Mauaji sugu yaliyoitikisa Kenya

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Zamani za kale ingekuwa vigumu kufikiria kama kungetokea muuaji sugu, mtu ambaye kuua imekuwa mazoea yake. Lakini katika miaka ya hivi majuzi tabia ya kustaajabisha na kuogofya imeonekana kujirudia mara kwa mara.
Simulizi zinazotolewa na jamaa za waathirika ni za kusikitisha. Mara nyingi, mtu anatoka akiwa anakwenda kwenye shughuli zake kama kawaida, lakini cha ajabu ni kwamba, ikiwa ndio zake 40 zimefika, licha ya kuwa ameaga ndugu, jamaa au marafiki na hata kugusia mipango ya keshoye, kutoka kwake siku hiyo, inaweza kuwa kwaheri ya kutoonana.
Pia kumekuwa na matukio yanayoacha maswali mengi zaidi kuliko majibu. Katika maandamano ya kupinga mswada tata wa fedha uliotupiliwa mbali na Rais William Ruto, familia zimejitokeza kutafuta wapendwa wao ama wanadaiwa kutekwa nyara au hawajulikani walipo.
Wakati joto la kisiasa likiwa bado liko juu, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) ilijitokeza na kuzungumzia dhidi ya mauaji ya kiholela kwa kuzingatia matukio kadhaa ya hivi karibuni, kwa mfano, ugunduzi wa mwili wa aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji Denzel Omondi katika machimbo ya Juja, ikitaka uchunguzi wa kina wa kisayansi kubaini chanzo na muda wa kifo chake.
Mambo mengi yakiwa yanaendelea kwa wakati mmoja, leo tuangazie mauji ambayo yamewahi kuishtua Kenya.
Collins Jumaisi Khalusha
Katika tukio la hivi karibuni zaidi, Collins Jumaisi Khalusha, 33, aliyetangazwa na polisi kuwa amekiri kuwaua wanawake 42, moja kwa moja akaingia katika kundi la wauaji sugu.
Hilo lilijiri baada ya miili 9 iliyokatwa katwa kupatikana imewekwa kwenye magunia, ikafungwa kwa kamba na kutupwa katika eneo la machimbo ya Kware ambalo kwa sasa linatukima kama eneo la kutupa takataka lililo karibu na kituo cha polisi mtaani Mukuru, jijini Nairobi.
Collins Jumaisi Khalusha alidai kuanza kwa kumuua mke wake na kuendelea na wanawake wengine tangu mwaka 2022.
Ofisa wa KNCHR Roseline Odede alisema katika taarifa waliotoa kwamba uchunguzi wa kina ufaa kufanyika.
"Matukio ya Mukuru kwa Njenga ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Kifungu cha 26 cha Katiba kinahakikisha haki ya kuishi kwa kila binadamu," Odede alisema.
Odede aliongeza kuwa tume hiyo inataka uchunguzi wa kitaalamu kuhusu vifo hivyo ili kubaini chanzo chake.
Lakini sasa kujulikana kwake kumezua maswali mengi kama vile, miili ya waathirika ilitupwa vipi mita chache kutoka kituo cha polisi bila wao kugundua, miili hiyo ilikuwa kwenye eneo hilo la jalalani kwa muda gani, polisi waliwezaje kumkamata mshukiwa ndani ya kipindi kifupi hivyo, waathirika ni kina nani na polisi wanasema nini kuhusu usalama wa wanawake nchini Kenya?
Shakahola

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tukio ambalo bado lipo kwenye kumbukumbu ya Wakenya ni mauaji ya watu katika madhehebu ya kidini iliyoongozwa na Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International.
Hadi kufikia kipindi mambo hayo yanajulikana paruwanja, ni vigumu kujua yalikuwa yameendelea kufanyika kwa muda gani huku idadi kubwa ya watu hasa watoto na wanawake wakiwa ndio walioathirika zaidi.
Inasemekana kwamba kiongozi wa madhehebu hiyo Mchungaji Paul Nthenge Mackenzie alitoa mahubiri tata kuwa nyakati za mwisho zimekaribia, na kuchochea mamia ya wafuasi wake “kufunga” hadi kufa ili kumwona Yesu, jambo ambalo anakanusha.
Pamoja na wenzake 38, wanakabiliwa na makosa 16, likiwemo la kutesa watoto, kati ya mwaka 2020 na 2023 katika Msitu wa Shakahola.
Wanayodaiwa kutekeleza ni pamoja na kuwapiga makofi na kuwachapa watoto wa kati ya miaka 8 na 14, na hivyo kuwadhuru mwili kwa tarehe tofauti.
Moja ya shitaka aliloshtakiwa nalo kiongozi wa kanisa hilo lilisema, “Paul Nthenge Mackenzie, almaarufu Mtumishi almaarufu Nabii almaarufu Papaa, tarehe zisizojulikana mwaka wa 2019 katika Kaunti ya Kilifi, kwa makusudi alimtoa mtoto wa miaka kumi na tatu (13) kutoka Shule ya Msingi ya Inavi na akashindwa kuhakikisha kwamba mtoto huyo anahudhuria shule mara kwa mara kama mwanafunzi."
Wafuasi wake walipatikana wakiwa katika mfungo usiokuwa na kikomo, wakidai kwamba waliarifiwa hiyo ni moja ya njia ya kwenda kukutana na mwokozi wao.
3. Evans Wafula
Mwaka 2021, mwanaume kwa jina Evans Wafula, alikamatwa na polisi kwa madai ya kushawishi wasichana wadogo kati ya umri wa miaka 10 na 15 ambao aliwanyanyasa king’ono na kuwaua zaidi ya 10.
Kulingana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alionyesha namna alivyowahadaa na kuwataja majina waathirika. Pia aliwapeleka polisi katika baadhi ya maeneo ambapo alitekeleza unyama huo na baadhi ya mabaki ya watoto hao kupatikana.
Lakini baada ya kukamatwa, polisi waligundua kuwa tayari Wafula alikuwa na rekodi ya uhalifu kwani alikamatwa mwaka 2018 kwa madai ya kunajisi watoto wawili wa Kibwezi ambapo alifikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana.
4. Masten Wanjala Milimo

Chanzo cha picha, Afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kenya (DCI)
Muuaji sugu Masten Milimo Wanjala aliyesemekana kuwa na umri mdogo ikilinganishwa na wengine, alikamatwa kwa madai ya mauaji ya watoto katika jiji la Nairobi.
Wanjala alisemekana kukiri kuwanyonya damu waathirika kabla ya kuwaua.
Alidai kumuua mwathirika wa kwanza akiwa na umri wa miaka 16.
Wanjala aliuawa na raia katika eneo alikozaliwa la Bungoma baada ya kutoroka kituo cha polisi cha Nairobi.
Inasemekana aligunduliwa na raia kuwa eneo hilo baada ya kuingia uwanjani wakati wenyeji walikuwa wanacheza mpira wa soka, akatambuliwa na kufuatiliwa hadi nyumbani, ambapo alivamiwa na wananchi na kuuawa.
5. Philip Onyancha
Philip Onyancha, 32, alikamatwa baada ya kukiri kuwaua watu 17, hasa wanawake.
Alisema aliingizwa kwenye madhehebu akiwa shuleni na mwalimu, ambaye alimwambia aue watu 100 na kunywa damu yao ili aweze kuwa na bahati nzuri.
Katika harakati za kutafuta ukweli, Bw Onyancha aliongoza polisi katika ziara ya kusikitisha, akiwaonyesha maeneo ya Nairobi, Mkoa wa Kati na Rift Valley ambapo anasema aliwaua waathiriwa wake.
"Lengo langu lilikuwa kuua wanawake 100. Nilifanikiwa kuua 17 na kulikuwa na 83 bado," aliambia gazeti la Daily Nation la Kenya.
Bw Onyancha pia aliwaongoza polisi kwenye nyumba za kulala wageni za bei nafuu ambapo alikiri kuwaua makahaba kadhaa na vilevile, kuwateka nyara watoto.















