia kwamba mume wake wa miaka sita, Irfan, na mtoto wake wa miaka mitatu, Yigit Kerim, walikuwa wameokolewa kutoka kwenye vifusi.
Lakini walikuwa wamehamishwa kwa muda wa saa kadhaa hadi hospitalini katika jimbo la Adana, wakiwa wamejeruhiwa vibaya miguu.

Ajabu, Necla na Yagiz hawakuwa wamejeruhiwa vibaya kimwili. Waliwekwa hospitalini kwa saa 24 kwa uangalizi kabla ya kuruhusiwa.
Necla hakuwa na nyumba ya kurudi, lakini mwanafamilia mmoja alimrudisha kwenye hema la muda la bluu lililoundwa kwa mbao na turubai. Kuna 13 kati yao huko kwa jumla - wote wamepoteza makazi yao.
Necla "anajaribu" kukubaliana na kile kilichomtokea. Anasema ana deni la Yagiz kwa kuokoa maisha yake.
"Nadhani kama mtoto wangu hangekuwa na nguvu za kutosha kushughulikia hili, nisingekuwa pia," anaelezea.
Ndoto yake pekee kwa mtoto wake ni kwamba hatapitia kitu kama hiki tena.
"Nina furaha sana yeye ni mtoto mchanga na hatakumbuka chochote," anasema.
Simu inapoingia Necla anatabasamu. Kutoka kwenye kitanda cha hospitali Irfan na Yigit Kerim wanatabasamu na kupunga mkono.
"Habari shujaa, hujambo mwanangu?" Irfan anamuuliza mtoto wake kupitia skrini.















