Kithure Kindiki sasa ndiye Naibu Rais mteule

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Bunge la Kitaifa limeafiki uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mteule wa Kenya baada ya jina lake kuwasilishwa na Rais William Ruto. Wabunge 236 walipiga kura ya 'Ndiyo' kuafiki uteuzi wa Kindiki .

Jina lake sasa litawekwa katika gazeti rasmi la serikali na kisha kuapishwa kuanza kuhudumu kama Naibu Rais .

Katiba inasema pindi rais anapowasilisha uteuzi kwenye Bunge, wabunge watapiga kura ya kulikataa au kuliidhinisha jina hilo. Pia hakuna sharti la kura ya thuluthi mbili.

“Prof. Kindiki, ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, atahitaji idhini kutoka kwa Bunge la Kitaifa kabla ya kushika nafasi ya Naibu Rais. Bunge lazima lipigie kura uteuzi ndani ya siku 60 baada ya kupokea jina hilo.

Baada ya kuidhinishwa, mteule atateuliwa rasmi na Rais kuwa naibu wake. Ingawa Katiba haijaweka bayana muda wa uteuzi huu, unatarajiwa kutokea mara baada ya kuidhinishwa na Bunge.

Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto lakini hatimaye akaamua kumchagua Gachagua.

Baadaye alielezea kwamba alimchagua Gachagua kwa sababu ya umri wake na alifikiri wangeelewana zaidi.

Mwanzoni mwa kuondolewa kwa Gachagua, kulikuwa na mazungumzo ya Kindiki kuwa ndiye anayefuata kuchukua nafasi yake.

Bunge la Seneti lilipiga kura ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua kufuatia mchakato wa siku mbili uliohusisha ushahidi wa kina .

Gachagua aliondolewa baada ya Maseneta kuunga mkono sababu tano kati ya kumi na moja zilizowasilishwa na Mbunge wa kibwezi kaskazini Mwinge Mutuse.

Mfahamu Profesa Kithure Kindiki

Abraham Kithure Kindiki alizaliwa tarehe 17 Julai 1972) na ni mwanasiasa na wakili wa Kenya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Serikali ya Kitaifa.

Aliwakilisha Kaunti ya Tharaka-Nithi katika Seneti ya Kenya kuanzia 2013 hadi 2022.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2013 na kuchaguliwa tena mwaka wa 2017.

Alikuwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti katika kipindi cha 2013-2017 na Naibu Spika wa Seneti kuanzia Agosti 2017 hadi 2020.

Akiwa wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Prof. Kindiki alipata shahada ya Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Moi na Diploma ya Mafunzo ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya.

Pia ana Shahada ya Uzamili katika Sheria ya Kimataifa ya Haki za Kibinadamu na Demokrasia na Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kimataifa, kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini.

Mapema katika taaluma yake, Prof. Kindiki alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi.

Pia aliwahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alipanda hadi kuwa Muhadhiri Mshiriki katika Shule ya Sheria katika taasisi hiyo hiyo.

Pia aliwahi kuwa Katibu wa Uwiano wa Kitaifa chini ya Rais Mwai Kibaki.

Msomi huyo mashuhuri katika sheria za Kimataifa na haki za binadamu, amewahi kuwa mshauri wa mashirika ya ndani na kimataifa ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) miongoni mwa mengine.

Yeye ni mwanachama wa Baraza kuhusu Mfumo wa Umoja wa Mataifa (ACUNS), Chama cha Kimataifa cha Utafiti wa Uhamiaji wa Kulazimishwa (IASFM), Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) na Tume ya Kimataifa ya Wanasheria, Kenya (ICJ- K).