Je, sheria ya udhibiti wa mapenzi ya jinsia moja Uganda imepokewaje?

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili

Tangu taarifa kuhusu kupitishwa kwa sheria inayodhibiti mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda kutiwa saini na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jumatatu, taasisi na watu mbalimbali wamekuwa wakichukua hatua na kutoa maoni kuihusu.

Sheria hii imepingwa imekabiliwa na upinzani mkali hususani kutoka kwa viongozi wa nchi za Magharibi pamoja na taasisi za kimataifa.

Rais wa Marekani Joe Biden aliikosoa vikali sheria mpya ya Uganda dhidi ya wapenzi wa jinsia moja akiitaja kuwa sheria ya Uganda dhidi ya wapenzi wa jinsi moja kuwa ni ukiukaji 'wa kutisha wa haki za binadamu' , akitaka sheria hiyo ifutwe.

‘’Hakuna mtu anayepaswa kuishi kwa hofu ya mara kwa mara maishani mwake au kufanyiwa vurugu na ubaguzi,’’, alisema Biden.

Biden amesema utawala wake utaangalia uwezekano wa kuiwekea vikwazo Uganda na kuweka masharti ya kuingia Marekani kwa watu wanaohusika na ukiukaji wa haki za binadamu na ufisadi nchini Uganda.

Mbali na Marekani, Uingereza pia imeonekana kukerwa na sheria ya udhibiti wa mapenzi ya jinsi moja.

‘’Serikali ya Uingereza imeshtushwa na kwamba Serikali ya Uganda imetia saini muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja wa 2023 wenye ubaguzi kuwa sheria.’’, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Andrew Mitchell amesema katika taarifa yake.

Taarifa hiyo imesema Sheria hii inadhoofisha ulinzi na uhuru wa Waganda wote uliowekwa katika Katiba ya Uganda na kwamba itaongeza hatari ya ghasia, ubaguzi na mateso, kurudisha nyuma mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, na itaharibu sifa ya kimataifa ya Uganda.

''Tutaendelea kutetea haki na uhuru huu nchini Uganda na duniani kote.'' alisisitiza Waziri wake wa mambo ya kigeni wa Uingereza.

Mbali na Uingereza pia taasisi za ufadhili zimeelezea kutoridhishwa na kuidhinishwa kwa sheria ya kudhibiti uhusiano wa kimapenzi wa watu wa jinsi moja nchini Uganda.

Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund), Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa kuhusu VVU/UKIMWI ( UNAIDS ), na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) wameeleza kushikitishwa na hatua ya Bw Museveni.

Katika taarifa ya pamoja taasisi hizo zimesema zinasikitishwa sana na athari mbaya ya Sheria ya Uganda ya Kupambana na Mapenzi ya jinsi moja 2023 kwa afya ya raia wake na athari zake katika mwitikio wa UKIMWI ambao umefanikiwa sana hadi sasa.

''Unyanyapaa na ubaguzi unaohusishwa na kupitishwa kwa Sheria hiyo tayari umesababisha kupunguza upatikanaji wa huduma za kinga na matibabu. Imani, usiri, na ushiriki usio na unyanyapaa ni muhimu kwa mtu yeyote anayetafuta huduma ya afya. Watu wa LGBTQI+ nchini Uganda wanazidi kuhofia usalama na usalama wao, na idadi inayoongezeka ya watu wanakatishwa tamaa kutafuta huduma muhimu za afya kwa kuhofia kushambuliwa, kuadhibiwa na kutengwa zaidi'', imesema taarifa hiyo iliyosainiwa pia na Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji, UNAIDS, na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni raia wa Uganda.

Nchini Uganda kwenyewe tayari makundi na wanaharakati wanaounga mkono mapenzi ya jinsi wamekwenda katika Mahakama ya Kikatiba , wakitaka kubadilisha sheria hiyo mpya, huku shutuma dhidi ya uamuzi wa Bw Museveni zikiendelea kutoka katika mataifa ya Magharibi.

Katika hoja yao kwa mahakama wamesema kuwa sheria hiyo ni kinyume na inapinga haki ya kutobaguliwa, kwa kuharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja.

Sheria hiyo mpya inataja kifungo cha maisha kwa wale wanaopatikana na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.

Lakini kwa upande mwingine, viongozi wa kidini wamemsifu Rais Museveni kwa kutia saini sheria ya kupinga mapenzi ya jinsi moja.

''Tunashukuru Rais ametia saini kuwa sheria Sheria ya Kupambana na Mapenzi ya Jinsi Moja …Nchi zinazotetea LGBTQI zimetuonyesha matokeo mabaya. Tunamshukuru rais kwa kutosalimu amri kwa vitisho vyao na kuilinda Uganda dhidi ya njia zao za kujiangamiza''. Alibainisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda Samuel Kaziimba katika taarifa yake, huku viongozi wengine madhehebu makuu Uganda wakimuunga mkono.

Kuhusu sheria mpya dhidi ya mapenzi ya jinsia moja

  • Mtu anayepatikana na hatia ya kulea au kusafirisha watoto kwa madhumuni ya kuwashirikisha katika vitendo vya wapenzi wa jinsia moja anakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
  • Watu binafsi au taasisi zinazounga mkono au kufadhili shughuli au mashirika ya haki za LGBT, au kuchapisha, kutangaza na kusambaza nyenzo na fasihi za vyombo vya habari vinavyounga mkono wapenzi wa jinsia moja, pia watakabiliwa na mashtaka na kufungwa gerezani.
  • Mnamo mwaka wa 2014, mahakama ya kikatiba ya Uganda ilibatilisha kitendo kingine ambacho kilikuwa kimeimarisha sheria dhidi ya jumuiya ya LGBT.
  • Inajumuisha kuharamishwa kwa ukuzaji na ufadhili vikundi na shughuli za LGBT, na pia kusisitiza kwamba vitendo wapenzi wa jinsia moja vinapaswa kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha, jambo linaloaaniwa na Magharibi.
  • Mahusiano ya watu wa jinsia moja yamepigwa marufuku katika nchi zipatazo 30 za Afrika, ambapo watu wengi wanashikilia maadili ya kihafidhina ya kidini na kijamii.