Njia ndefu yenye gharama ambayo meli kubwa za mizigo lazima zichukue ili kuepuka mashambulizi katika Bahari ya shamu

Chanzo cha picha, Alamy
Januari 17, MV Genco Picardie, ya Marekani, ilishambuliwa na Houthi katika Bahari ya Shamu; mojawapo ya njia ya baharini yenye shughuli nyingi na bila shaka ndiyo njia hatari zaidi kwa sasa.
Tangu Novemba, kundi la waasi la Yemen limeshambulia meli zinazopita kwenye Mlango wa Bab al-Mandab, njia yenye upana wa kilomita 32 inayotenganisha Afrika kaskazini na Peninsula ya Uarabuni.
Wafanyakazi wa meli ya MV Genco Picardie, hawakujeruhiwa na waliweza kuzima moto uliosababishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani.
Njia Ndefu yenye Gharama

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Takriban 12% ya biashara ya kimataifa hupitia Bahari ya Shamu kila mwaka, ni zaidi ya dola za kimarekani trilioni 1. Lakini kampuni nyingi za usafirishaji zimeanza kukwepa eneo hilo.
Mamia ya meli kubwa za mizigo, zingine zikiwa na urefu wa zaidi ya mita 300, sasa zinachagua njia ndefu ya kuzunguka bara la Afrika badala ya kuelekea Bahari ya Shamu na Mfereji wa Suez katika safari yao kutoka Asia kuelekea Ulaya.
Kwingineko, ukame mkali unaokumba Mfereji wa Panama na vita nchini Ukraine - ambavyo vimezuia usafirishaji wa nafaka katika Bahari Nyeusi - pia vinatatiza minyororo ya usambazaji wa kimataifa.
Operesheni za kijeshi za Marekani na Uingereza zenye lengo la kulinda meli na kuwazuia Wahouthi pia zilianza mwezi Novemba.
Mizigo inayobebwa na meli hizi inaweza kuwa na thamani ya mamilioni au hata mabilioni ya dola. Kwa hivyo haishangazi, kampuni za usafirishaji kuamua kupita njia zingine.
Hata hivyo, kuzunguka Rasi ya Afrika Kusini, huongeza takriban maili 3,500 za baharini (kilomita 6,500) na siku 10 hadi 12 za kusafiri kwa kila safari.
Safari hizo huhitaji mafuta ya ziada (yenye thamani ya dola milioni 1 kwa makadirio), marekebisho ya ratiba za uwasilishaji na kuongezeka kwa gharama.
Lakini kampuni nyingi zinafanya uamuzi huu badala ya kuhatarisha kushambuliwa na makombora na watekaji nyara.
Gharama kwa Watumiaji

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anna Nagurney, mwanauchumi kutoka Chuo Kikuu cha Massachusetts, anasema, "meli zimewahi kuzunguka Kusini mwa Afrika hapo awali, kwa sababu tofauti. Na katika kesi hii, kwa kuzingatia idadi kubwa ya bidhaa, kwa kweli hakuna njia mbadala.”
Msemaji wa Maersk, mojawapo ya makampuni kubwa ya meli duniani, anasema kuna ukomo kwa kiasi cha bidhaa zinazoweza kusafirishwa kutoka baharini hadi kwenye treni au ndege, kutokana na wingi wa mizigo ambayo meli zinaweza kubeba.
‘Hata hivyo, hali mbaya ya hewa wakati mwingine inayozikabili meli zinazosafiri kuzunguka kusini mwa Afrika inamaanisha chaguo hili lina hatari pia,’ aliongeza Nagurney.
“Kampuni zinazohusika na usafirishaji zina uzoefu wa kupata bidhaa zinakohitaji kwa njia moja au nyingine, na minyororo ya usambazaji bidhaa ulimwenguni,” anasema Wiese Bockmann, mtaalamu wa ngazi ya juu wa kampuni ya Lloyd's List Intelligence, inayohusika na biashara ya baharini.
Hii ndiyo sababu mtaalam huyo anasema mgogoro wa sasa wa Bahari ya Shamu haupaswi kuchukuliwa kuwa ndio kiama cha kwa sekta ya meli.
Hii haina maana kwamba mabadiliko ya njia kwa meli kubwa za mizigo hayana madhara. Kulingana na ripoti, gharama zilizoongezeka zinaweza kuathiri watumiaji.
Swali kuu ni kwamba mgogoro wa Bahari ya Shamu utaendelea kwa muda gani. Kampuni za usafirishaji na wataalamu, wanasema unaweza kudumu kwa miezi kadhaa.
Uchafuzi wa Mazingira

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tunapaswa pia kufikiria juu ya athari kwa mazingira. Ongezeko la ghafla la safari za meli linaweza kusababisha kelele kubwa chini ya maji, ambazo zinaweza kuathiri idadi ya samaki na mamalia wa baharini.
Zaidi ya hayo, meli zinazosafiri maelfu ya maili zitatumia mafuta mengi zaidi na kutoa kaboni zaidi angani wakati wa safari.
Mwaka 2023, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Bahari liliweka malengo kuhusu uzalishaji wa gesi chafuzi kufikia 2050, ya kupunguza uzalishaji kwa angalau 20% ifikapo 2030.
"Ikiwa hili litaendelea, lengo lake la kupunguza uzalishaji wa hewa chafu mwaka huu halitofikiwa," alikiri Rico Luman, mtaalam wa uchukuzi katika kampuni ya huduma za benki na fedha ya ING.
Mtaalamu huyo anadokeza kwamba meli za mafuta zinasafiri kilomita nyingi tangu vita vya Ukraine kuanza, na vikwazo dhidi ya Urusi vimesababisha ukarabati wa njia nyingi za baharini. Matokeo yake baadhi ya meli zinazalisha kiwango kikubwa cha hewa chafu.
Kilicho wazi, ni kwamba mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya biashara ya kimataifa hayataharibu minyororo ya usambazaji. Lakini ni tishio kubwa kwa biashara na mabaharia ambao maisha yao yanasalia hatarini.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalllah












