Vita vya Pili vya Dunia: Ndege 600 za Marekani zilianguka milima ya Himalaya

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Soutik Biswas
- Nafasi, BBC
Jumba la makumbusho lililofunguliwa hivi karibuni nchini India linahifadhi mabaki ya ndege za Marekani zilizoanguka kwenye Milima ya Himalaya wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Tangu mwaka wa 2009, timu za India na Marekani zilizunguka milimani katika jimbo la kaskazini-mashariki la India la Arunachal Pradesh, kutafuta mabaki na wafanyakazi waliopotea wa mamia ya ndege zilizoanguka zaidi ya miaka 80 iliyopita.
Ndege 600 za usafiri za Marekani zinakadiriwa kuanguka katika eneo hili, na kuua takribani abiria na wafanyakazi wa anga 1,500 - wakati wa operesheni ya kijeshi ya miezi 42 ya Vita vya Pili vya Dunia nchini India. Miongoni mwa waliopoteza maisha ni marubani wa Marekani na China, waendesha mawasiliano ya redio na wanajeshi.
Operesheni hiyo ilitumia njia muhimu ya usafiri wa anga kutoka majimbo ya Assam na Bengal ya India ili kusaidia vikosi vya China huko Kunming na Chunking (sasa Chongqing).
Vita Vyafika India

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Vita kati ya madola ya Axis (Ujerumani, Italia, Japan) dhidi ya ushirika wa (Ufaransa, Uingereza, Marekani, Umoja wa Kisovieti, China), vilifika kaskazini mashariki mwa India iliyokuwa ikitawaliwa na Uingereza.
Njia ya anga ndio ikawa ya kuokoa maisha kufuatia Wajapani kusonga mbele hadi kwenye mipaka ya India, ambayo ilifunga njia ya ardhini kuelekea China kupitia kaskazini mwa Myanmar (wakati huo ikijulikana kama Burma).
Operesheni ya kijeshi ya Marekani, iliyoanzishwa Aprili 1942, ilifanikiwa kusafirisha tani 650,000 za vifaa vya vita, mafanikio ambayo yaliimarisha ushindi wa washirika wake. Marubani waliita njia hiyo ya hatari ya ndege "The Hump."
Kutafuta Mabaki

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Katika kipindi cha miaka 14 iliyopita, timu za Marekani na India zinazojumuisha wapanda milima, wanafunzi, madaktari, wanaakiolojia na wataalamu wa uokoaji waliingia katika misitu minene na miinuko iliyofikia futi 15,000 (mita 4,572) huko Arunachal Pradesh, inayopakana na Myanmar na China.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa usaidizi kutoka kwa watu wa makabila ya wenyeji safari zao za mwezi mzima zimefikia maeneo ya ajali, na kupata takribani ndege 20 na mabaki ya wafanyikazi kadhaa wa ndege waliopetea.
Ni kazi yenye changamoto; safari ya siku sita, baada ya safari ya siku mbili ya barabarani, hadi kufikia ugunduzi wa eneo moja la ajali. Timu moja ilikwama milimani kwa wiki tatu baada ya kukumbwa na dhoruba ya theluji.
"Kutoka tambarare hadi milimani, ni eneo lenye changamoto. Hali ya hewa inaweza kuwa kikwazo na kwa kawaida tunafanya kazi majira ya kumalizika kwa vuli na mwanzoni mwa msimu wa baridi," anasema William Belcher, mwanaanthropolojia aliyehusika katika safari hiyo (mtaalamu wa elimu ya binaadamu ihusuyo asili na maendeleo yake).
Mabaki mengi yamegundulika; mitungi ya oksijeni, bunduki, mafuvu ya kichwa, mifupa, viatu na saa – vyote vimepatikana kwenye vifusi na sampuli za DNA zilizochukuliwa kutambua waliofariki. Baadhi ya maeneo ya ajali yamevamiwa na wanakijiji kwa miaka mingi na baadhi ya mabaki huyauza kama chuma chakavu.
Makumbusho Mpya

Chanzo cha picha, HUMP MUSEUM
Mabaki yaliyopatikana sasa yako Jumba jipya la Makumbusho lililofunguliwa la, ‘The Hump Museum’ huko Pasighat, katika mji wa Arunachal Pradesh, chini ya milima vya Himalaya.
Balozi wa Marekani nchini India, Eric Garcetti, alifanya ufunguzi wa makumbusho hiyo tarehe 29 Novemba, akisema, "Hii sio tu zawadi kwa Arunachal Pradesh au familia zilizoathiriwa, lakini ni zawadi kwa India na dunia."
Mkurugenzi wa jumba la makumbusho, Oken Tayeng anasema: "Pia ni kutambua mchango wa wenyeji wa Arunachal Pradesh ambao ni sehemu ya misheni hii ya kuheshimu kumbukumbu za wengine."
Simulizi za Mashuhuda

Chanzo cha picha, WILLIAM BELCHER
Meja Jenerali William H Tunner, rubani wa Jeshi la Anga la Marekani, anakumbuka, hali ya hewa kwenye milima ya Himalaya, “ilibadilika dakika hadi dakika, maili hadi maili.”
Tunner anasema, “dhoruba ya upepo mkali, mvua ya mawe na mvua nzito vyote vilileta changamoto kubwa wakati wa kuidhibiti ndege.”
Theodore White, mwandishi wa jarida la Life aliyeruka mara tano kwa ajili kuandaa makala yake, aliandika kwamba, “rubani wa ndege moja iliyobeba wanajeshi wa China bila parashuti aliamua kutua baada ya ndege yake kupigwa na barafu.”
Rubani mwenza na mwendeshaji wa redio walifanikiwa kutua kwenye mti mkubwa na walitangatanga kwa siku 15 kabla ya wenyeji kuwapata. Jamii za wenyeji katika vijiji mara nyingi huwaokoa na kuwauguza manusura wa ajali hizo.
“Haishangazi kuona simu za rununu zimejaa sauti za ‘mayday.’ Ndege zilipeperushwa mbali sana na kugonga milimani hata marubani hawakujua kwamba wamepeperushwa kwa umbali wa maili 50,” Tunner.
Dhoruba moja iliwahi dondosha ndege tisa na kuua abiria na wafanyakazi 27. Katika mawingu haya, mtikisiko hungeongezeka zaidi na sijawahi ona hali kama hiyo popote ulimwenguni kabla au tangu wakati huo," anaeleza Tunner.
Wazazi wa watu waliopotea walikuwa na maswali juu ya watoto wao: "Mwanangu yuko wapi? Je, yuko huko juu katika ardhi nzuri, anakunywa maji kwenye chemchemi, au bado anazurura katika misitu na milima ya India?" Anauliza Pearl Dunaway, mama wa rubani aliyepotea, Joseph Dunaway, katika shairi lake la 1945.
"Wanaume waliokuwa wakipigana na Wajapani msituni na katika milima mchana kutwa na usiku kucha, kila siku kwa mwaka mzima. Ulimwengu pekee wanaoujua ni ndege. Hawaachi kuzisikia, kupaa nazo, kuzikarabati huku wakilaani. Lakini hawachoki kutazama ndege zikienda China," anasimulia White.
Operesheni hiyo kwa kweli ilikuwa kazi ya hatari ya vita vya angani vilivyofika mlangoni mwa India.
"Milima na watu wa Arunachal Pradesh walikuwa katikati ya matukio, ushujaa na majanga ya Vita vya Pili vya Dunia na operesheni ya Hump," anasema Tayeng.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Munira Hussein.












