Daktari wa Marekani ambaye hawezi kusahau alichokiona Gaza

as

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Jenna Ayyad mwenye umri wa miaka saba - amehamishiwa kusini mwa Gaza ambako anapokea matibabu.
    • Author, Fergal Keane
    • Nafasi, BBC

Onyo: Makala haya yana maelezo na picha ambazo zinaweza kuwahuzunisha baadhi ya wasomaji

Sam Attar anaamini aliacha sehemu ya nafsi yake huko Gaza. Alishuhudia mateso na hakuweza kugeuka nyuma. Ni sehemu ambayo sasa hawezi kuisahau.

Ni wiki tatu zimepita tangu arudi nyumbani Chicago, Marekani lakini anahisi kama jana.

Jenna, msichana mdogo aliyedhoofika, akiwa kwenye kitanda cha hospitali, huku mama yake akimwonyesha Sam video kwenye simu ya siku yake ya kuzaliwa. Siku za furaha kabla ya maafa.

Mama mwingine ambaye mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 10 alikuwa ametoka tu kufariki.

"Mama huyo aliniambia kwa uso wa huzuni mtoto wake amekufa dakika tano tu zilizopita. Wafanyikazi walikuwa wakijaribu kuufunika mwili wake kwa blanketi lakini alikataa kuwaruhusu. Alitaka kutumia muda zaidi kuwa naye.

Alikuwa akihuzunika, akilia, na akakaa hivyo kwa takriban dakika 20, hakutaka kuondoka ulipo mwili wa mwanawe."

Pia kulikuwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 50, aliyesahaulika katika chumba, akiwa amekatwa miguu yote miwili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mwanaume huyo amepoteza watoto wake, wajukuu zake, nyumba yake," Sam anasema, "na yuko peke yake kwenye kona ya hospitali hii yenye giza, funza wakitoka kwenye majeraha yake na alikuwa akipiga kelele:

‘Mafunza wananila nikiwa hai, tafadhali nisaidie.' Hiyo ilikuwa moja kati ya mara nyingi, niliacha kuhesabu lakini. Hao ndio watu ambao bado nawafikiria kwa sababu bado wapo.

Sam katika miaka yake ya 40, mtoto wa madaktari wawili, alizaliwa na kukulia huko Chicago, anafanya kazi kama daktari wa upasuaji katika hospitali ya Northwestern. Akiwa Gaza alihifadhi shajara za video na kurekodi matukio.

Kwa wiki mbili mwezi Machi na Aprili - kwa niaba ya NGO ya Palestinian American Bridge - alifanya kazi katika hospitali za Gaza ambazo zilikuwa na upungufu mkubwa wa kila kitu isipokuwa wagonjwa waliojeruhiwa vibaya. Siku alipoingia Gaza alishuhudia njaa.

"Tulizungukwa na watu waliokuwa wakigonga magari, baadhi ya watu wakijaribu kurukia magari. Madereva hawasimami kwa sababu wakisimama watu wanarukia kwenye magari. Hawajaribu kutudhuru. Wanaomba tu chakula. Wana njaa.

Kila siku kulikuwa na msongo wa mawazo katika kutekeleza maamuzi, kuamua ni nani angeweza kuokolewa, na nani hakuwa na nai hakuna tumaini la kupona.

Wagonjwa walikuwa wamelala kwenye sakafu za hospitali wakiwa wamezingirwa na damu na bandeji, vilio vya uchungu na vya jamaa waliokuwa na huzuni.

Huwezi kusahau huzuni kama hivyo. Hata kama wewe ni daktari uliyefunzwa na uzoefu wa muda mrefu wa maeneo ya vita kama Ukraine, Syria na Iraq.

"Bado nawafikiria wagonjwa wote niliowahudumia," anasema, "madaktari wote ambao bado wako Gaza.

Kuna hatia na aibu kidogo kuondoka kwa sababu kuna mengi ya kufanya. Mahitaji ni mengi sana. Na unawaacha watu ambao bado wapo na bado wanateseka."

Pia unaweza kusoma

Hali ni Mbaya

s

Chanzo cha picha, Sam Attar

Maelezo ya picha, Dk Attar amefanya safari tatu kwenda Gaza tangu vita vilipoanza na anapanga kwenda tena

Safari yake ya mwisho – ikiwa ni ya tatu kwenda Gaza tangu vita kuanza - alijiunga na timu ya kwanza ya madaktari wa kimataifa kupelekwa katika hospitali kaskazini mwa Gaza ambako utapiamlo umekithiri.

Misheni hiyo iliandaliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ambalo limeonya juu ya kutokea baa la njaa.

Takriban 30% ya watoto walio chini ya umri wa miaka miwili wanaripotiwa kuwa na utapiamlo mkali, na 70% ya wakazi wa kaskazini mwa Gaza wanakabiliwa na kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita "njaa mbaya."

Mwezi uliopita Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, aliishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita unaoweza kutokea kutokana na mzozo wa chakula huko Gaza.

"Kuendelea kwa vikwazo vya Israel katika kuingia kwa msaada huko Gaza, pamoja na namna inavyoendelea kushambulia, kunaweza kuwa ni matumizi ya njaa kama silaha ya vita," alisema.

Israel inakanusha hili na imeilaumu Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kwa utoaji wa polepole au usiotosheleza wa misaada.

Serikali ya Israel ilisema hesabu za Umoja wa Mataifa kuhusu njaa zilitokana na "dosari nyingi za kiufundi." Serikali imesema ilifuatilia ripoti za vyombo vya habari kwamba masoko ya chakula huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kaskazini, yana bidhaa za kutosha.

"Tunakataa moja kwa moja madai yoyote kwamba Israel inakusudia kuwaweka na njaa watu wa Gaza," ilisema taarifa kutoka COGAT - Mratibu wa Shughuli za Serikali katika eneo hilo.

Mkasa wa Jenna

xd

Chanzo cha picha, Sam Attar

Maelezo ya picha, "Mahitaji ni mengi sana. Na unawaacha watu ambao bado wapo na bado wanateseka."

Kulikuwa na msichana mdogo, Jenna Ayyad, mwenye umri wa miaka saba, "mifupa na skeletoni tu" mama yake alitarajia kufika kusini mwa Gaza ambako vifaa bora vya matibabu vinapatikana.

Jenna ana utapiamlo. Anaugua ugonjwa ambao hufanya usagaji chakula kuwa ngumu. Hali yake mbaya imechangiwa na hali ya vita na pia anasumbuliwa na wahaka.

"Nifanye nini? Hawezi kutibiwa," Nisma Ayyad alisema. "Hali yake ya kiakili ni ngumu sana. Hazungumzi kabisa na mtu yeyote. Hali yake ni mbaya, na kama mama, siwezi kufanya chochote."

Dkt Attar anasema wakati timu yake ikipakia kurejea Gaza kusini, mamake Jenna alimwendea.

"Mama yake Jenna alinijia na kusema, 'Nilidhani tunaondoka nawewe? Kwa nini unaondoka na sisi tunabaki?"

Sam alilazimika kumweleza kuwa msafara huo kwenda kusini uliidhinishwa tu kwa usambazaji wa mafuta na chakula na sio kubeba wagonjwa.

Lakini kabla ya kuondoka Sam na wenzake walijaza karatasi muhimu ili Jenna ahamishwe. Ingechukua siku kadhaa lakini walihakikisha makaratasi yanafika kwenye ofisi zinazofaa. Sam alipokwenda kuzungumza na mama yake Jenna, mama wengine waligundua.

"Tatizo vyumba viko wazi, pamoja na wagonjwa kama 10 katika chumba kimoja. Kwa hiyo wakati akina mama wengine waliponiona nikizungumza naye, wote walinivamia."

Jenna alihamishwa na sasa anatibiwa katika hospitali ya International Medical Corps karibu na Rafah.

Takwimu za Kutisha

as

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Sehemu kubwa za Gaza ni magofu na msaada kidogo sana umefika maeneo ya kaskazini

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa mwezi uliopita wengi wa waliouawa katika vita hivyo ni wanawake na watoto; watoto 13,000, wanawake 9,000.

Vita hivi sasa viko katika mwezi wake wa saba. Mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa mateka yamekwama.

Mchana na usiku waliojeruhiwa na walio na utapiamlo hufika katika hospitali chache zinazofanya kazi ambazo zimesalia. WHO inasema ni hospitali 10 tu kati ya 36 za Gaza ambazo bado zinafanya kazi.

Kusafiri Gaza kunaweza kuwa hatari sana kwa wafanyikazi wa misaada. Mfano vifo vya wafanyakazi saba wa kutoa misaada, wakiwemo Waingereza watatu, wakati jeshi la Israel liliposhambulia msafara wao kwa mashambulizi ya makombora tarehe 1 Aprili.

Sam anaelezea kupanga foleni saa katika vituo vya ukaguzi vya Israel. "Mara nyingi tunasubiri saa moja hadi nne ili Waisraeli kuidhinisha msafara kwa sababu wanaendesha operesheni za kijeshi."

Daktari wa Marekani anataka kuona ushirikiano wa pamoja ili msaada zaidi ufike kaskazini.

"Kaskazini inahitaji msaada zaidi, inahitaji chakula zaidi, mafuta mengi, maji mengi, barabara zinapaswa kufunguliwa. Kuna wagonjwa wengi ambao wanahitaji kuhamishwa kutoka kaskazini kwenda kusini. Hospitali zimezidiwa."

Ana matumaini atarudi tena Gaza hivi karibuni.

Mfanyakazi wa huduma ya kwanza, Nabil ambaye Sam alikuwa akimuona kila siku, akiwaleta majeruhi kwa matibabu, hadi yeye mwenyewe akawa mhanga ambaye alichomolewa kwenye kifusi na wenzake. Yuko hai lakini hataweza kuondoka Gaza.

Daktari ambaye binti yake aliuawa lakini alipata ukarimu wa kumfariji mama ambaye mtoto wake mdogo alikuwa akiugua jeraha la ubongo lililosababishwa na mlipuko ya bomu.

Kuna wagonjwa na familia zao ambao huwaona madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya sio wasaidizi tu, lakini ni mwanga wa ubinadamu katika mahali pa hofu na uharibifu.

Hawa wote ni watu wa Sam. Wote hawa

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah