UN yalaani shambulio hatari la angani katika gereza la Yemen

Maelezo ya video, Watu wamekuwa wakiwatafuta manusura vifuzi vya gereza hilo

Umoja wa Mataifa umelaani shambulizi la anga dhidi ya kituo kimoja cha mahabusu nchini Yemen na kuua zaidi ya watu 70.

Kituo hicho kilichopo katika mji wa Saada, ambao ni ngome ya waasi wa Kihouthi kaskazini -magharibi mwa Yemen, kilishambuliwa siku ya Ijumaa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yake alisema "makabiliano yanapaswa kukomeshwa".

Katika taarifa siku ya Jumamosi, muungano unaongozwa na Saudi Arabia - kupigana na waasi wa Houthi nchini humo walipinga kutekeleza shambulio hilo la angani.

Muungano huo pia ulisema eneo hilo liko katika orodha ya maeneo ambayo hayapaswi kushambuliwa kama ilivyofikiwa katika makubaliano na Umoja wa Mataifa na haikuwa imeripotiwa na shirika la Msalaba mwekundu.

Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Saudia-vimekuwa vikipigana na waasi wa Kihouthi tangu mwaka 2015. Maelfu ya raia wakiwemo zaidi ya watoto 10,000, wameuawa na wengine kujeruhiwa kutokana na vita hivyo.

Mamilioni ya watu wanasemekana kusambaratishwa na huku wenine wengi wakikabiliwa na tishio la njaa.

Saa kadhaa baada ya shambulio la angani, wahudumu wa uokozi bado wanatoa miili kwenye vifusi, huku matumaini ya kupata manusura ikiendelea kudidimia, anasema mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati, Anna Foster.

Idadi kamili ya waliofariki haijabainika. Shirka la kutoa msaada wa kimatibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) linasema karibu watu 70 waliuawa, ijapokuwa idadi ya waliofariki inatarajiwa kuongezeka.

Televisheni inayoendeshwa na Wahouthi ilionyesha wanaume wakiondoa vifusi kwa mikono yao katika eneo la tukio na waliojeruhiwa wakiwa hospitali ya eneo hilo. MSF ilisema hospitali moja imepokea zaidi ya majeruhi 200.

"Bado kuna miili mingi katika eneo la lililoshambuliwa, baadhi ya watu hawajulikani walipo," Ahmed Mahat, Mkuu wa MSF nchini Yemen, aliambia shirika la habari la AFP. "Ni vigumu kujua ni watu wangapi waliuawa. Inaonekana ilikuwa kitendo kibaya sana cha ghasia.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken pia alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.

Matumaini ya kupata manusura kwenye vifusi yanasemekana kufifia

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Matumaini ya kupata manusura kwenye vifusi yanasemekana kufifia

Katika maeneo ya kusini, watoto watatu waliuawa walipokuwa wakicheza kandanda wakati shambulizi la anga lilipopiga kituo cha mawasiliano katika mji wa bandari unaodhibitiwa na waasi wa Hudaydah, shirika la misaada la Save the Children lilisema.

Karibu na nchi nzima ilikumbwa na hitilafu ya mtandao, hali ambayo vyombo vya habari vya Houthi vilihusisha na shambulio dhidi ya kituo cha mawasiliano.

Saudi Arabia ilisema kuwa muungano huo ulifanya mashambulizi ya anga huko Hudaydah.

Muungano huo umeongeza mashambulizi ya angani tangu waasi wa Houthi wafanye shambulio la nadra la ndege zisizo na rubani na makombora katika UAE siku ya Jumatatu. Raia watatu waliuawa katika shambulio la kwanza la aina yake katika emirates.