'Ikiwa Urusi itashinda, China itatufanyia vivyo hivyo': Wataiwan wanaopigana (na kufa) kwa ajili ya Ukraine

Tseng Sheng-guang alikufa mnamo Novemba wakati akipigania Jeshi la Kigeni la Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tseng Sheng-guang alikufa mnamo Novemba wakati akipigania Jeshi la Kigeni la Ukraine

Katika kanisa moja huko Lviv magharibi mwa Ukraine, mama ya Tseng Sheng-guang anamtazama kwa mara ya mwisho mwanawe ambaye amelala kwenye jeneza.

Ameandamana na jamaa wengine na watu kadhaa wa Ukraine ambao wanataka kutoaheshima zao za mwisho kwa mtu aliyekufa maelfu ya kilomita kutoka nyumbani kwake, akipigania nchi ambayo hakuwahi kuitembelea hapo awali.

“Mwanangu Sheng-guang, nataka ujue kwamba ulikuwa jasiri sana,” asema mama yake. "Utakuwa mtoto wangu daima na ninajivunia hilo."

Tseng alikuwa akipigana na Jeshi la Kimataifa la Kikosi cha Ulinzi cha Eneo la Ukraine wakati aliuawa mwezi uliopita katika mji wa mashariki wa Lyman. Alikuwa Mtaiwan wa kwanza kuuawa akiwa vitani nchini Ukraine.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya kifo chake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine ilisema Tseng "alitoa mhanga kwa ajili ya mapambano ya uhuru wa Ukraine."

Maelfu ya wanajeshi wa kigeni wamesafiri kwenda Ukraine kupigana, na idadi ya WaTaiwani kati yao ni ndogo, inakadiriwa kuwa karibu 10.

Lakini uvamizi kama wa Urusi unakodolea macho kisiwa hicho kidogo, kinachopakana na China.

China inahoji kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake na inasema kuwa itaiunganisha, hata kwa nguvu. Taiwan inajiona kama eneo huru kutoka China.

Mvutano katika eneo la bahari linalogawanya maeneo yote mawili uliongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya ziara ya mwanasiasa wa Marekani Nancy Pelosi nchini Taiwan mwezi Agosti mwaka huu, jambo ambalo liliikasirisha Beijing.

China ilijibu kwa mazoezi ya kijeshi kuzunguka kisiwa hicho.

Huduma ya kijeshi

Sammy Lin, rafiki wa karibu wa Tseng, alisema wasiwasi kuu wa kijana huyo ni kwamba siku moja, Taiwan itapatwa na hatima sawa na Ukraine: "Nakumbuka aliwaambia marafiki zake kwamba hangeweza kustahimili Waukraine wakinyanyaswa na kuuawa na Warusi."

Tseng alikuwa mmoja wa "watu sahihi zaidi" ambao alikutana nao, Lin alisema.

Mamake Tseng Sheng-guang alisafiri kuchukua mabaki ya mwanawe.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mamake Tseng Sheng-guang alisafiri kuchukua mabaki ya mwanawe.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Taiwan ina sera ya watu wanaoandikishwa kujiunga na jeshi, jambo ambalo huwafanya wale wanaokamilisha kustahiki kujiunga na Jeshi la Kigeni la Ukraine.

Jack Yao, 28, pia ni mmoja wa wale waliofanya uamuzi wa kwenda.

Aliwasili Ukraine siku tatu baada ya Rais Volodymyr Zelensky kutoa wito kwa watu wa kujitolea wa kigeni kujiunga na vita vya Ukraine, wakisafiri kutoka Taipei hadi Poland na kisha hadi mji mkuu wa Kyiv.

"Nilikuwa nikiangalia hali hiyo tangu mwaka jana, haswa kwa Warusi wakihamisha wanajeshi na vifaru hadi kwenye mpaka wa Ukraine. Hakuna aliyeamini kuwa inaweza kutokea," aliambia BBC.

"Hali ya Taiwan na kile kinachotokea huko ni sawa. Nilikuwa nikifikiria juu ya nini ningefanya kusaidia Ukraine," aliongeza.

Alijiunga na Jeshi la Kigeni la Georgia na kupokea majukumu ya karibu ya upelelezi wa mapigano. Alipofika, Warusi walikuwa bado wanajaribu kuteka mji Kyiv.

"Kulikuwa na mashambulizi kadhaa kwa makombora na mabomu wakati Warusi walikuwa Bucha," anasema, akimaanisha mji wa kaskazini mwa mji mkuu.

"Nilikuwa na misheni, na niliwaona watu wetu wakiuawa katika mlipuko. Bomu lililipuka karibu mita 50 nyuma yao."

Wakati wa burudani, aliweza kujadili hali ya Taiwan na wanachama wa kitengo chake. "Mvulana mmoja alikuwa ameishi Taiwan kwa miaka miwili na alijua hali hiyo.

Taiwan na Ukraine ni kama ndugu kwa 100%. Walikuwa wakiniambia kuwa siwezi kufa hapa kwa sababu nilipaswa kurudi kulinda nchi yangu. " alisema.

Jack Yao

Chanzo cha picha, Jack Yao

Maelezo ya picha, Jack Yao - nchini Poland - alijiandikisha kupigana nchini Ukraine siku tatu tu baada ya Rais Zelensky kuwaalika watu kupigania nchi yake.

Wakati Yao amerejea kwenye biashara yake ya kahawa nchini Taiwan, wengine wanasalia nchini Ukraine. Katika video ya hivi majuzi ya shirika la kutoa misaada la Kiukreni, WaTaiwani wawili walielezea sababu zao za kukaa katika eneo la mapigano."Sababu kuu tuliyokuja hapa ilikuwa kulinda usalama wa Waukraine," wanasema huku wakiinua bendera ya Taiwan.

"Pia tunahofia kwamba ikiwa Urusi itashinda, China itafanya vivyo hivyo huko Taiwan. Kwa hiyo tuko tayari kuja Ukraine, kutoa maisha na uhuru wetu kwa ajili ya usalama wa watu wa hapa." Bado, sio WaTaiwani wote waliokwenda Ukraine walikuwa na motisha za kijiografia.

Mnamo Juni, Li Chenling aliiambia idhaa ya BBC ya Kichina kwamba alikuwa huko kwa sababu alitaka kuishi maisha "ya kukumbukwa". Ameongeza kuwa iwapo Taiwan itavamiwa, nia yake ya kupigana itategemea mwitikio wa serikali zote mbili za Taiwan na Marekani.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema mara kwa mara serikali yake itailinda Taiwan kutokana na uwezekano wa shambulio la China. Hata hivyo, msimamo rasmi wa Washington ni moja ya "utata wa kimkakati": haijitolea kuitetea Taiwan, lakini haiondoi chaguo pia.

Mwezi uliopita, Rais Biden alisema haamini kwamba uvamizi wa China dhidi ya Taiwan ulikuwa karibu. Alisema hayo baada ya kukutana ana kwa ana na Rais wa China Xi Jinping kabla ya mkutano wa G20 mjini Bali.

WaTaiwan wana misimamo na mitazamo tofauti juu ya uwezekano wa migogoro, anasema Paul Huang wa Jukwaa la Maoni ya Umma la Taiwan.

"Inafurahisha, lakini watu wengi zaidi wanaonekana kuashiria kuwa hawajali," aliiambia BBC.

"Kama tulivyoona huko Ukraine, wasiwasi walio nao watu kuhusu tukio fulani hauathiri kwa vyovyote uwezekano wa tukio hilo kutokea, wala haimaanishi kiwango cha maandalizi," alisema.