Mfahamu Mussa Azzan Zungu

Chanzo cha picha, BUNGE TANZANIA
Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu ndiye Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimwanasiasa mkongwe na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika siasa na utumishi wa umma.
Mnamo Novemba 11, 2025, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akipokea kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge.
Uteuzi wake ulifanyika kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku Spika aliyekuwepo , Dk. Tulia Ackson, kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Kwa ushindi huo, Zungu aliandika historia kama Spika wa nane wa Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwake, akifuata nyayo za viongozi mashuhuri kama vile Adam Sapi Mkwawa, Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anna Makinda, Job Ndugai na Dk. Tulia Ackson.
Elimu na Maisha ya Awali
Zungu alianza safari yake ya kielimu katika Shule ya Msingi St. Joseph's (sasa inaitwa Forodhani) jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1958 na 1965. Baada ya hapo aliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Kinondoni (1966-1967) na baadaye Shule ya Tambaza (1968-1969).
Akiwa mwanafunzi, alianza kushiriki katika shughuli za kisiasa kupitia chama cha TANU, ambapo aliongoza tawi la chama shuleni.
Baada ya masomo ya sekondari, Zungu alihamia Toronto, Canada, ambako alisomea stashahada ya ufundi wa vyombo vya anga na urubani.
Alifanya kazi nchini humo kama mhandisi wa ndege hadi mwaka 1982, kisha akaendelea kufanya kazi katika Falme za Kiarabu hadi mwaka 1993 kabla ya kurejea nyumbani Tanzania.
Safari ya Kisiasa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Zungu alirejea rasmi kwenye siasa mwaka 2000, ambapo alichaguliwa kuwa diwani wa Kata ya Mchikichini kupitia CCM, ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa Naibu Meya wa Ilala.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilala, nafasi aliyoendelea kuishikilia kwa vipindi vitano mfululizo hadi mwaka 2025.
Ndani ya Bunge, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo: Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje (2007-2011), Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola (CPA) -Tanzania, alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii (2015-2018)
baadaye akawa Mwenyekiti wa Bunge katika vipindi vya 2012 na 2016. Mwaka 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi aliyohudumia hadi mwisho wa kipindi cha Bunge la 12.
Kufuatia kujiuzulu kwa Spika Job Ndugai, Zungu alichaguliwa kuwa Naibu Spika, kabla ya kupanda ngazi hadi kuwa Spika wa Bunge la 13 mwaka 2025.
Uzoefu wake ni mkubwa na misimamo yake kisiasa huenda ikaleta utofauti wa kimaamuzi, ingawa wengi hawaoni tofauti kubwa atakayoileta kwenye bunge la sasa na machoni mwa walio nje ya bunge.















